ZAITUNI KIBWANA NA HUSSEIN OMAR
ACHANA na ushindi wa Simba walioupata juzi dhidi ya watani wao wa jadi Yanga, Haruna Niyonzima ndilo jina linalotajwa zaidi kwenye mchezo huo kufuatia kiwango alichokionyesha.
Mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Simba waliibuka na ushindi wa penalti 5-4, Niyonzima aliupiga mpira mwingi sana na kuibua shangwe kubwa kwa Wanamsimbazi hao.
Niyonzima ambaye amesajiliwa na Simba kutokea Yanga, juzi aligawa mipira kwa uhakika, kupiga chenga na kumiliki mipira kwa ufasaha bila kupoteza.
Kiungo huyo mfupi pia aliweza kukaba, kusaidia ulinzi na hata kuanzisha mashambulizi jambo ambalo wengi hawakutarajia.
Kwa kiwango hicho kimetofautishwa sana na kile alichokuwa akicheza Jangwani, ambapo kiungo huyo alipokuwa anakutana na Simba alicheza kwa kiwango duni na kuibua gumzo kubwa nchini.
Niyonzima alipokuwa Jangwani alikuwa akicheza kwa kudeka na mara nyingine alikuwa akipoteza ‘move’ za mabao, kutokana na staili yake ya kurudisha mipira nyuma pale timu inapokuwa inashambulia.
Kutokana na tabia hizo, mashabiki wengi wa Yanga walikuwa wakimtaja Niyonzima kuwa ni mmoja wa wachezaji wanaowahujumu hasa ikifika mechi dhidi ya Simba.
Lakini tofauti na matarajio ya wengi, Niyonzima juzi alikuwa msaada mkubwa kwenye ngome ya Simba na kuwateka mashabiki wa timu hiyo.
Niyonzima ambaye anajulikana kama fundi wa pasi, juzi aliweza kuchezesha timu, pasi zake za mwisho zenye macho pamoja na uwezo wa kukaba.
Hakika huyu si yule Niyonzima wa Jangwani, kwani alionyesha kipaji cha hali ya juu hasa uwezo wake wa kuchezesha wenzake kupitia pasi fupi fupi.