Tuesday, October 27, 2020

Nasubiri kuona ‘unafiki’ wetu kwa Serengeti Boys

Must Read

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya...

NA HASSAN DAUDI

HATIMAYE timu ya soka ya taifa ya vijana walio chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, imeshindwa kukata tiketi ya kushiriki Fainali za Mataifa Afrika kwa umri huo zitakazofanyika mwakani nchini Madagasca.

Ni historia nyingine mbaya kwa Tanzania hasa baada ya kaka zao Taifa Stars kuchemsha kwenye mbio za kuwania nafasi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika mwakani nchini Gabon.

Serengeti wamefeli kutinga kwenye mashindano hayo baada ya kuambulia kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa wenyeji Congo Brazzaville.

Matokeo hayo yanakuja ikiwa ni wiki chache tangu Serengeti Boys walipoibuka na ushindi wa mabao 3-2 katika mchezo wa awali uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Congo wameitupa nje Serengeti Boys kutokana na faida ya mabao mawili waliyoyapata ugenini huku wakifanikiwa kuwazuia vijana hao wa Tanzania kutikisa nyavu zao.

Hata hivyo, kabla ya kuvaana na Congo, Serengeti Boys waliiondoa Afrika Kusini ikiwa ni baada ya kusitisha safari ya timu ya visiwa vya Shelisheli.

Shelisheli walikumbana na makali ya Serengeti Boys baada ya kuondoshwa kwenye mshindano kwa jumla ya mabao 9-0.

Wasauzi nao waliambulia sare ya bao 1-1 wakiwa kwao kabla ya kuchapwa mabao 2-1 na vijana hao wa Kitanzania.

Ni wazi kabisa kuwa mbio za vijana hao wa kocha Bakari Shime ‘Mchawi Mweusi’ katika kufukuzia safari ya Madagasca zilikuwa za kuvutia mno, inatia moyo na kufufua matumaini ya soka letu.

Hata hivyo, kipo kilichonisukuma kuandika makala haya hasa baada ya Serengeti Boys kukosa nafasi hiyo ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo ya kimataifa.

Hakuna asiyekumbuka kile kilichoikuta timu yetu ya vijana wenye umri wa miaka 17 mwaka 2004.

Kwa wasiokuwa na kumbukumbu ya kile kilichotokea, hicho ndicho kipindi ambacho Watanzania wengi walikuwa na majonzi makubwa kutokana na kile kilichoitokea timu yao ya Serengeti Boys.

Baada ya juhudi kubwa ikiwemo kuwafunga Zimbabwe katika mchezo wa mwisho na hatimaye kufuzu fainali hizo zilizofanyika mwaka mmoja baadaye, Serengeti Boys walikumbana na rungu la Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf).

Baada ya kujiridhisha na ushahidi uliotokana na uchunguzi wa kina, ilibainika kuwa staa wa Serengeti Boys, Nurdin Bakari, alikuwa na umri wa miaka 23 badala ya 17.

Ikumbukwe kuwa ni katika kipindi hicho ndipo Nurdin aliposajiliwa na Simba SC ambako taarifa zake za uhamisho zilionesha kuwa ana umri wa miaka 23.

Kutokana na kosa hilo la kudanganya umri, Serengeti Boys waliokuwa wakinolewa na kocha Abdallah ‘King’ Kibadeni na msaidizi wake marehemu Silvester Marshi, walijikuta wakipokonywa nafasi ya kucheza michuano hiyo ya Gambia.

Wengi wanaamini kuwa kikosi kile kingefanya vyema Gambia na mwishowe kuiweka Tanzania kwenye ramani ya soka barani Afrika na ulimwenguni kote.

Licha ya kufuta ndoto hizo, pia Tanzania ilifungiwa kushiriki michuano ya vijana wenye umri huo kwa kipindi cha miaka mitatu.

Nafasi ya Serengeti Boys nchini Gambia ilichukuliwa na Zimbabwe ambao hata hivyo hawakuchukua taji hilo lililobaki kwa wenyeji baada ya kuchomoza na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa fainali dhidi ya Ghana.

Huo ndio ukawa mwisho wa sapoti ya Serikali na wadau wa mchezo wa soka kwa vijana hao, wakasahaulika na kutelekezwa. Hakuna aliyetaka kujua wanaishi vipi, wapi na nini hatima yao katika mchezo wa soka.

Baada ya miaka kadhaa kama wasemavyo waswahili kuwa siku hazigandi, mashabiki wa soka wakajisahau na kuanza kuwashangilia akina Athumani Iddi ‘Chuji’, Nurdin, Amir Maftah na wengineo ambao waliibukia kwenye timu za Ligi Kuu Bara zikiwemo Simba na Yanga.

Mbali na Nurdin, Chuji, ambao waliichezea Simba kabla ya kujiunga na mahasimu wao Yanga, wengine waliotokea Serengeti Boys hiyo na kuwika ligi kuu ni aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Hassan Bwaza, Patrick Mangungulu, Julius Mrope, Juma Jabu, Omari Matuta na Yusuf Mgwao ‘Wanchope’.

Licha ya kuwapotezea walipotupwa nje ya mashindano ya Gabon, sasa walionekana ‘malaika’ walipokuwa na jezi za Simba, Yanga, Moro United na klabu nyingine.

Kwa jinsi walivyofungiwa vioo baada ya sakata la Nurdin, ukweli ni kwamba kama si juhudi zao binafsi katika kufukuzia ndoto zao, basi wasingeonekana tena kwenye ulimwengu wa soka, wangekwishapotea.

Kwa kuiangalia ‘performance’ ya kikosi cha sasa cha Serengeti Boys, hakijatofautiana sana na kile cha miaka 12 iliyopita kilichokuwa na akina Chuji.

Chini ya kocha Shime vijana hao wameonesha kuwa wanaweza kufanya makubwa katika harakati za Tanzania kujiweka katika ramani ya ulimwengu wa soka.

Niipongeze Serikali kwa kudhamini safari ya Serengeti Boys kwenda kuweka kambi nchini Madagasca kujiandaa na mchezo wa kwanza dhidi ya Congo.

Lakini je, kushindwa kwao kukata tiketi ya kwenda Madagasca ndiyo wamejichongea kama ilivyokuwa kwa wale wa mwaka 2004?

Tumejipanga vipi kuepuka unafiki wetu wa kuwasusa wachezaji wa Serengeti Boys katika kipindi hiki walichofeli, huku tukisubiri miaka kadhaa ijayo ili tuwashangilie wakiwa na jezi za klabu zetu?

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika ujumbe kupitia ukurasa wake wa...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya kinda wa zamani wa timu...

Afua Suleiman afunguka ‘Utalijua Jiji’ ilivyompa ustaa mjini

NA JEREMIA ERNEST JINA alilopewa na wazazi wake ni Afua Suleiman na hata alipojitupa kwenye ulimwengu wa muziki wa...

Keche: Kundi maarufu Ghana linalowatamani Diamond, Kiba, Harmonize

JIACHIE na Staa Wako, wiki hii tumetua mpaka Accra, Ghana kwa kundi maarufu la muziki nchini humo, Keche linofanya vizuri na ngoma...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -