Saturday, October 31, 2020

‘Uhuni’ huu wa soka tumeutoa wapi?

Must Read

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya...

NA HASSAN DAUDI,

USIPOZIBA ufa utajenga ukuta, ni msemo maarufu sana miongoni mwa jamii zetu. Msemo huu unamtahadharisha mtu kuwa kitendo cha kupuuza tatizo dogo, kinaweza kumsababisha kujikuta akitumia nguvu na mali nyingi kulitatua pindi likiwa kubwa.

Kwa kiasi fulani, msemo huo unashabihiana na ule usemao tabia hujenga mazoea, yaani ukiwa na kawaida ya kufanya kitu fulani, kuna kipindi hutoweza kukiacha, licha ya ukweli kwamba kinaweza kuwa na madhara kwa upande wako.

Nimeanza na misemo hiyo ya Kiswahili ikiwa ni katika kujaribu kuakisi kile kilichotokea juzi katika mchezo wa mahasimu Simba na Yanga.

Mtanange huo unaofahamika kama ‘Kariakoo derby’, ulikuwa ni wa kwanza kuwakutanisha wababe hao wa Ligi Kuu ya Vodacom Bara kwa msimu huu wa 2016-17.

Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kuziona nyavu za Simba kupitia kwa bao la mshambuliaji hatari raia wa Burundi, Amis Tambwe, katika dakika ya 26.

Mahasimu wao, Simba walichomoa bao hilo zikiwa zimesalia dakika chache kabla ya kumalizika kwa mchezo huo, baada ya mpira wa kona uliopigwa na Shiza Kichuya kutinga wavuni moja kwa moja.

Ikumbukwe kuwa Simba walipata bao hilo la kusawazisha, licha ya kucheza wakiwa pungufu baada ya kiungo wao Jonas Mkude kulimwa kadi nyekundu baada ya kuzozana na mwamuzi wa mchezo huo, Martin Saanya.

Ukweli ni kwamba, mbali na mapungufu yaliyojitokeza ambayo ndiyo kiini cha makala haya, timu zote zilionyesha soka la kuvutia.

Pongezi zaidi zinapaswa kuelekezwa kwa Simba, ambao licha ya kuwa pungufu kwa sehemu kubwa ya mchezo huo, walipambana na hatimaye kupata bao la kusawazisha.

Hata hivyo, kama nilivyosema hapo awali, kuna kasoro ambazo zilijitokeza katika mchezo huo na kama zitaendelea kujitokeza katika siku zijazo, huenda Tanzania ikakumbana na rungu la Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Ukiachana na FIFA, vitendo hivyo vinaashiria kuwa huenda ipo siku Tanzania itashuhudia vifo vya mashabiki viwanjani kama ambavyo imekuwa ikitokea katika nchi za wenzetu.

Baada ya Tambwe kuipatia Yanga bao katika kipindi cha kwanza, mashabiki wa soka wanaoaminika kuwa ni wa Simba, walifanya kile kinachoweza kuelezwa kuwa ni ‘ushamba’ wa soka.

Huku FIFA wakiwa na kampeni nyingi za kuhamasisha amani katika mchezo wa soka, kwa mashabiki hao hali ilikuwa tofauti. Kwao, mchezo wa soka ulikuwa na maana ya vita kati ya pande mbili.

Mashabiki hao hawakukubaliana na bao la Tambwe, wakidai kuwa alitumia mkono kuuweka vizuri mpira kabla ya kupasia nyavu na kilichowakera zaidi ni kadi nyekundu aliyopewa Mkude.

Ni kweli hawakuridhishwa na maamuzi ya mwamuzi Saanya, lakini je, kuvunja viti na kurusha chupa uwanjani ilikuwa ni njia sahihi ya kupingana maamuzi hayo?

Ni matukio ambayo hayatakiwi kupewa nafasi katika michezo mingine ijayo, kwani inahatarisha usalama viwanjani.

Inapaswa kufahamika kuwa, kama mwamuzi alikosea, alitakiwa kuwajibishwa na waajiri wake ambao ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na si mashabiki.

Ni rahisi kubashiri kuwa waliofanya vitendo vya vurugu hawakuwa sehemu ya jamii ya soka, ni wahuni fulani waliovamia mchezo huo wa kistaarabu.

Kisheria, refa akiwa na wasaidizi wake, ndiyo wenye uamuzi wa mwisho kwa kile kinachoendelea uwanjani.

Ndiyo maana hata mashabiki wa Simba walipofanya kila aina ya vurugu, matokeo hayakubadilika mpaka pale Kichuya aliposawazisha.

Je, kama vurugu zao hazikubadili matokeo, kulikuwa na umuhimu gani wa wao kuharibu mandhari ya uwanja huo uliojengwa kwa kodi yao na Watanzania wengine ambao si wapenzi wa soka?

Lakini pia, ikumbukwe kuwa mwamuzi naye ni binadamu kama walivyo mashabiki, si rahisi kuamini kuwa atakuwa sahihi kwa kila atakachokiona katika mchezo husika.

Kama ilivyo kwa viongozi, wachezaji, mashabiki, hata waamuzi huwa na presha kubwa wanapochezesha mechi kati ya Simba na Yanga, hivyo kuna muda hujikuta wakizidiwa nguvu na kimuhemuhe cha pambano hilo na hatimaye kutoka mchezoni.

Kama mashabiki wale wanaodhaniwa kuwa wa Simba wangelifikiria hilo, ni wazi wangeachana na kile walichokifanya na badala yake wangeishinikiza TFF kumuadhibu mwamuzi huyo.

Lakini pia, hata baada ya kuanzisha vurugu hizo kutokana na kukerwa na bao la Tambwe na kadi nyekundu ya Mkude, walifanya hivyo pia baada ya Kichuya kuisawazishia Simba bao.

Hakuna namna ambayo unaweza kujenga hoja kutetea uhuni wa ‘wapuuzi’ wale na itashangaza kama atatokea kiongozi au mchezaji atakayekuwa upande wao.

Vurugu hazikuwa na msingi, ingawa huenda kile walichokilalalamikia kilikuwa cha msingi.

Ni matukio kama haya ndiyo yaliyosababisha mpaka leo baadhi ya michezo ya Ligi Kuu Misri imekuwa na kiwango maalumu cha mashabiki wanaoruhusiwa kuingia uwanjani.

Miaka kadhaa iliyopita, zaidi ya mashabiki 70 wa mabingwa wa ligi kuu nchini humo Al-Ahly, walipoteza maisha katika mazingira kama hayo.

Kwa kile kilichotokea juzi, ni wazi ipo siku hilo litatokea katika moja ya michezo ya hapa Tanzania.

Kwanini Tanzania ifikie huko kwa ujinga wa watu wachache ambao vitendo vyao hivyo vimewatofautisha na wanamichezo wengine?

Huenda hilo linatokana na adhabu dhaifu ambazo hutolewa na TFF kila matukio kama hayo yanapojitokeza.

Barani Ulaya, matukio hayo ya ajabu hupewa uzito mkubwa na mara nyingi timu ambayo mashabiki wake wamehusika, hulazimika kucheza baadhi ya mechi zake bila sapoti ya mashabiki.

Bila shaka huu ni wakati mwafaka kwa TFF kufanyia kazi sheria hiyo ambayo kwa kiasi fulani imepunguza matukio ya kihuni viwanjani barani Ulaya.

Bila kupoteza maana ya kile ninachokisema, TFF waanze na timu ambayo mashabiki wake walivunja viti Taifa juzi, wapewe adhabu ya kucheza bila mashabiki.

Ukiacha hilo la mashabiki, ni wazi kabisa kuwa mbali na mashabiki, hata wachezaji wa Tanzania hawajielewi.

Kadi nyekundu aliyopewa nahodha Mkude iliakisi weledi mdogo walionao wachezaji wetu na ndiyo maana wamekuwa wakiishia VPL huku wenzao wa Afrika Magharibi ‘wakitusua’ barani Ulaya.

Ni kweli mashabiki wengi wana uelewa mdogo wa sheria za soka, hasa ile ya nguvu ya mwamuzi katika mchezo, lakini hata staa kama Mkude anayechezea timu kubwa kama Simba?

Kwa kubishana na mwamuzi, huku akijua umuhimu wake kikosini katika mchezo dhidi ya Yanga, ni wazi amejitia aibu na kujiweka kundi moja na mashabiki wake. Wassalamu.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika ujumbe kupitia ukurasa wake wa...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya kinda wa zamani wa timu...

Afua Suleiman afunguka ‘Utalijua Jiji’ ilivyompa ustaa mjini

NA JEREMIA ERNEST JINA alilopewa na wazazi wake ni Afua Suleiman na hata alipojitupa kwenye ulimwengu wa muziki wa...

Keche: Kundi maarufu Ghana linalowatamani Diamond, Kiba, Harmonize

JIACHIE na Staa Wako, wiki hii tumetua mpaka Accra, Ghana kwa kundi maarufu la muziki nchini humo, Keche linofanya vizuri na ngoma...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -