Monday, October 26, 2020

Nyota wa kuamua matokeo, Simba Vs Yanga

Must Read

Fati aweka rekodi Barcelona

CATALUNYA, Hispania ANSU Fati ameweka rekodi ya mchezaji kinda wa kwanza kufunga mabao...

Lampard amshika mkono Silva

MANCHESTER, England KOCHA wa Chelsea, Frank Lampard, amesema atamtumia, Thiago Silva, katika mechi nyingi msimu huu licha ya...

Tuchel awatolea uvivu Mbappe, Neymar

PARIS, Ufaransa KOCHA wa PSG, Thomas Tuchel, amechukizwa na kiwango kibovu walichoonyesha mastaa wa timu hiyo, Kylian...

NA ZAINAB IDDY,

KUNA mijadala mikubwa miwili ambayo kwa sasa  imeteka mazungumzo ya Watanzania wengi, mmoja  ukiwa ni tetemeko la ardhi lililotokea Kanda ya Ziwa, hasa Mkoa wa Kagera, mwingine ni mechi ya Watani wa Jadi, Simba na Yanga.

Kwa upande wa tetemeko, hiki ni kisa kibaya zaidi kuwahi kutokea na kusababisha madhara kutokana na kusababishja vifo vya watu wengi na uharibifu wa mali.

Kumekuwa na jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali, taasisi za umma, kiraia  na watu kuhakikisha wahanga wa tukio la tetemeko wanapata msaada unaohitajika.

Ukija kwenye hilo la mechi baina ya Simba na Yanga, wadau wengi wa soka wamekuwa wakizijadili timu hizo ambazo leo zitashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuumana.

Mjadala kuhusu mechi hii umekuwa mkali kutokana na mashabiki wa timu hizo kila upande kujigamba kuwa una kikosi bora ambacho kitaibuka na ushindi.

Mara nyingi watani wa jadi wanapokutana kumekuwa na matukio mengi yanafanyika nje na ndani ya uwanja, kabla na baada ya mchezo kumalizika, huku baadhi ya wachezaji wakiangaliwa kwa jicho la tatu, ikiaminika kuwa ndio wanaweza kuamua matokeo.

Kwa kutambua hilo, BINGWA linakuchambulia wachezaji kutoka kila upande na nafasi ya kila mmoja katika kuamua matokeo ya mchezo huo unaotarajiwa kuwa na upinzani na msisimko wa hali ya juu.

Maana yake ni kwamba, mbali ya mafunzo waliyopata kutoka kwa makocha wao, Hans van der Pluijm wa Yanga na Joseph Omog wa Simba, sifa binafsi walizonazo zinaweza kutoa mchango unaoweza kuufanya upande mmojawapo kushinda mchezo huo.

Shiza Kichuya vs Deus Kaseke

Kwa uzoefu, Kaseke tayari anajua vizuri mikiki mikiki ya mchezo, tofauti na Kichuya ambaye anatarajia kucheza kwa mara ya kwanza.

Kwa upande wa viwango vyao uwanjani na faida kwa kila mmoja, kwanza hawa wote ni mawinga kiasili na wana kasi wawapo na mpira.

Pia wanatofautiana kwa mambo haya: Kaseke anapenda kushambulia kwa kupitia eneo la kati akitumia vizuri nguvu alizonazo kuichachafya ngome yoyote, huku Kichuya akipendela kushambulia kutokea pembeni.

Mashabiki wa soka wanataka kuona nani atang’ara na kumfunika mwenzake kwenye mchezo huo.

Kiujumla watabeba majukumu makubwa ya kuamua matokeo ya mchezo, ikizingatiwa kwamba kila mmoja kwa wakati huu ni mchezaji wa kutumainiwa kwenye kikosi chake.

Ibrahim Ajib vs Donald Ngoma
Kazi za mastraika hao ni kuhakikisha nyavu za wapinzani wao zinatikisika kwa kufunga mabao.

Lakini washambuliaji hawa licha ya kufanana kimaumbile (wote ni warefu), wana uwezo tofauti pia.

Ajibu licha ya kwamba ni mahiri katika kufunga, pia ana uwezo mkubwa wa kuchezesha timu, hasa kwenye eneo zima la ushambuliaji.

Ni mtoaji mzuri wa pasi ambazo huwa ni hatari kwa safu yoyote ya ulinzi.

Kwa upande mwingine, Ngoma ni mshambuliaji hatari katika suala la utupiaji mabao. Mzimbabwe huyo amekuwa ni mwiba mkali kwa mabeki wa timu pinzani, hasa kutokana na uwezo wake wa hali ya juu wa kukokota mpira na nguvu.

Kuelekea mechi hiyo ya watani wa jadi, watazamaji wanawaangalia na kuwategemea sana washambuliaji hawa katika suala la kumaliza mchezo mapema, lakini shida iliyopo ni safu za ulinzi za timu hizi mbili jinsi zilivyo imara kwa sasa.

Laudit Mavugo vs Amis Tambwe

Kama ilivyo kwa Ngoma na Ajib, ili mchezo huo uweze kunoga washambuliaji hawa wanaotoka nchi moja na waliowahi kucheza timu moja ya Vital’O ya Burundi, wanatakiwa kuhakikisha wanacheka na nyavu kama ilivyo kawaida yao.

Tambwe yuko hivi, ni  mshambuliaji anayezijua mno njia za kufunga mabao, hasa ya vichwa.

Tambwe amekuwa akifanya mambo makubwa, licha ya kwamba ana kimo kifupi ambacho kinaweza kukupa wasiwasi kama anaweza kufanya kitu kama hicho.

Aina ya uchezaji wa Mavugo haitofautiani na Tambwe, kwa maana kwamba naye ni mviziaji mzuri.

Mshambuliaji huyu ana desturi ya kuibuka ghafla kwenye njia za krosi, hasa zile zinazopigwa na mabeki wa pembeni na hasa hasa ya beki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Mzamiru Yassin vs Thaban Kamusoko

Eneo la kati la vikosi vya Simba na Yanga linawategemea sana vijana.

Ni viungo wenye majukumu ya kupandisha mashambulizi na kuziba mianya ya wapinzani kupitisha mipira.

Huu ni mchezo wa kwanza wa wapinzani wa jadi kwa Mzamiru tangu ajiunge na Simba akitokea Mtibwa  Sugar.

Kwa maana nyingine, hii itakuwa fursa nzuri kwake kuonyesha kwanini Simba walifika bei.

Kwa Kamusoko, ambaye ni mara yake ya tatu kukipiga mchezo wa mahasimu hao, atakuwa ana kazi kubwa ya kukabiliana na kijana huyo katika harakati za kuisaidia timu yake huku uzoefu wake ukitazamiwa kumbeba.

Jamal Mnyate vs Simon Msuva

Mnyate anacheza nafasi ya kuungo mshambuliaji, ambaye kwenye mechi alizopata nafasi kwenye kikosi cha kocha Omog ameweza kuonyesha uwezo mzuri na kumkosha Mcameroon.

Licha ya kuwa mzuri pia katika kufunga, ni hodari wa  kupandisha mashambulizi  na kutoa pasi zenye macho ambazo mara nyingi zimekuwa mtihani kwa mabeki wa timu pinzani.

Kwa upande wa Msuva, naye anafahamika kwa soka lake la kasi na pia ni moja ya wachezaji wazoefu katika mtanange huo wa watani.

Wawili hao kila mmoja ana nafasi kubwa ya kuamua matokeo katika mchezo huo kama watafanya kazi zao ipasavyo.

Jonas Mkude vs Mbuyu Twite

Msimu uliopita, Mkude alionekana si lolote, lakini msimu huu hali imekuwa kinyume kutokana na kuiongoza Simba vema, ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja mpaka sasa.

Kwenye mechi alizocheza mpaka sasa, kiungo huyo anayesifika kwa uwezo mkubwa wa kupiga mashuti makali ya mbali ameonyesha kiwango cha hali ya juu.

Kwa upande wa Twite, anaonekana kutokuwa kwenye ubora wake wa misimu miwili iliyopita, lakini kitu pekee kitakachombeba kwenye mchezo huo kama atapangwa ni uzoefu alionao katika mechi za watani.

Wawili hao kila mmoja ana nafasi ya kuifanya timu yake kucheka au kulia kama ataamua kupambana kweli kweli.

Method Mwanjali vs Vicent Bossou

Mwanjale ni beki mpya wa kikosi cha wekundu wa Msimbazi aliyesajiliwa msimu huu.

Mlinzi huyo raia wa Zimbabwe ameonyesha kiwango kizuri na kuifanya safu ya ulinzi ya Wekundu hao kuwa bora msimu huu.

Kwa upande wa Bossou, hakuna ubishi kuwa ndiye beki bora wa kati kwa sasa, baada ya kuonyesha uwezo mzuri msimu uliopita na mechi chache za ligi alizocheza msimu huu.

Ubora wake unategemewa sana kuona anayadhibiti mashambulizi yote yatakayofika langoni mwao katika mechi hiyo na iwapo kama ikitokea akatetereka, atakuwa amewakaribisha vijana wasumbufu kama Kichuya na Ajib kufanya kazi yao.

Jjuuko Murshid vs Andrew Vincent ‘Dante’

Murshid ni beki wa kimataifa wa Uganda ambaye kwenye timu yake ya taifa anategemewa na ameiwezesha kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2017).

Katika kikosi cha Simba ni mzoefu katika mechi za watani wa jadi, kwani msimu uliopita alikuwa katika kikosi kilichopigwa mabao 2-0 na Yanga.

Ubora aliouonyesha msimu huu unategemewa, hususan katika kuwadhibiti safu ya ushambuliaji ya Yanga.

Kwa upande wa Vicent, hii itakuwa ni changamoto yake ya kwanza tangu alipojiunga na Yanga akitokea Mtibwa Sugar.

Uchezaji wake umeonekana kumkuna Kocha Hans van der Pluijm na anaonekana kuelekea kuwa mrithi wa nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ama Kelvin Yondani.

Kama atapewa nafasi katika mchezo wa leo, anaweza kufanya mambo makubwa ili mradi tu kama atakuwa mtulivu.

Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ vs Haji Mwinyi

Mchezo huu ndio utakaotoa majibu ni mchezaji gani anapaswa kuwa chaguo namba moja katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars.

Atakayeonyesha ubora mkubwa atajihakikishia tiketi ya kuanza pale Stars itakapoikabili Ethiopia mwezi ujao, katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki.

Ni dhahiri mashabiki wengi wa soka watakaofika uwanjani kushuhudia mpambano wa leo wataelekeza akili zao kwa watu hawa wawili ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakijadiliwa kwamba nani mkali zaidi ya mwingine, wapo wanaodai Tshabalala ni zaidi, huku wengine wakidai Mwinyi ni bora.

Hapo itakuwa ni vita ya beki mkali wa krosi na mwingine akiwa na uwezo wa hali ya juu wa kudhibiti kasi ya winga yeyote machachari.

Juma Abdul vs Hamad Juma

Ni upande utakaokuwa na ushindani sana katika mchezo huo, kutokana na viwango vya mabeki hao ambavyo wamevionyesha kwenye michezo michache ya ligi pale timu zao zilipokuwa dimbani.

Abdul, mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, anatarajia kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Ajib na Mavugo, ambao wamekuwa na tabia ya kushambulia wakitokea pembeni.

Hamad ambaye ni mlinzi mpya wa kulia wa klabu ya Wekundu wa Msimbazi aliyesajiliwa kuongeza nguvu kwenye ukuta wa Simba, ambao hadi sasa haujaruhusu  mabao mengi, atakuwa na kazi moja ya kupambana na wasumbufu wa Yanga, akiwemo Ngoma na Kaseke.

Vicent Angban vs Deogratius Munishi

Ndio makipa namba moja wa timu hizo, Angban anaidakia Simba, huku Munishi akiwa Yanga.

Makipa hao wote wana uzoefu na mechi za watani.

Hatua hiyo inayafanya mabenchi yao ya ufundi kuwaamini katika utendaji wao wa kazi.

Licha ya kwamba katika mechi ya msimu uliopita Simba ilifungwa mabao 2-0, huku langoni akiwapo Angban, lakini tangu kuanza msimu huu ameonekana kuimarika zaidi.

Kama akijiepusha na papara anaweza kuwa kikwazo kwa washambuliaji wa Yanga kupata mabao.

Kwa upande wa Yanga, Munishi tayari ameshaidakia timu yake kwenye mechi ya watani takribani mechi sita,

Katika michezo mitano ambayo Yanga imecheza mpaka sasa, Munishi hajaruhusu nyavu zake kutikiswa.

Mchezo wake wa mwisho kukaa langoni ulikuwa ni dhidi ya African Lyon, uliomalizika kwa Yanga kushinda mabao 3-0.

Bao moja ambalo Yanga imeruhusu ni dhidi ya Stand United ambalo kikosi hicho cha Jangwani kilichapwa 1-0.

Kwa upande wa Angban, yeye amefungwa mabao mawili tu katika michezo sita ya Ligi Kuu msimu huu mpaka sasa.

Itakuwa ni vita kali baina ya walinda milango hawa wawili mahiri.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Fati aweka rekodi Barcelona

CATALUNYA, Hispania ANSU Fati ameweka rekodi ya mchezaji kinda wa kwanza kufunga mabao...

Lampard amshika mkono Silva

MANCHESTER, England KOCHA wa Chelsea, Frank Lampard, amesema atamtumia, Thiago Silva, katika mechi nyingi msimu huu licha ya kuwa na umri wa miaka...

Tuchel awatolea uvivu Mbappe, Neymar

PARIS, Ufaransa KOCHA wa PSG, Thomas Tuchel, amechukizwa na kiwango kibovu walichoonyesha mastaa wa timu hiyo, Kylian Mbappe na Neymar, kwenye mechi...

IBRA:Kifaa kipya Konde Gang aliyetembea kwa mguu kumwinda Harmonize

NA BRIGHITER MASAKI UKITAJA vijana wanaofanya vizuri katika mziki wa bongo fleva, huwezi kukosa kumtaja msanii chipukizi anayefahamika zaidi...

Jay-Z: Mama aliingilia bifu langu na Nas

-Z: Mama aliingilia bifu langu na Nas New York, Marekani HAKUNA shabiki wa Hip hop asiyelifahamu...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -