NA MAREGES NYAMAKA
LICHA ya Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, mashabiki wa timu hiyo juzi Jumapili walionekana kuchukizwa na kitendo cha kocha Joseph Omog kumtoa kiungo Mohamed Ibrahim.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, bao la pekee lilifungwa na Ibrahim baada ya kupokea krosi ya beki Javier Bokungu.
Licha ya kufunga bao hilo huku akionyesha kiwango maridadi, kocha Omog aliamua kufanya mabadiliko ambapo alimtoa Ibrahim na kumwingiza mshambuliaji Juma Liuzio.
Kitendo cha kocha huyo kumtoa Ibrahim kilionekana kuwakera mashabiki wa timu hiyo ambao walisikika wakimpinga kwa hatua hiyo.
“Kocha umebugi sana, haiwezekani Mo amecheza vizuri si tu kwa sababu amefunga, lakini unaona ana kiu ya kufanya kitu na bado alikuwa mwiba kwa mabeki wa timu pinzani halafu unamtoaje nje mchezaji kama huyo,” alisikika mmoja wa mashabiki.
Mchezaji alionyesha ishara ya kutopendezwa na uamuzi wa kocha wake huyo kwani baada ya kutoka uwanjani aliketi moja kwa moja katika benchi badala ya kuwapa mikono wachezaji wenzake kama ilivyozoeleka.