Tuesday, October 27, 2020

MWENYE TIKETI YA MBELGIJI SIMBA NI HUYU

Must Read

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya...

Afua Suleiman afunguka ‘Utalijua Jiji’ ilivyompa ustaa mjini

NA JEREMIA ERNEST JINA alilopewa na wazazi wake ni Afua Suleiman na hata alipojitupa...

NA AYOUB HINJO


MAISHA yanaonekana kwenda kasi katika mitaa ya Msimbazi, unajua kwanini? Mambo yaliyotokea hivi karibuni yalionekana kushusha morali kwa timu hiyo, huku mashabiki na wanachama wakiwa na wasiwasi mkubwa.

Lakini ukiacha hilo, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, amekuwa katika wakati mgumu kwenye mazoezi ya timu hiyo yanayofanyika Uwanja wa Boko Veterans, Dar es Salaam kwa kuendelea kuinoa vikali safu ya ushambuliaji ambayo inaonekana kusuasua.

Baada ya michezo saba ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuchezwa na klabu hiyo, ni mabao nane tu yalifanikiwa kufungwa huku wakikosa nafasi nyingi zinazotengenezwa.

Msimu uliopita, Simba ilikuwa hatari kwa kupachika mabao huku wakibadili kila nafasi iliyotengenezwa kuwa bao na kuwafanya mashabiki wao kuishi katika kilele cha furaha ambayo iliwapelekea kutwaa ubingwa baada ya misimu mitano kupita.

Msimu uliopita ulipomalizika, Simba walifanikiwa kufunga mabao zaidi ya 50 na kuwa timu iliyopachika mabao mengi zaidi ya klabu yoyote.

Siri ya mabao ya Simba msimu uliopita, ilibebwa na nahodha wa kikosi hicho, John Bocco, mwenye urefu na kasi kubwa pindi anapokaribia lango la wapinzani, huku akisifika kwa kufunga mabao kwa kichwa.

Unajua kwanini Bocco? Msimu uliopita, Emmanuel Okwi, aliyechukua kiatu cha dhahabu kwa ufungaji bora, alipachika mabao 20 akiwa kando ya nahodha huyo aliyetwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa klabu hiyo.

Tangu kuanza kwa msimu huu, Okwi hakupata nafasi kubwa ya kucheza kutokana na majeraha aliyoyapata katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Mtibwa Sugar uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Kukosekana kwa Okwi, kulitoa fursa kwa straika mpya, Meddie Kagere, kucheza sambamba na Bocco, huku akifanikiwa kufunga mabao manne mpaka sasa, kando ya mpachika mabao huyo wa zamani wa Azam FC.

Kuna tofauti kubwa inaonekana pindi Bocco anapokosekana uwanjani, michezo miwili aliyokosa mpaka sasa, kombinesheni ya Okwi na Kagere imezalisha bao moja pekee lililopachikwa katika mchezo dhidi ya African Lyon kabla ya suluhu na Yanga.

Katika mchezo mwingine, Bocco alitokea benchi kuchukua nafasi ya Okwi dhidi ya Mtibwa Sugar, ukiwa ni mchezo wa Ngao ya Jamii ambao Kagere alifanikiwa kufunga bao moja kati ya mawili yaliyopachikwa kimiani na Simba.

Kwa kiasi fulani, Okwi na Kagere wanafanana katika uchezaji wao, mikimbio na kujipanga kwao hakutofautiani sana. Kutokana na hali hiyo, mara kadhaa ilisababisha wachezaji hao kukutana sehemu moja wakiwa wamefuata mpira.

Nyota hao wawili wa kimataifa, wote wamenufaika na uwapo wa Bocco ambaye mpaka sasa amepachika mabao mawili katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwa kiasi kikubwa, mafanikio ya safu ya ushambuliaji ya Simba, yapo katika mabega ya Bocco ambaye haimbwi sana na mashabiki wa timu hiyo kama ilivyo kwa wenzake hao wawili.

Mastraika hao watatu walicheza pamoja msimu huu katika mchezo dhidi ya Ndanda uliomalizika kwa suluhu ndani ya Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara na kuzua maswali mengi kama inawezekana kuwatumia wote kwa pamoja.

Uchezaji wa Bocco ni tofauti na Okwi au Kagere, mara nyingi husimama katika eneo la wapinzani kuvizia mipira itakayopelekwa eneo hilo huku akionekana kuwa mwepesi kutengeneza nafasi za mabao kwa wengine.

Uwezo huo aliokuwa nao Bocco, unatumiwa vizuri na wachezaji wanaomzunguka kama ilivyoonekana kwa Okwi aliyepachika mabao 20 msimu uliopita na Kagere aliyeweka kambani manne mpaka hivi sasa.

Kila mmoja amenufaika kwa wakati wake kando ya nahodha huyo, inawezekana kwa wachezaji watatu kucheza pamoja ikiwa kama watapata michezo mingi kwa pamoja na kutengeneza kombinesheni ya utatu.

Kwa kifupi, ni ukweli usiopingika kuwa Bocco ndiye mambo yote katika suala zima la mabao Simba.

Hivyo, iwapo mshambuliaji huyo atakuwa fiti na kupewa nafasi kila mechi, ndiye atakayempa heshima Mbelgiji Aussems kwani atakiwezesha kikosi chake kuvuna mabao kila mechi watakayoshuka dimbani na hatimaye kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Lakini iwapo Bocco hatakuwapo katika mipango ya Aussems, ni wazi straika huyo atakuwa amehatarisha kibarua cha Mbelgiji huyo ndani ya Wekundu wa Msimbazi hao.

Kazi kwake Aussems, aombe Mungu Bocco awe fiti siku zote na kuwa mbali ya wimbi la majeruhi kwani ni wazi mshambuliaji huyo ndiye aliyeishika tiketi ya ndege ya kocha wake huyo.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya kinda wa zamani wa timu...

Afua Suleiman afunguka ‘Utalijua Jiji’ ilivyompa ustaa mjini

NA JEREMIA ERNEST JINA alilopewa na wazazi wake ni Afua Suleiman na hata alipojitupa kwenye ulimwengu wa muziki wa...

Keche: Kundi maarufu Ghana linalowatamani Diamond, Kiba, Harmonize

JIACHIE na Staa Wako, wiki hii tumetua mpaka Accra, Ghana kwa kundi maarufu la muziki nchini humo, Keche linofanya vizuri na ngoma...

Katwila: Sitaidharau Mbeya City

NA VICTORIA GODFREY KOCHA wa timu ya Ihefu, Zuberi Katwila, amesema hawaraidharau  Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -