NA ZAINAB IDDY
ZIKIWA zimebaki siku chache kupigwa kwa pambano la watani wa jadi Simba na Yanga, wachezaji wa timu ya Simba juzi jioni waliwekwa kitimoto na mabosi zao.
Simba na Yanga zitakutana Agosti 23, mwaka huu katika mchezo wa Ngao ya Jamii unaoashiria ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2017/18, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Taarifa ambazo BINGWA limezipata kutoka ndani ya kambi ya Simba iliyopo Unguja, Zanzibar, zinasema kuwa licha ya benchi la ufundi kuongeza dozi ya mazoezi, pia wamelazimika kukaa na wachezaji na kuzungumza nao pamoja na viongozi waliopo visiwani humo.
“Kwa sasa tunafanya mazoezi asubuhi na joini, lakini jana (juzi) baada ya chakula cha usiku tuliitwa wachezaji wote na kukaa na benchi la ufundi na viongozi waliokuwepo kwa takribani saa mbili kuzungumzia mechi iliyopo mbele yetu.
“Kikubwa tulitakiwa kutambua namna mechi hiyo ilivyo na presha kwa mashabiki, hivyo ili kuwafurahisha ni lazima tuifunge Yanga kwa idadi kubwa ya mabao na kuchukua kombe,” alisema mmoja wa wachezaji.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa, mbali na kupewa majukumu hayo pia walitakiwa kuwa makini na kuongeza juhudi vinginevyo wanaweza kupoteza mechi dhidi ya Yanga.
“Tumeambiwa kuwa mpira hauwezi kuingia golini wenyewe, hivyo kila mmoja anatakiwa kujituma kwa nafasi yake ili kuhakikisha timu inapata matokeo, kwani baadhi ya viongozi wameahidi zawadi kwa wachezaji watakaoonyesha kiwango bora uwanjani,” alieleza.