Saturday, October 31, 2020

Tatizo la Diamond ni Tandale, fedha au tuzo?

Must Read

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya...

NA MICHAEL MAURUS,

JUMANNE ya wiki iliyopita katika ukurasa huu, nilianza na mfululizo wa makala haya yanayohusiana na maisha ya msanii wa muziki wa kizazi kipya, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Katika makala hayo, nilielezea jinsi Diamond anavyochukiwa na baadhi ya wapenzi wa muziki hapa nchini pamoja na ukweli kwamba ndiye msanii mwenye mafanikio zaidi kwa kutwaa tuzo nyingi nje ya nchi.

Japo Diamond alitoka kapa katika tuzo za MTV MAMA mwishoni mwa wiki iliyopita nchini Afrika Kusini, lakini tayari alikuwa amebeba tuzo ya Afrimma iliyotolewa nchini Marekani hivi karibuni.

Tuzo hiyo iliyomtambua Diamond kama msanii Bora wa Kiume wa Afrika Mashariki, ni moja kati ya tuzo kibao zilizopo katika kabati la msanii huyo, zikiwamo za Channel O, MTV-Base Africa, MTV EMA, BET na nyinginezo.

Pamoja na mafanikio hayo, bado Diamond amekuwa hapewi heshima inayomstahili kutoka kwa baadhi ya Watanzania wenzake.

Japo ni ukweli kwamba si Watanzania wote wanaomshabikia Diamond, lakini inapotokea msanii huyo amefanya kitu kikubwa ambacho mwisho wa siku kinabaki kuwa fahari ya Tanzania, si sahihi kuona kuna wengine wanamponda na kubeza mafanikio yake.

Mathalani, baada ya Diamond kukosa tuzo za MTV MAMA, Watanzania kemkem wameonekana kumbeza kwa hilo kupitia mitandao ya kijamii na hata hadharani.

Ukitafakari kwa makini, utabaini kuwa wanaomponda Diamond Platnumz ni wale ambao wanasahau kuwa mafanikio yake yametokana na kujituma kwake katika kazi yake.

Hao ni wale ambao wanachokumbuka wao ni wapi ametokea msanii huyo, hasa wanapokumbuka picha zake za utotoni akionekana kutoka katika familia duni, huku wakisahau kuwa hata wanasoka wa Kibrazil kama Ronaldo di Lima, Rivaldo, Neymar na wengineo au Mnigeria Nwako Kanu na wengineo wengi, walitokea katika maisha duni kuliko hata ilivyokuwa kwa Dimaond na baadaye kuwa watu maarufu duniani wakimiliki fedha na mali za thamani kubwa.

Wakati mwingine pia unaweza kuwaza kuwa huenda wanaombeza Diamond kutokana na mafanikio yake wanafanya hivyo kwasababu tu msanii huyo ametokea katika mazingira ya kawaida kabisa ya Tandale na si Masaki, Mbezi Beach au Oysterbay.

Unaweza kujiuliza iwapo mafanikio anayoyapata Diamond Platinumz yangekuwa ni kwa msanii Ambwene Yesaya ‘AY’, aliyekulia Masaki, naye angekuwa akibezwa kiasi hicho?

Ni wazi jibu ni hapana. Sasa kwanini iwe hivyo kwa Diamond? Au ni kwasababu ‘kwao ni Mbagala?’ Tafakari.

Mwisho wa siku, Watanzania ni vema wakafahamu kuwa mafanikio ya Diamond kama ilivyo kwa wengineo hapa nchini na kwingineko, hutokana na uwezo, jitihada, umakini, malengo pamoja na mapenzi dhidi ya shughuli husika.

Pamoja na hayo, tulielezea safari ya Diamond tangu alipozaliwa Oktoba 2, mwaka 1989 katika Hospitali ya Amana, Dar es Salaam, kuelekea mafanikio aliyo nayo sasa ambapo tuliishia jinsi alivyopata fedha za kurekodi wimbo wake wa kwanza wa Toka Mwanzo.

Baada ya kuhaha kusaka fedha za kurekodi wimbo wake wa kwanza, aliamua kuuza pete ya dhahabu aliyokuwa amevaa na mama yake aivae.

Msanii huyo katika kufanikisha azma yake hiyo, aliamua kumdanganya mama yake huyo kuwa aliipoteza na hivyo kutumia fedha hizo kuingia studio kurekodi wimbo wake wa Toka Mwanzo.

Hata hivyo, wimbo huo haukufanikiwa kubamba kwani haukuwa katika kiwango cha juu, japo angalau ulianza kumtambulisha kama msanii wa muziki.

Lakini japo kazi yake hiyo haikutamba, angalau ilimfanya aweze kupata marafiki walioshangazwa na uwezo wake wa kuimba, lakini pia kutunga mashairi.

Miongoni mwa watu walioguswa na Diamond na kumsogelea kwa karibu, ni

Chizo Mapene.

Mdau huyo wa muziki hapa nchini, aliamua kumsaidia msanii huyo, lakini alishindwa kutimiza azma yake hiyo baada ya kupata matatizo ya kifedha.

Hali hiyo ilielekea kukatiza ndoto ya Diamond kuwa mwanamuziki kutokana na kukosa mtu wa kumsaidia kurekodi, hivyo kuwa katika wakati mgumu mno.

Matokeo yake, inaelezwa kuwa hata aliyekuwa mpenzi wake kwa wakati huo, aliamua kumwacha mkali huyo kutokana na ‘kufulia’ kwake.

Kama msemo wa Kiswahili unavyosema, ‘mgaagaa na upwa hali wali mkavu’, ndivyo ilivyokuwa kwa Diamond kwani baada ya kuhaha kwa muda mrefu kusaka fedha za kumwezesha kuingia studio, hatimaye mwaka 2009 alikutana na Msafiri Peter ‘Papaa Misifa’ ambapo baada ya mazungumzo, mfanyabiashara huyo alikubali kumsaidia.

Hapo ndipo msanii huyo alipofanikiwa kuingia studio na kurekodi wimbo wake uliojulikana kama ‘Nenda Kamwambie’.

Wimbo huo ulifanikiwa vilivyo kumtambulisha msanii huyo kama mwenye kipaji cha aina yake katika muziki kwani aliimba kwa umahiri wa hali ya juu, huku mashairi yake yakiwa na ujumbe matata wa kimapenzi.

Japo Diamond amekuwa akishindwa kukiri, lakini wimbo huo unaonekana ni kama ‘lilikuwa ni dongo’ kwa mpenzi wake aliyemwacha mkali huyo kutokana na ufukara wake.

Kuanzia wimbo huo, nyota ya Diamond ilianza kung’ara kwa kasi ya aina yake na hivyo kupata mashabiki lukuki kila pembe ya Tanzania na kwingineko.

Muda si mrefu, Diamond alitoa albamu yake ya kwanza iliyokwenda kwa jina la Mbagala ambayo ilikuwa na nyimbo 10.

Nyimbo hizo ni Kamwambie, Mbagala, Nitarejea, Binadamu, Usisahau, Nalia na Mengi, Nakupa, Wakunesanesa, Uko Tayari, Toka Mwanzo na Jisachi.

Albamu hiyo ilimtangaza vilivyo Diamond kwani takribani nyimbo zake zote zilikuwa za kiwango cha juu na hivyo kuwagusa wengi.

Hapo ndipo msanii huyo alipoanza kupata kazi katika maeneo mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi ambapo alifanya shoo za aina yake na kumwezesha kuvuna fedha kadiri alivyoweza.

Pamoja na umahiri wa kuimba na kutunga mashairi yenye kumgusa mtu yeyote, kuanzia masikini hadi matajiri, vijana hadi wazee na wengineo, faida nyingine iliyomsaidia Diamond ni uwezo wake wa kucheza.

Katika shoo zake, Diamond amekuwa akiimba na kucheza kwa umahiri wa hali ya juu, huku akisindikizwa na wanenguaji wake.

Ni kutokana na mafanikio yake hayo, Diamond amekuwa na shauku ya kufanya kazi zake kwa umakini wa hali ya juu, hivyo kufikia hatua ya kurekodi kazi zake nje ya nchi, zaidi ikiwa ni Afrika Kusini.

Hayo yote yamemfanya kuonekana kama Balozi wa Tanzania nje ya nchi kutokana na mafanikio yake, akiwa ametwaa tuzo lukuki.

Mwisho wa siku, mafanikio yote hayo ya Diamond, kuanzia kimuziki hadi kimaisha, yametokana na kujituma kwake katika fani hiyo, lakini zaidi ikiwa ni malengo yaliyobebwa na kipaji chake.

Una lolote la kusema juu ya safari ya Diamond Platinumz? Nitumie kupitia namba ya simu 0622556022 au michietz@yahoo.com

Previous articleKIBONZO
Next articleNO PLUIJM, NO PROBLEM
- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika ujumbe kupitia ukurasa wake wa...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya kinda wa zamani wa timu...

Afua Suleiman afunguka ‘Utalijua Jiji’ ilivyompa ustaa mjini

NA JEREMIA ERNEST JINA alilopewa na wazazi wake ni Afua Suleiman na hata alipojitupa kwenye ulimwengu wa muziki wa...

Keche: Kundi maarufu Ghana linalowatamani Diamond, Kiba, Harmonize

JIACHIE na Staa Wako, wiki hii tumetua mpaka Accra, Ghana kwa kundi maarufu la muziki nchini humo, Keche linofanya vizuri na ngoma...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -