Tuesday, October 20, 2020

SIMBA, YANGA KUSIMAMISHA NCHI DAKIKA 90 LEO

Must Read

Director Kenny: Harmonize alinipeleka WCB nikafanya video ya Lavalava

MWONGOZAJI bora wa video nchini, Kenned Sanga a.k.a Derector Kenny kutoka Zoom Extra, ametua   hapa Jiachie na...

Rogers mwanamuziki anayevutiwa na Marijani

NA JEREMIA ERNEST BONGO Star Search (BSS), ni shindano lililofanikiwa kuibua vipaji vingi vya...

Ihefu, Azam patachimbika Sokoine, Katwila ndani

NA ASHA KIGUNDULATIMU ya Ihefu inatarajia kushuka uwanjani kucheza na Azam ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu...

NA WAANDISHI WETU, ZANZIBAR


USIKU wa leo nchi itasimama kwa dakika 90 kupisha pambano la nusu fainali la michuano ya Kombe la Mapinduzi kati ya Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, huku mashabiki wa soka nchini na kwingineko wakiwa na shauku ya kufahamu nani atakayemtambia mwenzake.

Iwapo hakutapatikana mshindi ndani ya dakika 90, mshindi atapatikana kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.

Wakongwe hao wa soka nchini, wanakutana Zanzibar ikiwa ni mara ya nne ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1975 na Yanga ilishinda mabao 2-0, ukiwa ni mchezo wa fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame). Wafungaji walikuwa ni marehemu Gibson Sembuli na Sunday Manara ‘Computer’.

Mwaka 1992, timu hizo zilivaana mara mbili, ya kwanza ikiwa ni Kagame Cup ambapo zilitoka sare ya bao 1-1, Hussein Masha, akiifungia Simba, wakati lile la Yanga likiwekwa kimiani na Said Mwamba ‘Kizota’ kabla ya Wekundu wa Msimbazi kushinda kwa mikwaju ya penalti 6-5.

Mara ya tatu ilikuwa ni mwaka huo huo, lakini ikiwa ni katika mchezo wa Kombe la Muungano ambapo Simba walishinda bao 1-0, shukrani kwa bao la Damian Kimti.

Kwa mara nyingine, watani wa jadi hao walikutana mwaka 2011 katika fainali ya Kombe la Mapinduzi ambapo Simba walishinda mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa usiku, huku wauaji wakiwa ni Mussa Hassan ‘Mgosi’ na Shija Mkina.

Kuelekea mchezo wa leo, Simba waliokuwa Kundi A, wamefika hatua hiyo ya nusu fainali baada ya kuongoza wakiwa na pointi 10, huku Yanga wakimaliza nafasi ya pili Kundi B kutokana na pointi zao sita.

Jambo la kufurahisha katika mchezo wa leo ni kwamba, inakutana safu bora ya ulinzi ya Simba ambayo katika michezo yake hiyo minne waliyocheza, wameruhusu kufungwa bao moja tu dhidi ya safu kali ya ushambuliaji ya Yanga ambayo katika michuano hiyo imeshafunga jumla ya mabao nane.

Safu hiyo ya ushambuliaji ya Yanga ilianza kushtua wapinzani wao baada ya kuwaangamiza bila huruma Jamhuri ya Pemba mabao 6-0 na baadaye kuibuka na ushindi mwingine wa mabao 2-0 dhidi ya Jang’ombe Boys kabla ya kushangazwa na Azam FC walipofungwa mabao 4-0.

Kutokana na mabao hayo, Yanga ndiyo timu pekee inayoonekana kuwa na safu kali ya ushambuliaji lakini kilichowaangusha ni safu yao ya ulinzi kukubali kuruhusu mabao hayo 4-0 kutoka kwa Azam FC ambapo kama wangejikaza na kuambulia angalau suluhu wangekuwa na safu kali ya ushambuliaji na pia ukuta wao ungeitwa wa Berlin.

Kwa upande wao Simba walianza kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Taifa Jang’ombe na kuibuka na ushindi mwingine wa bao 1-0 dhidi ya KVZ na kutoka suluhu dhidi ya URA kabla ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Jang’ombe Boys na kufanikiwa kutinga hatua hiyo ya nusu fainali wakiongoza kundi lao.

Matokeo hayo yanamaanisha kuwa Simba wana ukuta imara chini ya Abdi Banda na Method Mwanjali, kwani wameruhusu bao moja peke yake na uimara wao utazidi kudhihirika kama watazuia moto wa akina Donald Ngoma, Amissi Tambwe pamoja na Simon Msuva usiku wa leo.

Katika michezo hiyo ambayo Simba na Yanga wamecheza michuano hiyo ya Mapinduzi kuna baadhi ya mapungufu ambayo kila moja itatakiwa kuyarekebisha vinginevyo yanaweza kuigharimu moja kati ya timu hizo na kupeleka kilio kwa mashabiki wao.

Kwa upande wa Yanga walionekana kuanza vizuri michuano hiyo, lakini kadiri muda ulivyokuwa ukienda walionekana kuchoka kwani walianza kwa kushinda mabao 6-0 yakapungua mchezo wa pili na kuwa 2-0 na kumaliza hatua hiyo ya makundi kwa kufungwa mabao 4-0 dhidi ya Azam FC jambo lililowashtua mashabiki wao.

Nini wanatakiwa kukifanya Yanga

Baada ya kuondoka kwa Vincent Bossou kwenda kujiunga na timu yake ya Taifa ya Togo, safu ya ulinzi imekuwa chini ya Kelvin Yondani na Vincent Andrew ‘Dante’ ambao katika mchezo dhidi ya Azam FC walionekana kupwaya kidogo na kuruhusu mabao hayo 4-0.

Anachotakiwa kukifanya kocha wao, George Lwandamina ni kuwaambia mabeki wake hao wasije wakafanya makosa mengine kwani kosa lolote watakalolifanya linaweza kumtengenezea jina kubwa, Laudit Mavugo, ambaye anaonekana kuanza kurudi kwenye ukali wake aliokuwa nao Vital’O ya Burundi.

Zullu asianzishwe kwanza

Yanga wana mtu anayeitwa Justice Zullu ‘Mkata Umeme’, kiungo ambaye alisajiliwa kutoka Zesco United ya Zambia, lakini bado ile kasi iliyotarajiwa haijaonekana ndiyo maana katika mchezo dhidi ya Azam FC na Wanajangwani hao walijikuta wakizidiwa eneo la kiungo mpaka pale alipoingia Juma Makapu ndiyo ikawa afadhali kidogo.

Wanajangwani hao wanatakiwa kuwa makini sana katika eneo hilo la kiungo ambapo Thaban Kamusoko na Haruna Niyonzima wakishirikiana na Makapu, wanatakiwa kufanya kazi ya ziada vinginevyo wakiwaacha Mkude na Mzamiru Yassin kujinafasi usiku huo utakuwa mrefu kwa mashabiki wao.

Ngoma, Tambwe na Msuva

Katika safu ya ushambuliaji ya Yanga, hakuna shaka kwani shughuli yao ni nzito kuanzia Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka kwenye michuano hiyo ya Mapinduzi kwani japo hawakuweza kufurukuta mbele ya Azam, lakini hilo halifuti ukweli kwamba wana uchu wa mabao.

Katika mchezo huo dhidi ya Azam, Ngoma hakuwepo ila leo anatarajiwa kuungana na wenzake na kama Abdi Banda na Method Mwanjali, watafanya kosa lolote, wanaweza wakajuta kuwafahamu washambuliaji hao.

Kwa upande wao, Simba safu yao ya ulinzi ni moja ya ngome imara kwani hilo linadhihirika mpaka Ligi Kuu na jambo ambalo linaweza kuwagharimu ni kutokuwa na kasi kwa Banda kwani hata katika mchezo wa Februari 20, 2016 pale Simba walipofungwa mabao 2-0 na Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu, Banda alishindwa kuhimili kasi ya Ngoma na kujikuta akimfanyia madhambi na kutolewa kwa kadi nyekundu.

Mzima Swichi naye asianze

Wakati Yanga kukiwa na ‘Mkata Umeme’, kwa upande wa Simba yupo James Kotei ‘Mzima Swichi’ ambaye pamoja na kuwa na uwezo mkubwa, lakini baadhi ya mashabiki wanataka asianzishwe na badala yake, Mkude na Muzamiru, wakabidhiwe rungu hilo.

Mara nyingi eneo hilo la katikati ndilo linaloweza kuamua matokeo hivyo baadhi ya mashabiki hao wanadhani kuwa ushirikiano wa Mkude na Mzamiru au Mwinyi Kazimoto, unaweza kuzima mbwembwe za Niyonzima na Kamusoko wasilete madhara eneo hilo la kiungo.

Mavugo na Luizio

Awali Mavugo alionekana si lolote lakini mambo makubwa aliyoyafanya huko Zanzibar hasa katika mchezo dhidi ya Jang’ombe Boys alipofunga mabao mawili katika ushindi wa 2-0 inaonyesha wazi akina Yondani na mwenzake Dante wanayo kazi kubwa ya kuzuia moto wao.

Uzuri wa Luizio ni kwamba, anaweza kutumia vizuri mwili alionao na katika michezo aliyocheza alionekana dhahiri kuwa msumbufu na mtu asiyeogopa mabeki hivyo kama wawili hao watapewa nafasi na kocha wao, Joseph Omog na wakajituma kama ilivyokuwa michezo iliyopita wanaweza wakawapa furaha mashabiki wao.

Katika nusu fainali nyingine, Azam FC watapambana na Taifa Jang’ombe mchezo wa mapema leo saa 10:00 na mshindi kwenye mchezo huo ndiye atakayecheza fainali na mshindi kati ya Simba na Yanga nusu fainali ya pili usiku wa saa 2:15.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Director Kenny: Harmonize alinipeleka WCB nikafanya video ya Lavalava

MWONGOZAJI bora wa video nchini, Kenned Sanga a.k.a Derector Kenny kutoka Zoom Extra, ametua   hapa Jiachie na...

Rogers mwanamuziki anayevutiwa na Marijani

NA JEREMIA ERNEST BONGO Star Search (BSS), ni shindano lililofanikiwa kuibua vipaji vingi vya wanamuziki wa Tanzania ambao miongoni...

Ihefu, Azam patachimbika Sokoine, Katwila ndani

NA ASHA KIGUNDULATIMU ya Ihefu inatarajia kushuka uwanjani kucheza na Azam ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara  (VPL), utakaochezwa leo...

Mugalu atema cheche Simba

NA ASHA KIGUNDULA MSHAMBULIAJI wa Simba, Chris Mugalu, amesema wanakwenda mkoani Rukwa kupambana na kupata ushindi katika mchezo wao...

Malale aitisha Yanga

NA ZAINAB IDDY KOCHA Mkuu wa timu ya Polisi Tanzania, Malale Hamsini, amezisikia sifa za kocha mpya wa Yanga,...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -