Thursday, October 29, 2020

SIMBA 4-1 YANGA… Mchezo wote uliishia hapa

Must Read

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya...

NA AYUBU HINJO

DAR es Salaam ilizizima, ilipambwa kwa rangi nyekundu na nyeupe katika mitaa mbalimbali. Furaha isiyo na kifani, isiyoelezeka ilitosha kuwapeleka Simba kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho ambayo watacheza dhidi ya Namungo FC.

Fahari kwa kila mchezaji anayecheza Tanzania ni kucheza Simba na Yanga, lakini ni fahari zaidi iwapo atakuwa sehemu ya mchezo unaozikutanisha timu hizo mbili zenye historia kubwa katika nchi hii.

Kipi kingine unahitaji kutoka Dar es Salaam kama utafunga bao katika mechi ya watani wa jadi? Sidhani kama yupo mchezaji asiyependa sifa kutoka kwa maelfu ya mashabiki waliotimiziwa raha zao kwa dakika 90 tu.

Jiulize ilikuwaje kwa mashabiki wa Simba walioudhuria mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Yanga katika Uwanja wa Taifa?

Jioni moja yenye kumbukumbu isizoweza kufutika katika vichwa vya Wanamsimbazi, ilikuwa jioni ya kipekee ambayo kila mmoja alishuhudia Yanga wakipokea kipigo kizito mithili ya paka mwizi.

Jioni iliyokaribisha usiku kwa utulivu. Kila shabiki wa Simba alitembea kifua mbele, hakuna aliyejali, furaha iliwafanya kufanya starehe hata zile walizosikia. Maisha yanahitaji nini tena?

Hapa namzungumzia mchezo wa juzi. Simba waliitawanya Yanga kwa mabao 4-1. Gerson Fraga, Clatous Chama, Luis Miquissone na Mzamiru Yassin walipeleka furaha mitaa ya Msimbazi, huku Feisal Salum ‘Fei Toto’ akiwafuta Wanajangwani machozi kwa bao pekee.

Iko hivi, Simba inayofundishwa na Sven Vandenbroeck iliingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa bao 1-0 na Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa Machi 8, mwaka huu, Uwanja wa Taifa.

Pia, mechi ya kwanza kuzikutanisha timu hizo msimu huu ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2 huku Yanga wakisawazisha mabao hayo kupitia kwa Balama Mapinduzi na lile la kujifunga kwa beki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba, hiyo ilikuwa baada ya Meddie Kagere na Deo Kanda kuwatanguliza mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mechi ya juzi haikuhitaji pointi, mshindi wa mchezo huu ametinga fainali ya ASFC ambayo inatoa mwakilishi wa nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Afrika.

Kipi kilitokea katika mchezo huo wa watani wa jadi uliochezwa mida ya 11 jioni kwa saa za Afrika Mashariki?

SIMBA WALIFANIKIWA WAPI?

Pengine, mashabiki wa Simba walikuwa na wasiwasi mkubwa zaidi, baada ya kushindwa kupata ushindi katika michezo miwili iliyopita dhidi ya Yanga.

Mechi zilizopita zilionyesha Simba hawakuwa tayari kucheza dhidi ya wapinzani wao. Lakini, juzi waliingia tofauti, makosa yaliyotokea michezo ya nyuma hayakupewa nafasi tena.

Kila mpira waliogombea na Yanga walishinda. Hiyo ilikuwa dalili nzuri kwao. Kubwa zaidi, jinsi walivyoweza kutambua majukumu yao kila mpira ulipokuwa kwao au kwa wapinzani.

Sven aliingia na mfumo wa 4-2-3-1. Mfumo ambao uliwauliza maswali mengi Yanga na wakali hao wa Jangwani kushindwa kutoa majibu sahihi.

Moja, Fraga na Mkude waliipa Simba uwiano mzuri kwa wakati wote, mmoja alikaba na mwingine aliisukuma timu kwenda mbele. Walitimiza majukumu yao.

Uwepo wa wawili hao uliwapa ahueni mabeki wa kati wa Simba, Kennedy Juma na Pascal Wawa ambao hawakufikiwa kiurahisi na wapinzani wao. Mipira mingi iliyoelekezwa katika lango lao haikuwa na madhara.

