NA ELIYA MBONEA, ARUSHA
MAKOCHA wa riadha kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWZ), mkoani Arusha, Athony Muingereza na Andrew Panga, wametajwa kuhusika kwa karibu zaidi na ushindi wa mwanariadha Alphonce Simbu (25).
Simbu alishika nafasi ya kwanza kwenye mbio za Mumbai Marathon kwa kufanikiwa kushika nafasi ya kwanza akitumia saa 2:09:28, huku akiwaacha mbali wanariadha saba kutoka nchini Kenya akiwamo Joshua Kipkorir aliyetumia saa 2:09:50.
Akizungumzia mchango mkubwa uliotolewa na makocha hao, Simbu alisema ana kila sababu ya kuwashukuru, kwani walitumia muda, fedha na mali zao kuhakikisha anatimiza malengo yake ikiwamo ushindi aliopata Mumbai Marathon.
Maandalizi ya kushiriki mbio hizo aliyafanyia mkoani Arusha akiwa na wanariadha wenzake, ambapo walifanya mazoezi maeneo tofauti huku Muingereza akishiriki mwanzo mwisho.
“Namshukuru sana mwalimu Muingereza, Mungu ambariki kwani anatusaidia wanariadha kwa kutumia mali, fedha na muda wake, ni mwalimu anayependa riadha. Kwani amekuwa akitumia usafiri wake kukimbia na sisi mbio ndefu kwenye mazoezi.
Mwalimu Panga pia amekuwa msaada mkubwa kwetu. Hawa wote wamekuwa wakiweka mafuta kwenye vyombo vyao vya usafiri na wanahakikisha tunakimbia umbali wa kilomita 32 mpaka 40 bila kuwalipa.
Simbu anayeishi kwenye nyumba yake kwa sasa alikishauri Chama cha Riadha nchini (RT), kuwangalia kwa jicho la karibu walimu hao ili kuongeza ufanisi kwenye riadha nchini.
“Kuna walimu wachache wanaoweza kujitoa kama hawa. Si rahisi mtu aache shughuli za kumwingizia kipato atumie gari, fedha na muda wake kwa ajili ya kuona unafanikiwa ni wachache kwenye michezo,” alisema Simbu.
Simbu aliwashukuru pia wanariadha wenzake aliokuwa akifanya nao mazoezi kabla ya kwenda Mumbai India kushiriki mashindano hayo.