LONDON, England
KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger, amethibitisha kuwa staa wake, Alexis Sanchez, atakuwamo katika mchezo wao wa Jumapili Ligi Kuu England ambao utawakutanisha na mahasimu wao, Liverpool.
Kauli hiyo ya Wenger imekuja baada ya nyota huyo raia wa Chile kutokuwamo kwenye kikosi hicho cha Gunners tangu msimu huu uanze na huku tetesi za kuhusu hatima ya kuendelea kukitumikia kikizidi kusambaa.
Mbali na kukosekana kikosini, pia hadi sasa Sanchez hajasaini mkataba mpya na klabu hiyo ya Emirates hivyo ina maana kwamba huenda akaondoka akiwa mchezaji huru ifikapo mwishoni mwa msimu huu.
Staa huyo mwenye umri wa miaka 28, kwa sasa anahusishwa kutaka kwenda kujiunga na Manchester City kabla ya dirisha la usajili halijafungwa Agosti 31, mwaka huu na alikuwa haonekani kama ataweza kucheza katika mchezo huo wa mwishoni mwa wiki.
Hata hivyo, jana Wenger aliwatoa mashabiki wake baada ya kusema kuwa ni lazima atakuwamo katika mtanange huo dhidi ya Liverpool.
“Yupo tayari kucheza,” alithibitisha Wenger katika mkutano wake na waandishi wa habari wakati akizungumzia mechi hiyo.
Mbali na kuzungumzia staa huyo pia Wenger alielezea uwezekano wa kupunguza kikosi chake wakati dirisha hilo la usajili likielekea ukingoni.