Monday, August 10, 2020

UPENDO KUSHINDA UFAHAMU

Must Read

Klabu zamiminika kuomba kutumia U/Nelson Mandela

NA ASHA KIGUNDULA UONGOZI wa Chama cha Soka Mkoa wa Rukwa (RUREFA), umesema umeanza...

Kipa mpya Azam atamba kumsaulisha Abarola

NA ZAINAB IDDY KIPA mpya wa Azam, David Kissu, ameuahidi uongozi na mashabiki wa...

Yanga: Hatuna mpango na wasugua benchi Msimbazi

NA ZAINAB IDDY UONGOZI wa Yanga, umesema hauna mpango wa kusajili wachezaji wanasugua benchi...

Ilipoishia jana

Kikundi cha kigaidi cha Swaba kilitoa mkanda wa video, kikisema kuwa kinamshikilia mtoto wa Rais, Shazayi binti Galim. Jambo ambalo lilikuwa si la kweli. Mkanda huo ulisema uongo mtupu. Swaba waliamua kutoa uzushi huo kwa maslahi yao binafsi, ikiwamo kuitishia Serikali ya Rais Galim na kuitaka itoe kiasi kikubwa cha pesa na kukipa eneo la Ramadan Kash, lenye visima viwili vya mafuta, eneo lililokuwa linashikiliwa na jeshi la nchi hiyo.

SASA ENDELEA

Serikali ya Pakistani pamoja na  Rais wake Galim Halim, waliiamini taarifa hiyo.  Kwa sababu serikali hiyo ilikuwa imemtafuta binti huyo kwa siku tatu bila manufaa yoyote.

Mikakati na mbinu mbalimbali zilianza kuandaliwa ili kumuokoa Shazayi kutoka katika mikono ya Swaba. Mama yake na Shazayi, mke wa Rais Galim Halim, hakutaka kunyamazishwa, alilia sana usiku na mchana. Akimlilia binti yake wa pekee.

RAMONA

Ramona alikuwa nchini Tanzania akiwa na lengo la kukutana na mama mzazi wa Roika ili kumuomba msamaha, na kumjulisha kuwa mwanawe, Roika hakuwapo tena duniani. Maumivu aliyozidi kuyapata kutokana na kusababisha kifo cha Roika, yalizidi kumnyima raha alijiona ni mtu mwenye hatia kubwa mbele ya dunia.

Akiwa katika msafara wa magari mawili, alikuwa akielekea eneo la Ua Jekundu, eneo lililokuwa mitaa ya Masaki. Huko ndiko alikokufahamu kuwa ni nyumbani kwa mama yake na Roika. Ingawa ilikuwa ni mara yake ya kwanza kukutana na mama Roika, alipanga kuanza kujitambulisha kwanza, kwani hakuwa na hakika kama Roika alishawahi kumueleza mama yake juu ya uhusiano wao.

Alishuka eneo hilo, lililokuwa na nyumba nyingi za matajiri wa jiji la Dar es Salaam, ambapo aliulizia kwa wenyeji wa mitaa hiyo. Kutokana na umaarufu wa Roika na wa marehemu baba yake mzee Malino, mara moja Ramona alionyeshwa nyumba.

Magari ya kifahari yaliegeshwa nje ya nyumba ya mama Roika. Ramona alishuka peke yake na kuwaacha walinzi wake ndani ya magari. Alipiga hatua na kugonga geti. Mlinzi wa getini, hakuwapo nyumbani kwa mama Roika siku hiyo, hivyo aliyekuja kumfungulia mlango ni msichana mzuri aitwaye Dina ambaye ni mdogo wake na Roika. Ramona alishtuka kumuona binti mzuri wa miaka 19 akimfungulia mlango. Moja kwa moja alijua kuwa msichana yule ni mdogo wake na Roika. Dina naye alipigwa na butwaa kumuona mrembo wa dunia kwenye geti la nyumba yao. Alibaki kumtazama kwa muda asielewe kitu.

“Samahani hapa ni nyumbani kwa mama Roika?” aliuliza Ramona kwa tabasamu hafifu.

“Ndio wala hujakosea karibu,” alijibu Dina kwa sauti nzuri na tabasamu pana.

“Je, mama yako yupo?”

“Ndio yupo, karibu.”

Kwa woga mkubwa, Ramona aliingia ndani. Tayari alijiona amekwisha jitoa muhanga, ingawa alizidi kuogopa kupita kiasi, mwili wake ulianza kutetemeka. Machozi yalianza kumtoka kwa siri pindi alipokuwa akimtazama Dina, kwani moyo wake ulizidi kuwa mahakama kuu, ukimhukumu kwa kumuua kaka wa msichana mzuri kama Dina.

Dina alitangulia pindi Ramona alipokuwa akimfuata kwa nyuma. Kwa wakati huo Dina alikuwa akijiuliza maswali mengi asipate kuelewa, alijiuliza kwa nini mrembo huyo wa dunia aje  nyumbani kwao.

Dina hakuwa anafahamu chochote kilichomkuta kaka yake, Roika, kwani mama yake hakumueleza kuhusu ujio wa kaka yake wa kuja kumuomba damu. Alichokuwa anakijua yeye ni kuwa kaka yake alirudi juzi nyumbani kwao, lakini hawakuonana kwani yeye alikuwa ametoka pale nyumbani.

Kwa furaha Dina alimkaribisha Ramona ndani. Ramona alikaa sebuleni, akitazama huku na kule ndani ya sebule. Mbele yake aliziona picha tatu. Picha ya Roika na ya mama yake, pamoja na mdogo wake. Picha hizo zilionyesha uzuri wa familia ile, kwani zilikuwa nzuri na zenye kupendeza.  Machozi yalianza kumtoka Ramona pale pale. Alikichukua kitamba cheupe  kwenye pochi yake na kijifuta. Kwa wakati huo Dina alikuwa amekwenda kumuamsha mama yake aliyekuwa amepumzika,  kwani hali yake kiafya ilikuwa bado haijakaa  vema kutokana na kutolewa damu siku mbili zilizopita.

Dina aliingia chumbani kwa mama yake na kumuamsha.

“Mama kuna mgeni,” aliongea Dina kwa furaha.

“Mgeni?” aliuliza mama Roika huku akishangaa wakati akitoka usingizi.

“Ndiyo.”

“Ni nani?”

“Mmh! Hata mimi imenishangaza, ila toka ukamuone mwenyewe.”

Mama Roika alishuka kitandani kwa uchovu mkubwa, alipiga hatua kuelekea sebuleni, wakati tayari Dina alikuwa amekwisha tangulia.

Macho yalimtoka mama Roika, pindi alipomuona mrembo wa dunia Ramona Fika pale sebuleni. Upesi kichwa chake kilifikiria kwa haraka mambo mengi aliyosimuliwa na mwanawe, kuhusu mrembo huyo na kilichompata Pakistani. Alijiuliza ni nini kilikuwa kimemleta pale nyumbani kwao. Alianza kujawa na woga kwa sababu alimfahamu Ramona kuwa ni mtu hatari. Macho ya Ramona yalimtazama mama Roika kwa woga mkubwa, lakini nafsi yake ilikuwa ikimwambia mara kwa mara kuwa liwalo na liwe. Dina aliyekuwa ameketi pale sebuleni, alishangazwa na tukio la wawili hao kuonana.

Nini kitafuatia, usikose kesho.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Klabu zamiminika kuomba kutumia U/Nelson Mandela

NA ASHA KIGUNDULA UONGOZI wa Chama cha Soka Mkoa wa Rukwa (RUREFA), umesema umeanza...

Kipa mpya Azam atamba kumsaulisha Abarola

NA ZAINAB IDDY KIPA mpya wa Azam, David Kissu, ameuahidi uongozi na mashabiki wa timu hiyo kuwa atajituma na...

Yanga: Hatuna mpango na wasugua benchi Msimbazi

NA ZAINAB IDDY UONGOZI wa Yanga, umesema hauna mpango wa kusajili wachezaji wanasugua benchi katika klabu ya Simba kwa...

TSHISHIMBI KUMFUATA MORRISON SIMBA

NA ZAINAB IDDY KIUNGO wa Yanga, raia wa DR Congo, Papy Tshishimbi, anatarajiwa kumfuata winga wa kikosi hicho, Bernard...

TSHISHIMBI KUMFUATA MORRISON SIMBA

NA ZAINAB IDDY KIUNGO wa Yanga, raia wa DR Congo, Papy Tshishimbi, anatarajiwa kumfuata winga wa kikosi hicho, Bernard...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -