LONDON, England
BADO uongozi wa Arsenal wako kwenye mazungumzo ya mkataba na nyota wao Alexis Sanchez na Mesut Ozil.
Wamebakiza miezi 18 kwenye mikataba yao ya sasa na tayari klabu mbalimbali zimeanza kuwamezea mate ikiwa mazungumzo kati yao na Arsenal yakikwama.
Lakini umeshawahi kujiuliza kati ya Ozil na Sanchez nani ni muhimu katika kikosi cha Arsenal? Makala haya yanakupa tathmini fupi katika kutafuta jibu la swali hili.
Kwanini ni Alexis
Sky Bet Championship,Today, 22:45pm
Norwich v Huddersfield
£20 Free Bet, No Deposit Needed
Sanchez
Sanchez amekuwa na maendeleo mazuri tangu alipotua Arsenal akitokea Barcelona mwaka 2014 kwa dau la pauni mil 35 na msimu huu amezidi kuwa moto zaidi.
Maamuzi ya Arsene Wenger kumpanga Sanchez straika wa kati imeonekana kulipa zaidi kuliko alivyokuwa akimpanga pembeni ya uwanja.
Mpaka sasa, Sanchez anafukuzana na straika wa Chelsea, Diego Costa, kwenye orodha ya wafungaji bora akitupia mabao 12 na kufikisha idadi ya mabao 56 kwenye michezo 116 aliyocheza tangu atue Emirates.
Ubora wa Sanchez hauko tu kwenye ufungaji, ana kasi, chenga na uwezo wa kukokota mpira unamfanya awe mchezaji hatari kwenye kikosi cha Arsenal.
Msimu huu ametengeneza nafasi 42 na kupiga asisti 5, hakuna mchezaji wa Arsenal aliyepiga asisti nyingi zaidi yake.
Kasi yake imekuwa msaada mkubwa katika kutengeneza njia za mabao kwenye safu ya ushambuliaji ya Arsenal.
Yeye ndiye mchango kwa Mesut Ozil na Theo Walcot kuingia katikati na kufunga mabao. Ni mpambanaji na panapohitaji matumizi ya nguvu Sanchez huwa tayari kujitoa.
Kwa msimu huu ni wazi kuwa Sanchez ndiye kiongozi wa safu ya ushambuliaji katika kikosi cha Arsenal, amefunga na kutengeneza nafasi za kutosha. Unaachaje kutambua mchango wake linapokuja suala la mkataba?
Kwanini ni Mesut Ozil
Wakati tukiujadili ubora wa Sanchez, hatutakiwi kusahau kipaji kikubwa cha soka Mungu alichokiweka katika mwili wa Mesut Ozil.
Fundi huyu wa mpira kutoka Ujerumani si mzuri kwenye kugombea mpira, hawezi purukushani. Mpira wake unaishi kwenye kichwa chake, huyu ndiye Ozil.
Ubora wa Ozil hauhitaji mjadala. Kocha wake, Arsene Wenger alikaririwa msimu uliopita akieleza ubora wa Ozil akisema: “Kama unapenda kuangalia mpira lazima utapenda kumtazama Ozil.”
Kocha wa sasa wa Man United, Jose Mourinho, wakati akiwa Real Madrid alisema: “Ozil ni mchezaji wa kipekee sana, hakuna mfano wake tena duniani.”
Ni fundi wa kupiga pasi, kupiga asisti na kutengeneza mashambulizi. Yeye ndiye injini ya mafanikio ya Sanchez kwa kutengeneza nafasi kwenye boksi, Ozil ndiye mwenye kuifanya Arsenal icheze soka safi unaloliona hivi sasa.
Msimu uliopita aliifikia rekodi ya asisti nyingi kwenye Premier League kwa kutoa asisti 19 na msimu huu ni kama amebadili mawazo yake kwenye ufungaji.
Bao la kiufundi alilofunga kwenye pambano dhidi ya Ludogorets mwezi Novemba, Arsenal ikishinda 3-2 lilitosha kuwakumbusha mashabiki wa soka yale yaliyokuwa yakifanywa na Dennis Bergkamp.
Mpaka sasa ameweka kambani mabao 9 kwenye michezo 20 aliyocheza na kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Arsenal.
Oktoba mwaka huu, alifikisha miaka 28 na hii ni ishara yuko kwenye kiwango bora kabisa katika maisha yake ya soka na kama akiendelea hivi huenda huu ukawa msimu bora zaidi kwa Ozil.
Umuhimu wake uwanjani ndio humfanya wakati mwingine Arsene Wenger kushindwa kumfanyia ‘sub’, hucheza kwa dakika zote anazopangwa uwanjani.
“Unachotakiwa kufanya ni kumtazama tu usoni mara moja kisha kimbia, lazima aulete mpira miguuni kwako,” aliwahi kukaririwa akisema Theo Walcott.