NA MARTIN MAZUGWA
KOCHA mkuu wa timu ya soka Tanzania ‘Taifa Stars’, Charles Mkwasa, ameita kikosi cha wachezaji 24 kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Ethiopia itakayochezwa Oktoba 8 mwaka huu, Addis Ababa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa jana na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, wachezaji hao wataanza mazoezi Oktoba 3 mwaka huu, kujiandaa na mechi hiyo.
Mechi hiyo ipo kwenye kalenda ya wiki ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) kwa wanachama wake kucheza mechi za kirafiki.
Wachezaji walioitwa ni Deogratius Munishi, Said Kipao, Aishi Manula, Shomari Kapombe, Juma Abdul, Vincent Andrew, Mwinyi Haji, Mohamed Hussein, David Mwantika na James Josephat.
Wengine ni Himid Mao, Mohammed Ibrahim, Jonas Mkude, Muzamir Yassin, Shiza Kichuya, Simon Msuva, Juma Mahadhi, Jamal Mnyate, Hassan Kabunda, Ibrahim Ajib, John Bocco, Mbwana Samatta, Elius Maguli na Thomas Ulimwengu.
Katika hatua nyingine, makocha wa timu ya Tanzania ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’, Bakari Shime na Muharami Mohammed, wamesema wako tayari kwa vita kukabiliana na Congo Brazzaville.
Serengeti Boys wanatarajia kucheza mechi ya marudiano ya kuwania kufuzu fainali za Afrika kwa vijana dhidi ya wenyeji Brazzaville utakaochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Alphonse Massamba-Debat.
Shime alisema timu iko vizuri, wamejiandaa na kila kitu kiko sawa, kama tulivyokusudia.
“Lakini pia tupo hapa Congo kuzoea hali ya hewa. Kwa bahati nzuri si tofuati na ya nyumbani Tanzania,” alisema Shime.
Shime alisema anatarajia kutumia mfumo wa 4-4-2 katika mechi hiyo ili kuhakikisha wanapata ushindi baada ya kupata ushindi wa mabao 3-2 kwenye uwanja wa nyumbani wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Fainali ya michuano hiyo itapigwa Aprili mwakani jijini Antananarivo, Madagascar.