NA ZAINAB IDDY
HUKU ikidaiwa kuwa kocha mtarajiwa mpya wa Yanga, Mzambia George Lwandamina, amehoji ni wapi aliko aliyekuwa kiungo mkabaji wa timu hiyo, Salum Telela, mchezaji huyo ameliambia BINGWA kuwa hana mpango wa kurejea katika kikosi hicho chenye maskani yake Jangwani, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na BINGWA, Telela alisema kwa sasa nguvu zake na akili yake yote ameielekeza katika elimu akichukua masomo ya usimamizi wa biashara.
“Hata kama ikitokea nikaambiwa nirudi Yanga, kutokana na mapendekezo ya huyo kocha mpya, sipo tayari kwani nimeamua kurudi darasani kwa kuwa ndio urithi wangu pekee utakaodumu kwenye maisha yangu, lakini soka ni ajira yenye mwisho.
“Lakini hata kama nitamaliza masomo bado akili yangu haipo tayari kuona narejea Yanga kwa hivi sasa, nitaangalia maisha mengine,” alisema Telela.
Telele aliyedumu na Yanga kwa takribani misimu minne, alitemwa katika kikosi cha Jangwani baada ya msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara kumalizika.