Mabeki wa Simba hawakupata presha kubwa kutoka kwa wapinzani wao, si katikati wala pembeni kwa akina Tshabalala na Shomari Kapombe.

WATATU WAIZAMISHA YANGA

Simba wanajivunia uwepo wa viungo wengi wenye uwezo mkubwa wa katika kikosi chao. Lakini, michezo ya karibuni Sven amekuwa akiwatumia Chama, Miquissone na Francis Kahata.

Watatu hao hawakutofauni na mzimu wa kutisha kwa wapinzani wao. Kila walichokifanya kiligeuka kuwa dhahabu na kuwaweka Yanga katika wakati mgumu kwa wakati wote.

Chama ni mchezaji wa kipekee katika kikosi cha Simba. Pengine, ni mmoja ya wachezaji bora wanaocheza eneo la kiungo cha ushambuliaji hapa nchini.

Mijongeo yake ‘movement’, maono ‘vision’ na maamuzi ‘decision’, anazielewa mno ‘frequence’ za mpira, anajua ni wakati gani anatakiwa kutoa pasi na ni wakati gani anatakiwa kukokota mpira. Ukiupenda mpira, utampenda tu Chama.

Kila kiungo aliyecheza dhidi ya Chama wote alitulizwa na sehemu ya ubongo wa kiungo huyo wa Zambia, ambao kitaalamu unaitwa ‘Cerebrum’.

Wote walifia hapo na kujikuta wakiwa watumwa wakufanya kila alichokuwa akifanya Chama, sikushangaa pia walipokuwa wakikimbia kufata nyayo zake, ni ngumu sana kucheza na Chama aliye katika kilele cha ubora wake.

Nyota huyo raia wa Zambia ni moyo au ubongo wa Simba katika eneo la ushambuliaji, uamuzi, hesabu na jinsi anavyoweza kufunga au kutengeneza nafasi za mabao anaonyesha ni mchezaji wa kipekee.

Tangu mwanzo wa mchezo huo Chama alionyesha utofauti. Mikimbio na pasi zake zilitosha kuwaadhibu Yanga ambao hawakujua kipi cha kufanya kumdhibiti kiungo huyo.

Ni ngumu kuiona Simba ikipoteza mchezo kama Chama yupo juu ya kilele cha kiwango chake. Ni ngumu mno. Alifunga bao la pili, pia, alihusika katika mabao mengine matatu waliyofunga dhidi ya Yanga.

Mwingine ni Miquissone, maarufu kwa jina la Konde Boy. Hakika Dar es Salaam imepata mtu wake. Mchezaji mwingine wa kipekee anayeipeperusha bendera ya Simba.

Kwa muda mfupi aliokuwa na Simba alianza katika michezo miwili dhidi ya Yanga. Ule waliofungwa bao 1-0 na huu walioshinda mabao 4-1.

Ni wachezaji wachache wenye uwezo wa kuitafsiri nafasi wanapokuwa uwanjani, basi Luis ni mmoja wao. Jinsi anavyo kakokota anatengeneza nafasi na vile anavyoingia kwenye eneo la wapinzani anaitafsiri nafasi.

Ni bahati kuwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara labda anapita zake kama wengine waliofanikiwa kufanya hivyo miaka ya nyuma.

Juzi, alikuwa mwiba kwa Yanga. Ni mchezaji pekee katika mchezo huo aliyechezewa rafu mara nyingi zaidi, pia, alimafanya mwamuzi Ramadhan Kayoko kuwaadhibu wapinzani wao kwa kuwaonyesha kadi za njano nne kupitia yeye.

Ni ngumu kutabirui anatumia mguu gani, yote inafanya kazi kwa ufasaha, ingawa, wa kushoto unaonekana kuwa na matumizi makubwa zaidi.

Pia, ndani ya kikosi hicho yupo Kahata. Labda, ni ngumu kuona kazi yake anapokuwa uwanjani. Amebarikiwa uwezo mkubwa wa kuchezea mpira na jicho lenye lensi kubwa ya kuona mbali.

Aina ya uchezaji wake wa kuingia ndani ulikuwa tatizo kwa mabeki wa pembeni Yanga, Juma Abdul na Jaffari Mohamed. Walirazimika kumfuata kila alipoingia ndani ya kuacha nafasi ambayo ilitumiwa na Kapombe au Tshabalala kushambulia.

YANGA WALIKWAMA WAPI?

Hawakutimiza hata nusu ya kile walichokifanya katika michezo miwili iliyopita dhidi ya Simba. Kila kitu kilikuwa tofauti kwao, safu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji hazikuwa vizuri.

Kila aina ya mpira waliogombea na Simba walishindwa. Mipira ya 50/50, mipira ya pili ‘second ball’, mipira ya juu na kubwa zaidi wachezaji walishindwa kutimiza majukumu yao ya msingi.

Mfumo wa 4-2-3-1 uliotumiwa na Luc Eymael ulishindwa kutamba dhidi ya ule wa Simba. Kocha huyo raia wa Ubelgiji alishindwa kuiunganisha timu yake katika eneo la kiungo ambalo wapinzani wao walitawala kwa kiasi kikubwa.

Pengine, kuanza kwa nahodha Pappy Tshishimbi, Haruna Niyonzima na Bernard Morrison kuliiweka Yanga rehani dhidi ya Simba ambao wachezaji wao walikuwa vizuri kimwili na akili.

Niyonzima alipata majeraha dhidi ya Biashara United wiki iliyopita, pia, hakucheza dhidi ya Kagera Sugar. Ilikuwa ngumu kwake kurejea na kutamba katika mchezo huo uliobeba matumaini makubwa ya mashabiki wa Yanga.

Upande mwingine, ule ulikuwa mchezo wa kwanza kwa nahodha Tshishimbi ambaye alikuwa nje kwa majeraha ya muda mrefu. Hakuonyesha kiwango kile kilichotarajiwa na wengi.

Naye, Morrison alikosa utimamu wa mwili, licha ya kucheza dhidi ya Kagera Sugar na kufunga bao pekee lililopeleka shangwe mitaa ya Jangwani, bado hakuonyesha kiwango kikubwa.

Labda, kocha alikuwa akimtengeneza kimwili na kiakili. Ndiye mchezaji pekee wa Yanga mwenye uwezo wa kuisambaratisha safu ya wapinzani kama akiwa kwenye kiwango bora.

Lakini, ilikuwa tofauti. Morrison hakuwa na siku nzuri kama ilivyokuwa katika mechi iliyopita ya Machi 8, mwaka huu. Mbaya zaidi alionyesha utovu wa nidhamu kwa kuondoka uwanjani baada ya kufanyiwa mabadiliko.

Ili kuifunga Simba, kwanza unatakiwa ujue jinsi gani ya kupambana nao katika aina yote mipira, yaani wakiwa nao au ukiwa miguuni mwenu.

Yanga hawakuwanyima uhuru viungo wa Simba kila walipokuwa na mpira. Hawakukera kila walipokuwa na mpira, kwa Simba ilikuwa faida.

Presha iliyotengenezwa katikati ya uwanja haikutakiwa kuwatoa kwenye mawazo yao kimbinu. Sababu, Simba imekusanya kikosi chenye wachezaji bora wenye uwezo wa kuamua lolote, popote.

Ilikuwa ngumu kujua kipi wanakifanya Yanga uwanjani. Kila walichokifanya kilienda tofauti na walivyotaka. Labda, hawakujiandaa kucheza dhidi ya Simba.

Au, michezo miwili ya mwisho dhidi ya vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara iliwapa ari kubwa ya kujiamini na mwishowe waliingia wakiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri zaidi.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika ujumbe kupitia ukurasa wake wa...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya kinda wa zamani wa timu...

Afua Suleiman afunguka ‘Utalijua Jiji’ ilivyompa ustaa mjini

NA JEREMIA ERNEST JINA alilopewa na wazazi wake ni Afua Suleiman na hata alipojitupa kwenye ulimwengu wa muziki wa...

Keche: Kundi maarufu Ghana linalowatamani Diamond, Kiba, Harmonize

JIACHIE na Staa Wako, wiki hii tumetua mpaka Accra, Ghana kwa kundi maarufu la muziki nchini humo, Keche linofanya vizuri na ngoma...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -