SALMA MPELI NA WINFRIDA MTOI
BAADA ya kubanwa na kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya Azam FC, kikosi cha Wekundu wa Msimbazi, Simba, jana kilianza kuifanyia kazi Mwadui FC katika mazoezi waliyofanya kwenye Uwanja wa Uhuru, kujiandaa na mchezo huo utakaopigwa Jumapili hii kwenye uwanja huo.
Kikosi hicho kilifanya mazoezi yake kwa takribani saa moja na nusu kuanzia saa 3:30 hadi saa 5:00 asubuhi, ambapo kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog na msaidizi wake Jackson Mayanja, walionekana kuwapa wachezaji mazoezi mepesi kabla ya kugawa vikosi viwili tofauti.
Katika vikosi hivyo, kila kocha alisimama na chake ambapo waliwapa wachezaji mazoezi ya utimamu wa mwili, kupiga pasi ndefu pamoja na mipira ya vichwa, huku wakikazania zaidi jinsi ya kutulia na mpira ndani ya 18.
Kwenye mazoezi hayo, Mayanja alisimama na wachezaji saba walikuwepo kwenye kikosi cha kwanza kilichocheza na Azam FC wakiwamo washambuliaji, Jonh Bocco, Nikolaus Gyan ambapo alikuwa anawakazania jinsi ya kutulia ndani ya 18 wanapopata mpira.
Baada ya kumalizika mazoezi hayo, Omog alisema walilazimika kugawa vikosi viwili; kimoja kwa wale wanaokuwa wanaanza kikosi cha kwanza na kingine kikiwa na wachezaji wa wanaosubiri wakichanganyika na baadhi wa kikosi cha kwanza.
Alisema wanaendelea na mazoezi kujiandaa dhidi ya Mwadui, kwani wanatambua utakuwa ni mchezo mgumu kutokana na wapinzani wao kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar, kwa kufungwa bao 1-0 na wao wametoka sare hivyo kila mmoja atahitaji kushinda.
“Tunaendelea na mazoezi kujiandaa dhidi ya Mwadui, tunawafahamu vizuri wapinzani wetu niliwaona msimu uliopita tulivyocheza nao walikuwa wazuri, sijui walivyojipanga kwa sasa ila najua utakuwa mchezo wa ushindani zaidi kila mmoja akihitaji kuondoka na pointi tatu,” alisema Omog.