NA HUSSEIN OMAR
WAKATI wachezaji wengi duniani wakiwa na shauku ya kuitwa kuzichezea timu zao za taifa, hali hiyo imekuwa ni tofauti kwa mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe ambaye ameomba kuachwa katika kikosi cha nchi yake ya Burundi kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji iliyopangwa kufanyika mwezi ujao nchini Kenya.
Tambwe ameamua kuchukua uamuzi huo aweze kupata muda zaidi wa kupumzika pindi Ligi Kuu Tanzania Bara itakaposimama baada ya kumalizika mzunguko wa kwanza na hivyo kukusanya nguvu kuisaidia timu yake katika mzunguko wa pili kuhakikisha inatetea ubingwa wake na hivyo kuwakata maini Simba waliopo kileleni kwa sasa.
Kauli hiyo ya Tambwe imeonekana kama ‘mwiba mchungu’ kwa watani wao hao wa jadi, Simba, ambao msimu huu wamedhamiria kufanya kweli na hatimaye kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, kwa sasa wakiwa kileleni na pointi zao 20 baada ya kucheza mechi nane.
Akizungumza na BINGWA jana, Tambwe alisema uchovu wa kucheza mechi nyingi bila kupumzika zimeufanya mwili wake kuchoka hivyo kushindwa kucheza katika kiwango chake hali ambayo inamlazimu kupata muda wa kupumzika ili aweze kuyatimiza majukumu yake katika klabu hiyo kikamilifu.
“Yaani natamani kupata wiki mbili hadi tatu kupumzisha huu mwili umechoka sana kwa kweli, ndio maana kuna kipindi mwili unakataa kabisa uwanjani.
“Kwa kweli sitaweza kucheza chalenji kwa hali hii ambayo naiona inabidi niombe kupumzika kuchezea timu ya taifa katika michuano ya chalenji mwaka huu,” alisema Tambwe.
Alisema amepanga kutumia mapumziko ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, yatakayomalizika Novemba 6, mwaka huu kupumzisha mwili wake.
“Mzunguko wa kwanza ukiisha tu sitaki kuusikia mpira wala kuugusa nitahakikisha napata mda mzuri wa kupumzisha mwili na kufanya mambo ya kijamii,” aliongeza Tambwe.
Tambwe kwa sasa ndiye kinara wa mabao katika kikosi cha Yanga akiwa na mabao manne, lakini akiwa ndiye anayetetea kiatu cha ufungaji bora alichotwaa msimu uliopita baada ya kutikisa nyavu za timu pinzani mara 21 na kuisaidia timu yake kuchukua ubingwa.