Friday, October 30, 2020

Upendo kushinda Ufahamu [18]

Must Read

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya...

Ilipoishia jana

Uamuzi aliokuwa ameufikia ni kuamua kumfuata Roika nchini Mexico, akijua kuwa Roika yuko huko kikazi.

SASA ENDELEA

NCHINI HAITI

UZIMA ndani ya kidonda cha mapenzi ulianza kuonekana kwa Roika. Alijiona mwepesi kidogo tofauti na siku zote. Kuwepo pembeni ya Ramona kulimpa matumaini makubwa ya kufanikiwa kumuoa mrembo huyo wa dunia.

Siku hiyo walikuwa wametoka nje ya hoteli ya Lompi kama walivyokuwa wamepanga. Walitembea huku na kule ndani ya jiji la Ampiana lililoko kusini mwa nchi ya Haiti. Walipita sehemu nyingi za starehe, wakifurahi na kuongea mengi. Kila mtu aliyewatazama alijua watu hao ni wachumba au mke na mume.

Licha ya Roika kuwa na amani, lakini moyo wake ulizidi kumjulisha kuwa, asijivune sana, bado Ramona hajawa wake. Maneno hayo yaliyokuwa yanamjia mara kwa mara, ndiyo yaliyokuwa yanamnyima raha, maana kuna muda mwingine alikuwa akijisahau, akijua kuwa tayari yeye na Ramona ni wapenzi.

Siku hiyo ya matembezi yao ilikuwa ni njema machoni pa Roika, aliyekuwa ameamua kumfuata mrembo huyo nchini humo na kuacha kurudi Tanzania, kwa mpenzi wake Biyanah. Roika alianza kuonyesha wazi kuwa anampenda Ramona, alifanya hivyo makusudi  ili Ramona alitambue hilo.

Baada ya kuzunguka sana katika mitaa mbalimbali, Roika na Ramona walikuwa wanarudi hotelini, njiani walitaniana na kuongea mengi. Hakika Roika alifarijika kwa kiasi kikubwa. Hata ingetokea Ramona akatae kuwa mpenzi wake, Roika angeomba awe anashinda naye muda wote. Maana mapenzi kwake yalishakuwa ni zaidi ya ugonjwa wa Ebola.

Saa mbili usiku walikuwa wanawasili hotelini, baada ya kutwa nzima kuzunguka katika jiji la Ampiana. Ramona alipitiliza chumbani kwake ambako aliingia kuoga, hali kadhalika Roika naye aliingia kuoga akakaa kumsubiri Ramona ili waongee kabla ya kwenda kulala.

Haukupita muda Ramona aliingia chumbani kwa Roika akiwa amevaa nguo ya kulalia, maungo yake yalionekana vizuri, kitambaa chepesi cha nguo hiyo kilimfanya Roika kuuona mwili mzima wa Ramona. Hakika aliteseka sana, hisia za mahaba zilimjia haraka. Aliishia kujikaza kiume, maana ndicho alichokuwa amebakiza mbele ya mrembo wa dunia Ramona Fika.

Licha ya Roika kuonyesha yote yale na kutesekea usiku na mchana kwa ajili ya Ramona, lakini Ramona yeye alikuwa mbali sana na hisia za mapenzi. Hakuonyesha dalili zozote kuwa ametokea kupenda, zaidi mambo yake yote anapokuwa na Roika aliyafanya na kuyaongea kiurafiki zaidi.

Roika kila akitaka kunyanyua ulimi wake amtamkie Ramona kuwa anampenda, akili yake iligoma kufanya hivyo. Muda mwingine aliogopa, akihofia kumuudhi Ramona.

Wakiwa wamekaa huku wakipata vinywaji mbalimbali, Roika alimwambia Ramona.

“Tumetembea sana katika mji huu, lakini hatujawatembelea wahanga wa tetemeko, tumefanya kosa kubwa sana.”

“Ni kosa lako Roika, kwa nini haukunikumbusha?” Ramona aliuliza.

“Wote tuna makosa, kwa nini na wewe ulisubiri mimi nikukumbushe, haujui watu wanahitaji misaada ili waendelee kuishi kama wengine,” Roika alijibu kwa swali.

“Unajua Roika matembezi yetu ya leo yalikuwa ni mazuri sana hadi tukasahau kuwatembelea  wahanga hao. Hata hivyo hakijaharibika kitu, kesho tutakwenda.”

“Hapo ndipo napokupendea unaonyesha kujali. Kesho asubuhi tutaelekea kwanza ubalozini,” aliongea Roika kwa tabasamu pana.

“Sawa Roika tutakwenda.”

Maongezi yao yaliendelea hadi saa 4:45 usiku, Roika alikuwa anaomba kimoyomoyo Ramona aelekee chumbani kwake kupumzika ili asije kumuona yule muhudumu aliyeitwa Sarah ambaye Roika alimwambia kuwa aje saa tano usiku, ingawa alikuwa anapenda kuendelea kukesha na Ramona lakini, alihofia binti huyo asije mharibia safari yake ya kusaka penzi la Ramona.

Baadaye kweli Ramona alianza kulegea kutokana na kusinzia, ukizingatia alikuwa amekunywa na pombe basi, hali yake ilikuwa si nzuri, alikuwa amechoka sana. Aliamua kumuaga Roika kuwa anakwenda kulala. Kwa tabasamu nzuri na macho ya kulegea kutokana na usingizi, alimwambia Roika:

“Roika rafiki yangu kipenzi, mimi nakwenda kulala naomba unishike, nisaidie kuinuka, maana nimechoka sana.”

Maneno hayo yalikuwa yamemfanya Roika kufarijika sana, kwa mara ya kwanza toka afahamiane na Ramona, alimshika bega la kulia kwa kupitisha mkono wake nyuma ya mgongo wa Ramona na mkono mwingine akavishika vidole vyake, vidole vilivyokuwa laini,  akamsaidia Ramona kuinuka pale kwenye sofa na kupiga hatua kuelekea chumbani kwake. Mwili wa Roika ulikuwa katika mateso makubwa ya kimahaba, alijihisi amekuwa kiumbe kipya. Alitetemeka huku jasho jembamba likimtiririka. Hakuamini kama amemshika Ramona, mwanamke aliyekuwa akimuota kila asubuhi, kila mchana, kila jioni na kila usiku.

Chumba kimoja cha mgeni ndani ya hoteli hiyo kilikuwa na sebule pamoja na chumba cha kulala, bafu na sehemu ya makabati. Roika alimpeleka Ramona hadi sebuleni kwake.

“Inatosha Roika, asante sana nawe nenda ukajipumzishe,” aliongea Ramona aliyekuwa ameushikilia mlango huku akitabasamu, ilionyesha pombe zilikuwa zinazidi kummaliza nguvu.

“Sawa, usiku mwema,” alijibu Roika kwa shingo upande, maana alikuwa akitamani kuendelea kumshika mrembo Ramona.

“Nawe pia good night my friend,” alijibu Ramona.

Roika alitoka mle chumbani akiwa hajaridhika kuitwa rafiki, aliumia sana maana yeye alitamani aitwe mpenzi na majina mengine yanayofanana na hilo. Alirudi chumbani kwake, akajifungia mlango na kujitupa kitandani. Baadaye akili ilimtuma kuiwasha simu yake ya mkononi, mawazo yake yalihamia kwa Biyanah, mwanamke anayeteseka kwa ajili yake. Roika hakujua ataushinda vipi mtihani huo wa kumuacha Biyanah na kuendelea na Ramona. Alimuonea huruma mtoto huyo wa bilionea Branko Rumo ambaye anapigana vikali na moyo wake unaompenda Ramona.

Usiku huo alishtuka sana baada ya kuona jumbe zaidi ya 50 kwenye akaunti yake ya Twitter, jumbe ambazo Biyanah alikuwa amemtumia akihitaji kujua yuko wapi, anafanya nini na atarudi lini, maana siku tatu zilikuwa zimekwisha na sasa inaelekea ya nne.

Aliziona picha ambazo Biyanah amemtumia zikimuonyesha mwanamke huyo akiwa katika majonzi na uchovu wa kutosha. Ilitia sana huruma, Roika aliumia kupita kawaida. Akiwa katika maumivu hayo, simu yake ilianza kuita, alipoitazama alikuwa ni Biyanah anayempigia. Hakuwa na nguvu ya kuipokea kutokana na kukosa jibu la kumpa mpenzi wake.

Mapenzi ya Roika na Biyanah yalianza siku tatu zilizopita, kabla Roika hajakutana na Ramona ndani ya ndege. Kwa kuwa akili ya Roika ilikuwa imekata tamaa na namna ya kumpata Ramona, mrembo wa dunia, ndipo akaamua kumkabidhi Biyanah moyo wake, moyo uliokuwa unampenda zaidi Ramona.

Hakuwa na uwezo wa kuipokea simu ya Biyanah, alibaki kuitazama kwa huzuni, asijue cha kufanya, maana hakujua atajibu nini na ataeleza lipi ili Biyanah apate kumuelewa. Simu ilikatika na kuanza kuita tena. Baada ya muda kulikuwa na simu saba zilizokuwa  hazijapokelewa (missed calls).

Baadaye simu haikuita tena, Roika alihuzunika sana, alipanga kumpigia Biyanah kesho asubuhi. Usiku huo alilala kwa shida kutokana na akili yake yote kuipelekea kwa Ramona, alikumbuka matukio yote waliyoyafanya katika matembezi yao ya kuanzia asubuhi hadi jioni, kicheko na uzuri wa Ramona vilizidi kuuchana moyo wa Roika, aliamini kabisa kuwa hawezi kuishi bila Ramona.

Usiku huo alipanga ikifika kesho, amwambie Ramona kuwa anampenda,  tayari alikuwa ameandaa kila aina ya silaha kutoka moyoni mwake, kwa ajili ya kumshambulia Ramona Fika, sasa alikuwa amejivika ujasiri yeye kama mwanamume.

“Siwezi kuishi maisha kama kunguru. Kila siku naumia mimi tuuuu!, wakati nafasi na wakati wa kumwambia Ramona kuwa nampenda upo tena  upo wa kutosha. Nina subiri nini, ninamsubiri Ramona mwenyewe aseme ananipenda? Huo utakuwa ni ujinga tena upumbavu wangu wa kutosha, ambao huenda utanigharimu hapo baadae. kesho ndio siku ambayo nitamwambia Ramona kuwa nilisafiri kutoka Mexico kuja hapa si kwa kitu kingine zaidi ya kumfuata yeye. Nitamwambia Ramona wewe ni mwanamke uliyeigusa mishipa ya moyo wangu kwa kiasi chote. Nimekuwa katika mateso makubwa ya mapenzi kwa muda mrefu. Nakupenda sana, tena sana, zaidi na zaidi. Moyo wangu unahitaji uhuru wa kuishi na uhuru huo unapatikana kwenye muziki wenye tenzi za rohoni kutoka kwako. Kilio changu kimevuka vilindi vya bahari. Nahitaji uwe mke wangu ambaye utaushikilia usukani wa merikebu yetu yenye familia ya watoto wazuri. Nakupenda Ramona,” alijisemea Roika peke yake kama mtu aliyechanganyikiwa.

Akiwa katika mawazo hayo, kengele ya kumjulisha nje kuna mtu anagonga ililia. Roika alishtuka, akijua kabisa kuwa huyo ni Sarah, mhudumu wa hoteli aliyekuwa amemuahidi jana kuwa aje saa tano usiku. Lakini hakwenda kufungua mlango.

Ni kweli Sarah alikuwa mlangoni akibonyeza kengele ili Roika amfungulie. Lakini dakika kumi nzima zilipita Roika hakuja kumfungulia. Machozi yalianza kumtoka Sarah, maana ni muda mrefu tokea alipoanza kugonga. Aliamua kukaa pale nje ya mlango, huku akiulaumu moyo wake kwa kumpenda mwanamume asiyempenda.

Ingawa mwanzo hakuhitaji kufanya mapenzi na Roika, lakini alianza kutamani hata kulala na Roika kwa usiku mmoja. Lakini kila alipozidi kubonyeza kengele ili Roika amfungulie ndio kwanza huku ndani Roika alikuwa tayari usingizini akimuota Ramona. Sarah alipitiwa na usingizi pale mlangoni kwa Roika hadi ilipofika saa kumi alfajiri. Ambapo aliamua kurudi katika vyumba vya wahudumu wenzake wa hoteli, maana saa 11 ilitakiwa aingie kazini.

Asubuhi ilipofika, asubuhi ya saa mbili Roika aliamka akiwa mchovu sana. Huku akiifikiria siku hiyo iliyokuwa ni siku ya hukumu kwenye penzi lake kwa Ramona. Siku ambayo alipanga kuwa atamtamkia Ramona kuwa anampenda.

Baada ya kuoga alivaa shati lake jeupe na kuelekea chumbani kwa Ramona. Alipofika alibonyeza kengele ili Ramona aje kumfungulia. Roika alishtuka kuona anayemfungulia mlango ni mhudumu wa hoteli (siyo Sarah), alibaki ameganda asijue nini kinaendelea.  Mhudumu huyo alikuwa na kifaa cha kufanyia usafi.

“Karibu Mr,” aliongea mhudumu huyo wa kiume.

“Mwenye chumba yuko wapi?” aliuliza Roika.

“Hayupo tayari amekwisha ondoka. Yaani amemaliza muda wake wa kuwa hapa. Ila kuna ujumbe ameuacha hapa mezani, nadhani ni  wako,” aliongea mhudumu huyo huku akimpa Roika bahasha nzuri nyeupe.

Roika alibaki ametoa macho, mapigo ya moyo wake yalianza kumuenda mbio, nguvu zilimuishia, akahisi muda huo ni saa yake ya kufa.

Nini kitafuatia? Usikose kesho

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika ujumbe kupitia ukurasa wake wa...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya kinda wa zamani wa timu...

Afua Suleiman afunguka ‘Utalijua Jiji’ ilivyompa ustaa mjini

NA JEREMIA ERNEST JINA alilopewa na wazazi wake ni Afua Suleiman na hata alipojitupa kwenye ulimwengu wa muziki wa...

Keche: Kundi maarufu Ghana linalowatamani Diamond, Kiba, Harmonize

JIACHIE na Staa Wako, wiki hii tumetua mpaka Accra, Ghana kwa kundi maarufu la muziki nchini humo, Keche linofanya vizuri na ngoma...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -