NA MARTIN MAZUGWA,
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Donald Ngoma, ameendelea kuwaumiza vichwa wapinzani wa timu hiyo katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika, Ngaya Club de Mde ya Comoro ambao wamekuwa wakisaka mikanda yake ya video.
Ngoma ambaye anasumbuliwa na maumivu ya goti aliyoyapata katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar, hajaonekana uwanjani tangu timu yake iliporejea Dar es Salaam kuendelea na mechi za ligi.
Akizungumza na BINGWA jana, Rais wa Ngaya, Ali Mohamed, alisema wamekuwa wakikifuatilia kikosi cha Yanga kila mchezo inayocheza ili kuisoma kabla ya kukutana nayo Februari 12, mwaka huu katika Dimba la Moroni.
“Kila siku tumekuwa tukiwafuatilia Yanga katika michezo wanayocheza, tumeona karibu kikosi kizima isipokuwa mshambuliaji wao, Donald Ngoma ambaye kwa sasa tumeamua tutafuta mikanda yake tuone ubora wake,” alisema.
Alisema kuwa iwapo watapata video za nyota huyo, watakuwa wamemaliza kila kitu hivyo timu yake kuona ni vipi inaweza kuwamaliza mabingwa hao wa Tanzania Bara.