Thursday, October 22, 2020

TIBA YA WAAMUZI WABOVU IPO KUANZIA SHULE ZA MSINGI, SEKONDARI

Must Read

Wanaompenda Carlinhos wapewa dili

NA ASHA KIGUNDULA      MASHABIKI na wanachama wa Yanga, wakiwamo wale wanaovutiwa mno na uchezaji...

UKITELEZA KWISHNEI

NA ASHA KIGUNDULAMIAMBA ya soka nchini, Simba na Yanga, leo wana vibarua vigumu vya kusaka pointi zote...

Director Kenny: Harmonize alinipeleka WCB nikafanya video ya Lavalava

MWONGOZAJI bora wa video nchini, Kenned Sanga a.k.a Derector Kenny kutoka Zoom Extra, ametua   hapa Jiachie na...

 NA HASSAN DAUDI

KUBORONGA kwa waamuzi ni ugonjwa sugu kwenye soka la Bongo. Hakuna anayeweza kulikataa hilo.

Ni nadra kutosikia malalamiko ya uchezeshaji mbovu wa waamuzi kila baada ya mchezo wa Ligi Kuu Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Mbali na ligi kuu, kumekuwa na kelele nyingi kutoka kwa makocha na viongozi wa timu za madaraja ya chini kuhusu waamuzi kushindwa kuzitafsiri sheria 17 za mchezo wa soka.

Nini chanzo cha waamuzi kuboronga huku wakijua umuhimu wao katika mchezo wa soka?

Wapo wanaoamini kuwa waamuzi wamekuwa wakihongwa kiasi cha fedha ili kupindisha sheria kwa lengo la kuzibeba baadhi ya timu katika mchezo husika.

Lakini pia, wapo wanaodai kuwa ni kweli waamuzi wengi wamekuwa wakifanya makosa ya kiweledi kwa kutojua vizuri sheria za soka.

Kwa upande mwingine, wadau wengi wa soka wamekuwa wakishauri njia mbalimbali za kuondoa madudu ya waamuzi uwanjani.

Wapo wanaoamini kuwa njia pekee ya kuwakomesha waamuzi wabovu ni kuwaongezea adhabu pindi wanapovurunda.

Kwa madai yao, faini kubwa na vifungo vya muda mrefu vitaweza kuwafanya waamuzi kuogopa kufanya makosa ya kizembe uwanjani.

Lakini pia, inaaminika kuwa kwa kuwafutia leseni za kuchezesha, itasaidia kuondoa tatizo la wamuzi wabovu kwenye medani ya soka la Tanzania.

Huenda zote hizo zikawa njia sahihi za kuondoa waamuzi ambao wamekuwa wakikwamisha maendeleo ya soka hapa nchini.

Lakini je, tumewahi kujiuliza ni wapi wanakotokea hao tunaowaita waamuzi wasio na viwango?

Ukijaribu kuchunguza kwa makini, unaweza kugundua kuwa bado Tanzania imekuwa nyuma katika kuibua vipaji vya wanafunzi wanaoonyesha nia ya kuwa waamuzi wa baadaye.

Hata wadau wanapozungumzia suala la michezo kupelekwa katika shule za msingi na sekondari, kundi hili la waamuzi huwa halipo vichwani mwao.

Mara nyingi hufikiria michezo shuleni huibua walinda mlango, mabeki, viungo, na mastraika pekee.

Ni wachache tu wanaoweza kwenda mbali kifikra na kutaka michezo hiyo kuibua waamuzi na makocha chipukizi.

Kwa kulisahau kundi hilo, hapo ndipo tunapojikuta tukiwa na waamuzi ambao hawakuandaliwa mapema.

Kama kungekuwa na mpango mzuri wa kuwaibua wanafunzi wenye vipaji vya kuwa waamuzi, basi leo hii kusingekuwa na kelele za maamuzi mabovu viwanjani.

Ni wazi kuwa tatizo la waamuzi vimeo limesababishwa na kukosekana kwa misingi imara. Kutokana na mfumo mbovu ulioppo sasa kwenye soka letu, waamuzi wengi huanza ‘kozi’ wakiwa na umri mkubwa.

Ndiyo maana imekuwa rahisi kwa mwanafunzi mwenye uwezo wa kusakata kabumbu kutokana na kusajiliwa na timu kubwa kuliko yule mwenye nia ya kuwa mwamuzi.

Mbali na kushindwa kuzitafsiri sheria 17 za mchezo wa kandanda, waamuzi wengi wamekuwa wakishindwa kufanya kazi katika maadili ya kazi hiyo na ndiyo maana wamekuwa wepesi kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Ikiwa chimbuko la waamuzi lingeanzia kwenye shule za msingi ambako kuna idadi kubwa ya watoto, ni wazi misingi imara ya miiko ya kazi hiyo ingeanzia huko.

Katika shule zetu, kuna idadi kubwa ya vijana wanaotamani kuwa waamuzi lakini wanakosa misingi ya namna hiyo.

Ni wakati wa Chama cha Waamuzi Tanzania kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka hapa nchini (TFF) kuhakikisha mafunzo ya uamuzi wa soka yanaanzia katika ngazi za chini, kwa maana ya shule za msingi na sekondari.

Kama tutaendelea kutegemea waamuzi wanaoibuka wakiwa na umri mkubwa, huenda tukaendelea kushuhudia haya yanayotokea mara kwa mara viwanjani.

Waamuzi wataendelea kupokea vipigo huku miundombinu ya viwanja vyetu ikiendelea kuharibiwa na wale watakaoshindwa kuzuia hasira zao kutokana na uzembe wa waamuzi.

Hata hivyo, huenda hatuwatendei haki waamuzi kwa kiasi fulani. Mashabiki wa soka wamekuwa wepesi sana kuwatupia lawama waamuzi bila kujiuliza chanzo cha kuvurunda kwao.

Ni lini imetokea kusikia mashabiki wakiwajia juu TFF kushinikiza maboresho ya masilahi ya waamuzi? Hebu tufikirie kuhusu hilo.

Ni mara ngapi waamuzi wamekuwa wakipaza sauti kudai kuwa fedha wanazolipwa na TFF hazikidhi mahitaji?

TFF jaribuni kuliangalia hilo kwa makini kwani masilahi mabovu kwa waamuzi yanatajwa kuwa sababu ya waamuzi kupokea rushwa kutoka kwa baadhi ya timu vigogo.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Wanaompenda Carlinhos wapewa dili

NA ASHA KIGUNDULA      MASHABIKI na wanachama wa Yanga, wakiwamo wale wanaovutiwa mno na uchezaji...

UKITELEZA KWISHNEI

NA ASHA KIGUNDULAMIAMBA ya soka nchini, Simba na Yanga, leo wana vibarua vigumu vya kusaka pointi zote tatu katika mechi za Ligi...

Director Kenny: Harmonize alinipeleka WCB nikafanya video ya Lavalava

MWONGOZAJI bora wa video nchini, Kenned Sanga a.k.a Derector Kenny kutoka Zoom Extra, ametua   hapa Jiachie na Staa Wako, safu inayokupa nafasi...

Rogers mwanamuziki anayevutiwa na Marijani

NA JEREMIA ERNEST BONGO Star Search (BSS), ni shindano lililofanikiwa kuibua vipaji vingi vya wanamuziki wa Tanzania ambao miongoni...

Ihefu, Azam patachimbika Sokoine, Katwila ndani

NA ASHA KIGUNDULATIMU ya Ihefu inatarajia kushuka uwanjani kucheza na Azam ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara  (VPL), utakaochezwa leo...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -