Tuesday, October 27, 2020

UPENDO KUSHINDA UFAHAMU [31]

Must Read

Tshishimbi atambulishwa kuvaa uzi wa AS Vita

NA MWENDISHI WETU KIUNGO wa zamani wa timu ya  Yanga, Papy Tshishimbi, ametambulishwa katika...

Kaseja: Hatukuwa dhaifu kwa Yanga

NA ZAINAB IDDY NAHODHA wa timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC),  amesema  hawakuwa dhaifu...

Kaze amuibua Zahera, aionya Simba

NA ZAINAB IDDY KOCHA wa zamani wa timu ya Yanga, Mwinyi Zahera, amesema aina...

Ilipoishia jana

“HATA mimi nimependezwa nawe, maana nchi yako ina watoto wengi viongozi, lakini hapa nakuona wewe tu na umeshinda hapa,” alijibu Roika kwa tabasamu pana.

Roika alipojibu hivyo, Shazayi alimtazama sana, dakika moja ilipita wote wakiwa kimya. Roika aliona aibu, akashindwa kuyahimili macho ya Shazayi, akamgeukia mtoto aliyekuwa kitandani kama njia ya kukwepa, asiendelee kutazamwa na mtoto huyo wa rais. Roika aliposema ageuke tena kumtazama Shazayi, Shazayi alishtuka na kujifanya anamungalia mtoto.

SASA ENDELEA

Kitendo hicho kilimuogopesha sana Roika. Lakini akili yake haikuhusisha kitendo hicho na hisia zozote za mapenzi, ingawa moyo wake ulimbishia na kumwambia kuwa kuna kitu kinaweza kuja kutokea kati yake na Shazayi mtoto huyo wa rais.

Dakika moja baadaye Shazayi alimtazama tena Roika na kumuuliza.

“Tunaweza kukutana tena kesho? Napenda kufahamiana zaidi na wewe.”

“Hakuna shida, je, tutakutana hapa hapa?” Roika aliuliza.

“Tunaweza kukutana hapa, lakini tutafuta sehemu nyingine yenye utulivu zaidi ili tuongee.”

“Sawa nitafika,” kwa unyonge Roika alijibu.

Shazayi alimuaga Roika, baada ya kuongea na madaktari, akawaaga watoto na kuondoka pale hospitalini. Msafara huo wa mtoto wa rais uliondoka pale hospitalini saa 11 jioni.

Mtoto wa rais alipoondoka, ndugu na jamaa waliruhusiwa kuingia wodini kuja kuwaona watoto wao. Ikiwa ni 11:30 jioni Roika naye aliwaaga wote pale hospitalini. Alipanda taksi na kurudi mji wa Nuruwani kuna hoteli ya Alashak. Njiani alikuwa akitafakari juu ya maisha yake ni namna gani atakamilisha nia yake ya kumuona Ramona mwanamke ambaye anaamini kwamba hawezi kuishi bila yeye. Huku suala la Biyanah ambaye kwa muda huo anajua kuwa yuko Tanzania likizidi kumuumiza kichwa.

“Inabidi nimwambie Biyanah ukweli, kuwa siwezi kuendelea kuwa naye. Mungu wangu sijui kama atanielewa,” alijisemea Roika.

Baada ya saa moja, Roika alikuwa anawasili hoteli ya Alashak. Mawazo yake yote yalikuwa ni kwa Ramona, alijua tayari Ramona atakuwa amekwisha malizana na wageni wake, wageni ambao yeye alipishana nao asubuhi wakati akitoka chumbani kwake.

Aliposhuka kwenye gari, alipiga hatua kuingia ndani ya hoteli, alipogeuka upande wa kulia, alimuona Ramona  akiwa amekaa bustanini. Aliahirisha kwenda ndani na kumfuata pale bustanini. Ramona alipomuona Roika alimfuata na kumkumbatia. Roika alibaki amesimama kama mtu aliyenyeshewa na mvua, akasita kuizungusha mikono yake kwenye kiuno cha Ramona.

“Mpenzi najua nimekuudhi sana kwa lile tukio la asubuhi nisamehe Roika wangu,” aliongea Ramona ambaye naye alionyesha kuwa amekwisha kunasa kwenye penzi la Roika.

Sauti nzuri ya Ramona ilimfanya Roika kuizungusha mikono yake kwenye kiuno na kumkumbatia vizuri Ramona.

“Ramona mbona hayo tulisha yamaliza asubuhi, wala usijali,” alijibu Roika kwa unyonge kidogo.

Ramona alimtazama Roika kwa macho yale yale yanayomtesa Roika siku zote.

“Roika nakupenda, toka ulipoondoka asubuhi, umeniacha katika wakati mgumu sana. Kwa sasa nimependa kweli. Mwanzo nilianzisha safari ya mapenzi kwa masihala, lakini sasa nakukabidhi moyo na mwili wangu uvifanye upendavyo.”

Maneno hayo yalikuwa mapya  masikioni mwa  Roika hakuwahi kufikiria kama kuna siku atakuja kuambiwa maneno mazuri kama hayo. Ilionyesha kuwa Ramona ameingia rasmi kwenye penzi la Roika.

Baada ya kukumbatiana na kuzungumza machache yaliowaweka katika msingi mzuri wa mapenzi. walikaa chini kuendelea na maongezi mengine. Muhudumu alikuja kuwaletea vinywaji.

Waliendelea kukaa pale bustani, baadae Ramona alimwambia Roika.

“Mpenzi nimekumbuka kitu. Kuna rafiki yangu amekuja kutoka Tanzania. Ni rafiki yangu sana kama ndugu.”

“Waooo kafika lini?” aliuliza Roika kwa tabasamu.

“Kafika jana usiku, wewe ulipolala nje ya hoteli baada ya kuniambia uko hospitalini, yeye alikuwa tayari kashafika na alilala kwangu. Ikiwezekana baadae twende tukamsalimie nataka nikutambulishe rasmi kama mme wangu mtarajiwa,” aliongea Ramona huku akimbusu Roika.

Roika alizidi kufarijika sana hakika alianza kuyaona maisha kwake ni mepesi.

“Nitafurahi kumuona.”

“Roika uliniambia kuna tukio la kigaidi limetokea, ilikuwaje?”

“Basi la abiria limelipuka na kuua abiria wote, na kulikuwa na basi la watoto pembeni, ambalo nalo limelipuka upande wa nyuma. Watoto wengi wamepoteza viungo vyao.”

“Mungu wangu, kwanini hivi lakini,” Ramona aliongea kwa masikitiko makubwa.

“Ndio hivyo tukio limekwisha tokea na watu wameshapoteza maisha yao, inaniuma sana,” alijibu Roika kwa majonzi zaidi.

Ramona alimshika Roika kichwa, akamtazama usoni na kumbusu.

Wakati Ramona na Roika wakiwa pale bustanini, Biyanah mwanamke tajiri mtoto wa bilionea Branko Rumo, alikuwa anaingia pale hotelini akiwa ndani ya gari. Gari ilikwenda kupaki karibu na bustani umbali wa hatua 20 kutoka pale Roika na Ramona walipo. Biyanah aliposhuka aligeuka kushota na baadae akageuka kulia.

Hakuyaamini macho yake, ambayo siku zote huwa yanamuonesha kitu halisi na cha kweli. Kwa macho yake yale yale mawili, alimuona Roika akiwa na Ramona wakiwa wamekaa bustanini na wakati huo Ramona alikuwa akimbusu Roika. Jasho jembamba lilianza kumtoka,  mwili wake ulitetemekea, alishindwa kuhema vizuri akabaki ameganda kama sanamu. Aliamini kuwa yule ni Ramona, kwa kuwa ndio hoteli aliyomkuta, lakini hakuamini kama yule ni Roika mwanaume wa maisha yake, mtu aliyepanga kumpa kila kitu ili aje kuwa mume wake wa ndoa. Alizidi kuyalazimisha macho yake yaendelea kutazama ili kujiridhisha hadi ndani ya moyo wake. Wakati huo Roika na Ramona hawakujua kama Biyanah yuko pale hotelini.

Baada ya kuamini kuwa yule ni Roika Malino mpenzi wake, mtu ambaye mapenzi yao yalianza siku tatu nyuma kabla Roika hajaondoka kwenda Mexico, Biyanah alishikwa na maumivu makali ya moyo, nguvu zilianza kumuishia, hasira zilimshika akatamani kuwasogelea pale walipo. Alipiga hatua kuifuata bustani, lakini alisita baada ya kuona eneo lile la hoteli lina watu wengi. Hasira na maumivu aliyokuwa nayo, aliona kuwa yanaweza kulete madhara makubwa. Hivyo alirudi kwenye gari na kumwambia dereva amrudishe hoteli ya New Bitaika. Alipofika hotelini, hakutaka kuzungumza na walinzi wala wafanyakazi wake. Alijifungia ndani na kulia sana, hasira alizokuwa nazo zilikuwa ni kubwa. Alivitupa vitu vyote vilivyokuwa juu ya dressing table. Alikaa chini na kuendelea kulia.

Maswali kwake yalikuwa ni mengi, maswali ambayo yalionekana kwenda kumpa wakati mgumu zaidi wa kumrudisha Roika katika himaya yake. Alijiuliza mapenzi kati ya Roika na Ramona yameanza lini, kwa nini Ramona hakuwahi kumwambia kuwa ana mpenzi anayeitwa Roika. Na kwanini Roika amkubalie na wakati tayari alikuwa na mpenzi. Kichwa kilimuuma Biyanah, maumivu ya mapenzi yalikuwa ni makubwa kuzidi uwezo wake. Alihisi hadi miguu inawaka moto, safari yake ya kutoka Tanzania kuja Pakistani, aliiona tayari kuwa ina madhara makubwa kwake.

Lengo la Biyanah kuja Pakistani, lilikuwa ni kuja kumuuliza rafiki yake Ramona juu ya ukaribu wake na Roika. Hii ilikuwa ni baada ya Ramona kumtumia picha ikimuonesha akiwa na Roika. Lakini lengo hilo lilikuwa limekwisha kuvunjika kwa kuwa tayari alikuwa amekwisha jionea mwenyewe kuwa Roika na Ramona ni wapenzi. Huku akitokwa na machozi, akilia kama mtoto mdogo, Biyanah alinyanyua simu yake ya mkononi na kumpigia Ramona.

“Ramona nakuomba uje huku hoteli ya Bitaika,” aliongea Biyanah.

“Ahaa Biyanah si ulisema utakuja wewe umebadili maamuzi?”

“Ndio nina shida fulani nataka uje unisaidie.”

“Biyanah hebu njoo wewe basi, halafu kuna kitu fulani kizuri nataka leo ukijue.”

“Naomba unielewe Ramona, naomba uje huku, tena ufike sasa hivi,” aliongea Biyanah na kukata simu.

Ramona akiwa na Roika pale bustanini, alikuwa ametoka kuongea na Biyanah kwa njia ya simu.

“Huyo ndio rafiki yako?” Roika aliuliza.

“Ndio anasema niende hotelini kwake anashida.”

“Nenda upesi.”

“Nakuacha kwa muda nisamehe mpenzi,” Ramona aliongea.

“Usijali nenda kamsikilize.”

“Sawa mpenzi,” alijibu Ramona huku akisimama pale kwenye kiti.

Aliposimama, aliinama tena, akambusu Roika na kuondoka pale bustanini, ambapo alielekea maegesho ya magari na kumuomba dereva wa hoteli, ampelekea New Bitaika Hotel.

Huku nyuma Roika alikuwa na furaha isiyo kifani. Sasa aliamini kuwa anakwenda kuikamilisha safari yake ya ndoa, kati yake yeye na Ramona. Lakini mawazo juu ya Biyanah ndio yaliokuwa yakimnyima raha, kila akifikira dhambi anayomtendea mwanamke huyo, aliumia sana. Alijilaumu sana kwa kumkubalia mwanamke asiyempenda.

Kwa unyonge alisimama pale kwenye kiti na kuondoka bustanini, ambapo alielekea kwenye lifti akapanda kwenda chumbani kwake gholofa ya nne. Baada ya kuoga, alikaa kumsubiria Ramona. Hakujua kabisa kuwa rafiki yake Ramona ndiye Biyanah. Laiti angejua, huenda angekuwa amejipanga kwa hatari yoyote ile.

Akiwa anatazama runinga, alimkumbuka Shazayi mwanamke mzuri mtoto wa Rais wa nchi hiyo. Alikumbuka ombi lake, aliloliomba mwanamke huyo la kumtaka waonane siku ya kesho ili wapate kufahamiana.

“Mh! mimi nifahamiane na mtoto wa Rais? mbona ni jambo gumu kwangu. Naogopa sana, sijui nisiende?” Roika alijisemea.

Ramona alishuka kwenye gari baada ya kuwa amefika hoteli ya New Bitaika. Hoteli aliyokuwepo kipenzi rafiki yake, Biyanah Rumo mwanamke tajiri. Alipiga hatua kuelekea ndani. Wafanyakazi wawili wa Biyanah walimpokea na kumkaribisha. Alipofika chumbani kwa rafiki yake, alimkuta Biyanah akiwa amesimama dirishani akitazama nje.

Nini kitafuatia? usikose alhamisi

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Tshishimbi atambulishwa kuvaa uzi wa AS Vita

NA MWENDISHI WETU KIUNGO wa zamani wa timu ya  Yanga, Papy Tshishimbi, ametambulishwa katika...

Kaseja: Hatukuwa dhaifu kwa Yanga

NA ZAINAB IDDY NAHODHA wa timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC),  amesema  hawakuwa dhaifu mbele ya Yanga, licha ya...

Kaze amuibua Zahera, aionya Simba

NA ZAINAB IDDY KOCHA wa zamani wa timu ya Yanga, Mwinyi Zahera, amesema aina ya mpira unaocheza kwa sasa...

Mtibwa yaitungua Azam Jamhuri, Prisons yazidi kupeta

NA GLORY MLAY TIMU ya Azam FC imepoteza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara jana baada...

KIPIGO CHA PILI MFULULIZO:Sven akalia kuti kavu Simba

Wengine benchi la ufundi watajwa, yeye alia na akina Bocco, Morrison NA WINFRIDA MTOI KOCHA Mkuu...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -