NA HUSSENI OMAR
SIMBA ni kama imeivua Yanga taulo ukweni, kutokana na kitendo cha wanachama wa timu hiyo Tawi la Tandale kwa Mtogole kuushinikiza uongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi kumsajili winga Simon Msuva katika kipindi cha dirisha dogo la usajili.
Akizungumza na BINGWA, Katibu Mkuu wa Tawi hilo, Ally Hamis, maarufu ‘Shababy Ponda’, alisema katika kipindi hiki ambacho Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) imesimama, wamepanga kupeleka mapendekezo yao kwa uongozi wa timu hiyo kuutaka ufanye kila linalowezekana kuhakikisha Msuva anasajiliwa na Wekundu hao wa Msimbazi.
Alisema wanachama wa Simba wamezitazama vyema timu zote 16 zinazoshiriki VPL msimu huu na kugundua kuwa ni mchezaji mmoja tu ndiye anaweza kucheza Simba na huyo si mwingine, bali ni Msuva.
“Kwa kweli sikufichi, karibia wanachama wote wa Simba Tanzania nzima kilio chao kwa viongozi wa juu wa kamati ya utendaji ni Msuva, tuna hamu sana huyu jamaa siku moja aje kuvaa uzi wa Simba kwa sababu ana uwezo wa kuichezea timu yetu,
“Sisi tunasema kama tatizo ni fedha basi tumtumie Kessy (Hassan Ramadhan) kumnasa Msuva, sisi tuwaachie Kessy kwa kuwa bado kuna kesi ya msingi kati ya Simba na Yanga kuhusiana na usajili wake na kisha wao watupe Msuva,” alisema Shababy.
Wanachama hao wa Simba wanaamini timu yao inaweza kutumia sakata la usajili wa Kessy. ambaye Kamati ya Sheria, Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ilimuidhinisha kuchezea Yanga katika VPL ili kumnasa Msuva.
Simba waliwasilisha malalamiko TFF wakidai Kessy kuwalipa Dola 60,000, sawa na Sh milioni 126, kutokana na kuvunja mkataba uliokuwa umalizike Juni 15, mwaka huu.
Baada ya kusikia kilio hicho cha wanachama wa Simba, Tawi la kwa Mtogole, BINGWA lilimtafuta Katibu Mkuu wa timu hiyo, Patrick Kahemele kulizungumzia suala hilo na kusema hawezi kusema chochote kuhusu maoni hayo kwa kuwa ni hoja ya wanachama haina uhusiano na uongozi.
“Hiyo ni hoja tu, umekwenda kuzungumza na wanachama wamesema hivyo, kwa upande wangu siwezi kuzungumzia suala kama hilo, kuhusisha na uongozi,” alisema Kahemele.
Alisema kila mwanachama katika timu hiyo ana haki ya kusema lolote, lakini wao kama viongozi kazi yao ni kufanya shughuli zote zinazohusiana na masuala ya kiutendaji.