NA SALMA MPELI,
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Amissi Tambwe, ameshonwa nyuzi sita baada ya kupasuka katika paji la uso katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Tambwe aliumia baada ya kugongana na kiungo wa Mtibwa Sugar, Shaaban Nditi, wakiwa wanawania mpira wa juu na kushindwa kuendelea na mchezo.
Akizungumza na BINGWA jana, Daktari wa Yanga, Edward Samwel, alisema kutokana na jeraha hilo, Tambwe alilazimika kushonwa nyuzi sita na sasa anaendelea na matibabu.
Samwel alisema kutokana na jeraha hilo, atakaa nje wa uwanja kwa kipindi cha wiki nne na kukosa mechi nne za Ligi Kuu Bara, ikiwemo ya Azam itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mechi nyingine atakayokosa ni Toto Africans itakayochezwa Oktoba 19 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza, Kagera Sugar utakaochezwa Oktoba 22 kwenye Uwanja wa Kaitaba na Mbao watacheza Oktoba 29, Uwanja wa Uhuru.
Samwel alisema ni mara ya pili kwa mchezaji huyo kuumia sehemu hiyo, kwani aliwahi kuumia wakati timu hiyo ilipoweka kambi Uturuki kujiandaa na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kushonwa nyuzi tatu.
“Atakuwa nje kwa muda kidogo kwa ajili ya jeraha hilo, lakini baada ya hapo ataanza mazoezi mepesi,” alisema Samwel.
Tambwe mpaka sasa amefunga mabao manne huku winga wa Simba, Shiza Kichuya, akiongoza aliyefikisha mabao sita.