Thursday, October 29, 2020

Nini nyuma ya pazia mateso ya R. Kelly?

Must Read

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya...

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

HALI inazidi kuwa mbaya kwa staa wa R&B, Robert Sylvester Kelly, ambaye kwa mashabiki wa muziki wanamfahamu kwa jina la R. Kelly.

Wakati bado akikabiliwa na mashitaka ya udhalilishaji wa kingono dhidi ya wanawake, kesi zake zikitarajiwa kusikilizwa hapo mwakani katika mahakama za Chicago na New York, wiki iliyopita yaliibuka mapya.

R. Kelly (52), anashutumiwa kwa kosa la rushwa, kwamba alihonga kiasi cha fedha ili aliyekuwa mpenzi wake, Aaliyah, afojiwe vyeti ambavyo vingerahisisha upatikanaji wa leseni ya ndoa yao.

Waendesha mashitaka walisema wawili hao walighushi vyeti mwaka 1994 ili Aaliyah (sasa marehemu) aonekane alikuwa na umri wa miaka 18, licha kwamba alikuwa binti wa miaka 15, hivyo lilikuwa kosa kuolewa.

Msanii huyo aliyewahi kutamba na ngoma ‘Storm Is Over’, ‘Step In The Name Of Love’ na ‘I Believe I Can Fly’, amekuwa gerezani mjini Chicago kwa miezi mitano sasa, pia akitarajiwa kuumaliza mwaka 2019 akiwa huko.

Mwandishi aliyemchunguza miaka 20

Huyo ni Jim DeRogatis aliyehitimu Chuo Kikuu cha New York mwaka 1989, akianza kazi ya uandishi wa habari za uchunguzi katika Jarida la Jersey.

Akiwa anaripoti vitendo vya uhalifu na siasa, pia alikuwa akifuatilia kila kilichokuwa kikitokea katika Gereza la Hudson na huko alifichua tukio la mfungwa kuuawa kwa kupigwa risasi na mmoja kati ya maofisa wa polisi.

DeRogatis ni mwandishi wa kwanza kuripoti juu ya mateso ya kingono anayofanya R. Kelly dhidi ya wanawake, akimfuatilia mwimbaji huyo tangu mwaka 2000 hadi leo hii.

Anasema kuna wanawake takribani 48 walioharibiwa maisha na nyota huyo wa R&B, akiongeza pia huenda idadi ni kubwa zaidi.

Juu ya alivyoanza kumfuatilia R. Kelly, DeRogatis anasema alipokea ujumbe kutoka kwa mwanamke aliyeandika: “Ni tatizo alilonalo Robert (R. Kelly) na ni kitu cha miaka mingi, ni suala la wasichana wenye umri mdogo.”

Aidha, DeRogatis anasema stori yake ya kwanza juu ya malalamiko hayo ya wanawake ilichapishwa mwishoni mwa mwaka 2000 lakini ilipuuzwa kwenye soko la muziki na hata vyombo vya habari vilipotezea.

Mwandishi mwingine, Dart Adams, anasema kati ya mwaka 1996 hadi 1999, alikuwa akisikia tu, kwamba R. Kelly si mtu mzuri kama ambavyo wengi walifikiria.

Naye David Dennis, ambaye pia ni mwandishi, aliongeza: “Nafikiri stori ya kwanza ya DeRogatis iliwafanya waandishi wengi wa kike wenye asili ya Afrika kuanza kuzama ndani, kuona kile kilichokuwa kikielezwa juu ya unyama wa R. Kelly dhidi ya wanawake.”

Kwa pamoja, waandishi hao wanakubaliana kwamba licha ya R. Kelly kufikishwa mahakamani mara kadhaa, ikiwamo ile ya mwaka 2008, ilikuwa ngumu kuwaaminisha walio wengi kwa kuwa msanii huyo alikuwa kipenzi cha wengi.

Mwanzo wa majanga, mastaa walivyomkimbia

Kila kitu kilibadilika na kuwa hovyo kwa R. Kelly mwanzoni mwa mwaka huu, Januari 3. Hiyo ni baada ya video ya ‘Surviving R. Kelly’ kuwekwa hadharani.

Ndani yake, wanaonekana wanawake mbalimbali, wakisimulia namna mwanamuziki huyo alivyowafanya watumwa wa kingono kwa nyakati tofauti.

Kashifa hiyo ilisababisha baadhi ya wanamuziki wakubwa, wakiwamo Lady Gaga, Meek Mill, Jada Pinkett, John Legend, Chance The Rapper, Ne-Yo, Omarion na Celine Dion, kutangaza wazi kuwa hawatamuunga mkono R. Kelly.

Si tu Gaga alisema anajuta kufanya naye kazi, pia alisisitiza: “Nasimama kwa asilimia 1000 na wanawake (waliodhalilishwa) na nawaamini… Natamani sauti zao zingesikika na kupewe uzito.”

Kwanini mastaa wanahofia kumtetea?

Wakati akina Lady Gaga wakisema wazi kuwa wanamlaani R. Kelly, wapo mastaa wakubwa waliobaki kimya tu, licha ya waandishi wa habari kuwaomba watoe maoni yao.

Katika hao, itoshe kuwataja washikaji wawili wenye majina makubwa kwenye soko la muziki wa Hip hop, Kanye West na Jay-Z.

Ni kwamba wanahofia kile kilichomkuta mwanamitindo wa Uingereza, Cara Delevingne? Yeye alijikuta akipoteza mashabiki 100,000 aliokuwa nao kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram kwa sababu tu alimtetea R. Kelly.

Majanga yanayofanana na hayo yalimkuta pia rapa raia wa Marekani mwenye asili ya Morocco, French Montana, ambaye ‘aliyaoga’ matusi ya mashabiki wake, kisa tu alisimama upande wa mkali huyo wa R&B.

Ili kuepuka balaa hilo, ambalo kwa upande mwingine lingekuwa na athari mbaya katika biashara zake, Montana alilazimika kurudi na kauli ya kumkataa R. Kelly, akisema yuko pamoja na wanawake waliopitia udhalilishaji uliofanywa na mwanamuziki mwenzake huyo.

Baba yake Beyonce afichua siri

Akihojiwa na gazeti la Metro, Mathew Knowles, ambaye naye amemtenga R. Kelly, anarejesha kumbukumbu zake katika miaka ya 1990, wakati staa huyo alipokaribia kufanya kazi na Kundi la Destiny’s Child lililokuwa likiundwa na wadada watatu, akiwamo Beyonce.

“Nilikuwapo, na hata mke wangu wa zamani, Tina, alikuwapo. Kitu kuhusu R. Kelly ni kwamba alipenda kurekodi nyimbo usiku mkubwa.

“Na tofauti iliyokuwapo kwenye studio yake ni kwamba chumba kimoja kilikuwa na vifaa na mlango uliofuata ni klabu, ambayo ungekuta watu 40 au 50 wakicheza muziki (usiku huo). Kulikuwa na wasichana wa umri wa miaka 15 na 16…” anasimulia.

Inawezekana R. Kelly anasingiziwa?

Mwanzoni mwa mwaka 2016, utafiti wa Chuo Kikuu cha Maryland ulieleza kwamba mastaa wenye ngozi nyeusi wako hatarini nchini Marekani kwa kuwa wamekuwa wakihusishwa na matukio ya uhalifu.

Utafiti huo wa Idara ya Sosholojia chuoni hapo, ukiongozwa na msomi wa Shahada ya Uzamivu (PhD), Joanna Pepin, ulifuatilia stori 330 za mastaa 66 waliokuwa na shutuma za udhalilishaji wa kijinsia kuanzia mwaka 2009 hadi 2011.

Mambo mawili yaliibuliwa na utafiti huo. Mosi, kesi za mastaa wenye asili ya Afrika zilikuwa mara tatu zaidi ya zile za wenzao wa kizungu.

Pili, asilimia kubwa ya stori za mastaa wa kizungu zilikuwa na utetezi ndani yake, ikiwamo kuelezwa walifanya hivyo wakiwa na hasira au wamelewa, tofauti na zile zilizowahusu watu weusi.

Mbali ya utafiti huo, madai ya mastaa wenye asili ya Afrika wanavyofanyiwa ukatili na vyombo vya habari vya Marekani, yaliwahi kuibuliwa mwaka 1991.

Mwanasiasa mwenye ngozi nyeusi, Clarence Thomas, alifika mbele ya Kamati ya Seneta kujitetea dhidi ya tuhuma za kumnyanyasa kingono mwanamke wa kizungu aitwaye Anita Hill.

Thomas alisema wazi kwamba Marekani haitaki kuona mtu mweusi akishika nyadhifa za juu, akiitaja nafasi aliyoitaka wakati huo, yaani kuajiriwa na Mahakama Kuu.

Kama huo unaweza kuwa mfano wa mbali, hakuna aliyesahau kilichomkuta mchekeshaji maarufu, Bill Cosby.

Mwigizaji huyo anatumikia kifungo cha miaka 10 gerezani kwa makosa yanayofanana na haya ya R. Kelly, unyanyasaji wa kingono.

Kumfika majanga hayo kunaelezwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na mpango aliokuwa nao wa kulinunua shirika la habari la NBC.

Orodha ni ndefu lakini itoshe kumtaja aliyekuwa mfalme wa Pop, Michael Jackson, ambaye kutokana na mafanikio yake, alitengenezewa kesi za aina hiyo, lengo likiwa ni kuumaliza umaarufu na kile alichokichuma kupitia muziki.

Ukirejea kwa R. Kelly, inafikirisha kidogo kuona mpenzi wake wa zamani, Joycelyn Savage, akiibuka na kukanusha madai ya kufanyiwa ukatili wa kingono na msanii huyo.

Kwa mujibu wa Savage, akaunti ya mtandao wake wa kijamii, ambayo ndiyo iliyoibua shutuma hizo dhidi ya R. Kelly, imetekwa na mtu anayeitumia kumchafua staa huyo.

“Imekuwa ikisemekana kwamba aliniacha na alinitesa… Nimeshasema, hiyo si kweli. Ni jambo la aibu kuona wanavyomtesa…”

Naye Azriel Clary, ambaye pia aliwahi kutoka kimapenzi na R. Kelly, anaungana na Savage na kusema wazazi wengi, wakiwamo wao, wamekuwa wakiwatumiwa mabinti zao kufungua kesi dhidi ya staa huyo ili tu kujipatia fedha na umaarufu.

Nikirejea kwa Montana, wakati anamtetea R. Kelly, kabla ya baaadaye kubadilika alipoona anashambuliwa na mashabiki, alisema: “Nafikiri wamnafanya (R. Kelly) kile walichomfanyia Michael Jackson.”

Hali ikoje gerezani?

R. Kelly kwa sasa anasota gerezani mjini Chicago, akisubiri kesi zake zitakazoanza kusikilizwa Aprili, mwakani. Nyota huyo ameshindwa kurejea uraiani baada ya jaribio lake la kupata dhamana kugonga mwamba miezi miwili iliyopita.

Hata hivyo, masharti aliyowekewa yameonekana kuwa si ya haki, kubwa ikiwa ni rafiki mmoja wa kike kati ya wawili aliokuwa nao karibu, ndiye anayeruhusiwa kwenda kumtembelea na atampisha mwingine baada ya siku 90, miezi mitatu.

Awali, R. Kelly alilalamikia kitendo cha kuwekwa chumba cha peke yake, jambo ambalo mwanasheria wake alilipatia ufumbuzi na sasa amechanganywa na watuhumiwa wengine.

Kile kilichoelezwa na mtandao wa udaku wa TMZ miezi miwili iliyopita ni kwamba R. Kelly alikuwa akiomba kutolewa gerezani kwa madai ya afya yake kuteterekea.

Hapo ndipo alipoibuka mwanasheria wake, Steve Greenberg, aliyesema R. Kelly amekuwa hapati huduma bora za kiafya akiwa gerezani na amekuwa akipuuzwa.

Lakini, waendesha mashitaka wamekuwa wakikana, wakisema R. Kelly ana uhuru wa kutosha, ikiwamo kuwa na simu zake tatu,  siku tatu kwa wiki za kufanya mazoezi, pia ‘ofa’ ya kununua vyakula na vinywaji.

Nini hatima yake?

Ikizingatiwa kuwa ana kesi maeneo mawili tofauti, kwa maana ya Chicago na New York, inaelezwa kwamba huenda akaishia gerezani kwa kipindi kisichopungua miaka 55.

Kwamba kwa mashitaka yanayomkabili Chicago, anakabiliwa na kifungo kinachoweza kufikia miaka 30, wakati pia ana rungu la miaka 25 endapo atakutwa na hatia kule New York.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika ujumbe kupitia ukurasa wake wa...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya kinda wa zamani wa timu...

Afua Suleiman afunguka ‘Utalijua Jiji’ ilivyompa ustaa mjini

NA JEREMIA ERNEST JINA alilopewa na wazazi wake ni Afua Suleiman na hata alipojitupa kwenye ulimwengu wa muziki wa...

Keche: Kundi maarufu Ghana linalowatamani Diamond, Kiba, Harmonize

JIACHIE na Staa Wako, wiki hii tumetua mpaka Accra, Ghana kwa kundi maarufu la muziki nchini humo, Keche linofanya vizuri na ngoma...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -