Tuesday, November 24, 2020

Ujumbe mzito aliouacha Mashali

Must Read

BEN POL AJA NA HIYO NDIO MBAYA

Na Mwandishi Wetu MSANII nguli wa muziki wa R&B na Bongo Fleva Benham Paul...

ZILE NI SALAM TU

NA MWANDISHI WETU KIPIGO cha mabao 7-0 walichokitoa Simba juzi kwa Coastal Union katika...

DEWJI: CHAMA NI SIMBA HADI 2022

Kiungo huyo raia wa Zambia, aliyetoa mchangomkubwakwaSimbakufikisharobo fainaliyaLigiyaMabingwaAfrikamsimuwa 2018/19, ikiwamo kutwaa ubingwa wa LigiKuuTanzaniaBarakwa misimumitatu mfululizo, awali...

NA ALLY KAMWE,

SAA sita mchana, Oktoba 13, 2016, jua la utosi likianza kuitesa dunia, tulishuka katika basi dogo na kuikanyaga ardhi ya Mji wa Bagamoyo kwa mara ya kwanza kwenye maisha yangu, kwani sikuwa nimefika kabla.

Hatukuwa na muda wa kupoteza, mwenzangu Martin Mazugwa, alitoa simu yake mfukoni na kumpigia mwenyeji wetu, “haloo Mashali”, aliongea kwa sauti iliyochoka kidogo.

“Niambie dogo,” ilisikika sauti ya Mashali akiwa mwenye hamu ya kutaka kujua tulipofika. Kama kumbukumbu zangu zipo sawa, nafikiri ilikuwa mara ya saba kuzungumza naye kwa simu tangu tulipoanza safari ya kutoka kituo cha mabasi cha Makumbusho, Dar es Salaam, mnamo saa tatu asubuhi.

“Tumeshashuka,” aliongea Mazugwa kabla ya kukatishwa kauli yake na Mashali, “Ok dogo, nipe dakika tatu tu nafika hapo.”

Baada ya maongezi hayo mafupi, nililiweka vyema begi langu mgongoni na kuangaza macho yangu katika kila pembe nikitafuta eneo lenye kivuli tukapumzike, sijawahi kumwamini ‘Mswahili’ kwenye ahadi, niliamini tulikuwa na zaidi ya dakika tatu za kusubiri.

“Oya dogo, tusogee pale, hili jua la Bagamoyo nahisi lina undugu na lile tuliloliacha Dar,” nilitania ili kuirejesha tumaini kwenye paji la uso la Mazugwa; alifurahi na tukasogea pembezoni kidogo na lililo geti kuu la kuingilia mabasi pale Bagamoyo.

“Anapiga,” alisema mwenzangu kwa kushtuka huku akinionyesha simu yake, nilitabasamu kwa mshangao! ‘Mashali ana ahadi za Kizungu kumbe’, nilijisemea moyoni huku nikijiweka sawa kuonana na mwenyeji wetu.

“Njoo kwenye hii gari nyeusi hapa kwenye kona ya kuingilia kituoni,” kwa kuwa simu iliwekwa ‘loud speaker’, niligeuza haraka macho yangu hadi kwenye eneo alilotuelekeza Mashali.

“Wale pale,” nilisema huku nikimuonyesha Mazugwa lilipo gari. “Tumewaona, poa tunasogea hapo,” alijibu mwenzangu na kukata simu. Hatukuwa na sekunde ya kupoteza pale, tulianza safari kulifuata gari jeusi. Ulikuwa mwendo wa hatua kama 20 hivi.

“Vipi, mbona mmepaki gari barabarani nyie,” alifoka trafiki mbele ya dereva wa ile gari ndogo nyeusi. “Ooh ‘sorry’ kaka, tulikuwa tunawasubiri hawa madogo, ni waandishi wa habari,” alijibu kwa kujiamini dereva.

“Sasa mmeshindwa kupaki pembeni, hamuoni kama mnaweza sababisha foleni hapa,” aliendelea kufoka yule askari wa usalama barabarani. Ghafla kipande cha mtu kilichokuwa kimejilaza kwenye siti ya mbele, kushoto mwa dereva kikainuka, alikuwa ni Thomas Mashali.

“Kaka unatukazia hata sisi?” Alihoji Mashali huku macho yake yakigongana na ya yule trafiki. “Ah Mashali!” alishangaa trafiki kisha kikafuata kicheko, tulicheka wote.

Sekunde, yule trafiki alimpa mkono Mashali na kusalimiana, kesi ikaishia pale. “Pandeni madogo,” alisema dereva huku akitufungulia mlango wa nyuma. “Usupastaa raha sana”, nilijisemea huku nikipanda kwenye gari kuanza safari.

Haikuwa safari ndefu sana, ni mwendo wa dakika 5 tu, tukafika eneo aliloweka kambi Thomas Mashali akijiwinda na mapambano mawili makubwa, dhidi ya Mmalawi na lingine nje ya nchi, yote alipanga kupigana kabla mwaka huu haujamalizika.

Tulizungumza mengi mno, hali ya ngumi Tanzania kwa sasa, wapi tunakwama na nini kifanyike. Nakumbuka alinipa agizo la kumpa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye kama Mungu akimchukua kabla hajaonana naye, Inaumiza sana!

“Kamwe mdogo wangu, kama nikifa leo bila kuonana na Waziri Nape, mwambie atupe jicho lake na kwenye ngumi, sio kila siku anakomaa na soka tu. Watoto wa masikini wengi huku wanavuja jasho bila faida yoyote, tunaumia sana na hamna tunachopata zaidi ya hela za kulipia ada watoto tu,” aliniambia Mashali huku akinigusa bega.

Mungu muweza wa kila kitu, mfalme wa viumbe vyote, baba yetu aliye juu mbinguni, hajawahi kukosea, siku 18 baada ya kuagana na Mashali kule Bagamoyo, amemchukua kiumbe wake!

Futi sita chini ya ardhi, utalala mwili wa ‘Rais wa Ghetto’, ‘Simba Asiyefugika’, hatutamwona tena mpaka hapo yatakapokuja tena maisha mengine baada ya haya, pumzika mahali pema peponi bingwa!

Nakumbuka utani wako kwa Fransic Cheka, leo umemuacha peke yake. Atapata wapi tena rafiki wa kubadilishana naye mawazo katika harakati za kuutoa mchezo wa ngumi kwenye kiza kinene? Tutakukumbuka daima bingwa wetu.

Mwisho uliniusia, siku watu watakapojikusanya na kusimulia mabaya yako, nisiache kuwasimulia mazuri yako machache ninayofahamu. Nikuahidi, sitaacha, nitasimulia kaka!

Ulipambana kwa nguvu zako na jasho lako kusaka tonge kwa ajili ya familia yako, unatosha ushujaa huo, mengine ni udhaifu wetu tu wa kibinadamu ambao wewe, mimi na yeyote yule, ameumbwa nao ndani yake, tutakukumbuka daima!

Nenda Mashali, naamini umekufa kabla ya kifo chako. Mipango yako uliyoniahidi kuifanya ndani ya miaka miwili ijayo, imefutika milele! Mungu mpangaji wa kila kitu, amepanga wakati huu urejee mbele yake, safari njema bingwa!

Kalamu yangu ina mengi ya kusema, ila kwa sasa acha nikuache upumzike. Nitampa salamu zako Waziri Nape, nitampa salamu zako Rashid Matumla, nitampa pia salamu zako mke wako mpendwa, huenda alikuwa hafahamu, lakini ukweli ni kuwa umekufa akiwa anaishi ndani yako.

Nenda msalimie mama yako kipenzi, zile ‘tattoo’ za machozi ulizochora chini ya macho yako zitatosha kumwonyesha ni namna gani uliishi ukimlilia tangu alipokutoka, msalimie sana, mwambie alizaa bingwa aliyeacha kumbukumbu nyingi mno kwenye mioyo ya Watanzania, safari njema kaka!

Usikose nakala yako ya BINGWA la Jumanne ya wiki ijayo kupata simulizi zaidi kuhusiana na Thomas Mashali, zaidi ikiwa ni visa na vituko mbalimbali vilivyokuwa vikimwandama, lakini pia jinsi rafiki na washindani wake wanavyomzungumzia.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

BEN POL AJA NA HIYO NDIO MBAYA

Na Mwandishi Wetu MSANII nguli wa muziki wa R&B na Bongo Fleva Benham Paul...

ZILE NI SALAM TU

NA MWANDISHI WETU KIPIGO cha mabao 7-0 walichokitoa Simba juzi kwa Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania...

DEWJI: CHAMA NI SIMBA HADI 2022

Kiungo huyo raia wa Zambia, aliyetoa mchangomkubwakwaSimbakufikisharobo fainaliyaLigiyaMabingwaAfrikamsimuwa 2018/19, ikiwamo kutwaa ubingwa wa LigiKuuTanzaniaBarakwa misimumitatu mfululizo, awali ilidaiwa alikuwa yupo katika hatuayamwishoyakujiunganaYanga.

Sven aruka kihunzi

NA ASHA KIGUNDULA KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, ameruka kihunzi na kuwaachia msala nyota wake, Clatous Chama na...

Sarpong ‘aua’ shabiki Simba

Na MWANDISHI WETU, MWANZA BAO la dakika ya 29 lililofungwa na Michael Sarpong wa Yanga juzi, limesababisha kifo cha...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -