NA ZAINAB IDDY
KOCHA Mkuu wa Majimaji, Kali Ongala, amekisikia kichapo walichokipata Simba kutoka kwa Azam na kutamka kwamba wajiandae kupokea kipigo kingine.
Simba walipokea kichapo cha bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na BINGWA, Ongala alisema anaendelea kukinoa kikosi ili waweze kuibuka na ushindi dhidi ya Simba, ambao wanatarajia kucheza Februari 5 mwaka huu kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Ongala alisema atatumia upungufu wa Simba waliouonyesha katika mchezo wao dhidi ya Azam ili waweze kubakisha pointi tatu nyumbani.
“Simba ilikuwa na nguvu mzunguko wa kwanza, lakini kwa sasa hakuna kitu, kwani kwenye mchezo wao na Azam wameweza kucheza soka lisilovutia na lisilo na mipango kiasi cha kufungwa kiurahisi hivyo hata wakija Songea wategemee kupoteana uwanjani.
Timu yangu inahitaji ushindi wa hali na mali na kama waamuzi watatafsiri vema sheria 17 za soka, kwetu ushindi ni lazima,” alisema Ongala.
Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa jijini Dar es Salaam.