Friday, January 15, 2021

VICHWA VITATU VILIVYOBEBA SIRI UBINGWA YANGA

Must Read

Usiyoyajua sare ya Leicester, United

NI katika mechi ya Ligi Kuu ya England iliyomalizika kwa sare ya mabaon 2-2.-Man United wamemiliki mpira...

Eti Zidane anapangiwa kikosi!

IMEFICHUKA kuwa wachezaji waandamizi wa Real Madrid walikaa kikao na Zinedine Zidane kumwambia wachezaji anaopaswa kuwapanga na...

DIDA ASAINI IHEFU FC

Golikipa wa zamani wa Yanga na Simba, Deogratius Munishi ‘Dida’ amejiunga na Timu ya Ihefu inayoshiliki Ligi...

NA ALLY KAMWE

ACHANA na mechi za kirafiki, nimewatazama Yanga kwenye michezo miwili na kugundua tatizo la kimbinu linalowasumbua kwa sasa.

Dhidi ya Simba na Lipuli, hakuna unachoweza kusifia kwa Yanga zaidi ya uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na si timu kwa ujumla. Hakuna muunganiko mzuri wa kikosi. Ni hatari hii!

Benchi la ufundi chini ya George Lwandamina, wamekuwa wakitumia mfumo wa 4-3-3 ambao kwa namna moja au nyingine unaonekana kuangushwa na wachezaji wawili. Raphael Daudi na Ibrahim Ajib.

Majukumu mengi ya Daudi kwenye mfumo huu yanafanywa na Kamusoko, huku majukumu ya Ajib, yakionekana kuigharimu timu wakati fulani. Kwanini wamefeli hawa?

Kuna mambo mawili katika kulielezea hili. Huenda viwango vya wawili hawa havijakaa vyema bado au hawajakaa vyema kwenye mfumo huu. Yote yanawezekana.

Nini kifanyike sasa? Yanga inahitaji matokeo sasa na hakuna namna wanayoweza kufanikisha hilo kama hawatarekebisha mbinu zao. Iko mifumo mitatu ambayo Lwandamina anaweza kuanza kuitumia kuanzia sasa.

Mfumo wa 3-4-3

Huu ni mfumo mama wa Muitaliano, Antonio Conte. Aliutumia akiwa na kikosi cha Italia, akautumia tena alipotua Stamford Brigde kukinoa kikosi cha Chelsea.

Kwa namna yoyote ile huwezi kuyaelezea mafanikio ya Chelsea msimu uliopita bila kuutaja mfumo huu. Lwandamina anaweza kuutumia pia kulingana na kikosi alichonacho msimu huu.

Kivipi? Twende taratibu hapa.

Mfumo huu unahitaji mabeki watatu nyuma. Mabeki imara wenye utulivu wa kichwa na mwili kwenye kufanya maamuzi. Pale Chelsea, Conte aliwatumia David Luiz, Garry Cahill na Cesar Azpilicueta.

Kwa Yanga, hapa Lwandamina anaweza kumrejesha kikosini Haji Mwinyi, akatengeneza ukuta wa Mzanzibar huyo sambamba na Andrew Vincent ‘Dante’ na Kelvin Yondani.

Kwanini Mwinyi ni faida hapa? Nitakwambia.

Sote tunajua ubora wa Mwinyi anapokuwa kwenye ubora wake. Mbali na uwezo wake wa kupokonya mpira bila kucheza rafu, Haji ana kichwa kizuri cha kuzielewa njia za mpira.

Ni mtulivu pia, kontroo yake iko vyema sana. Kimo chake na upambanaji wake kama akiaminiwa tena, unaweza kusaidia Yanga kuwa na safu imara sana ya ulinzi, akishirikiana na Dante na Yondani.

Upande wa watu wanne wa kati, tukiwa na maana ya viungo wawili na ‘mawing back’ mawili, Yanga ni matajiri kwenye eneo hili.

‘Wing back’ ya kushoto, Lwandamina anaweza kumtumia Gadiel Michael. ‘Wing back’ ya kulia, akachagua apendacho. Iwe Kessy au Juma Abdul, wote ni watu sahihi kwa mfumo huu.

Viungo wa kati ni Papy Kabamba Tshishimbi na Thabani Kamusoko. Faida ya wawili hawa wote ni ‘box to box midfielder’. Wanajua kukaba na kushambulia.

Kwa faida hiyo, Lwandamina anaweza kuwatumia wawili hawa kama ‘Double pivot’. Kama Jose Mourinho anavyowatumia Nemanja Matic na Paul Pogba, msimu huu. Inawezekana hii.

Watatu wa mbele, hapa kunahitaji utulivu kidogo. Mfumo unahitaji watu wawili wenye kasi, pembeni na mkali mmoja mwenye jukumu la kuweka mpira kimiani.

Conte alifanikiwa kwa kuwatumia Eden Hazard, Pedro na Diego Costa. Lwandamina anatakiwa kufanya nini? Rahisi sana.

Anaye Obrey Chirwa, huyu anatosha kucheza kama wingi ya kulia. Donald Ngoma akashambulia kutokea kushoto, kisha kati akasimama Amiss Tambwe.

Chirwa ana kasi na ni mzuri pia kwa kutupia. Iko hivyo pia kwa Ngoma. Ukijumlisha na Tambwe, Yanga wanaweza kuvuna mabao mengi mno kwenye safu hii.

Wakati ambao Gadiel Michael na Juma Abdul wakipanda kuleta balaa kwenye safu ya wapinzani, tayari Yanga itakuwa na watu watatu kwenye boksi. Watakosaje matokeo?

Nje una faida ya Ibrahim Ajib, Raphael Daudi, Said Makapu na Emmanuel Martin, bado Lwandamina atakuwa na chaguzi nyingi za kufanya ili kutafuta matokeo kutoka benchi.

 

Mfumo wa 4-2-3-1

Huu ni mfumo mwingine wa kisasa unaoweza kutumiwa na Lwandamina na ukampa mafanikio. Kivipi? Tunahitaji mabeki wanne wa nyuma.

Juma Abdul, Dante, Yondani na Gadiel Michael wanatosha kabisa kuusimamisha ukuta kwenye mfumo huu. Viungo wawili wa kati ni Tshishimbi na Kamusoko kama kawaida.

Mabadiliko kidogo yatakuja kwenye watu watatu watakaocheza mbele ya viungo wawili na nyuma ya straika mmoja wa mbele. Nitakuelezea pia hapa.

Mfumo utahitaji mawinga wawili na mtu mmoja atakayecheza huru uwanjani, ‘free play maker’. Huyu ni mtu mwenye kujua kumiliki mpira na uwezo wa kutengeneza nafasi na kufunga pia.

Hujamuona Ibrahim Ajib akiwa bora zaidi eneo hili? Pembeni ukawa na Chirwa akitokea kulia na Ngoma akitokea kushoto, huoni faida ya Ajib mwenye jukumu la kuuchezea mpira atakavyo?

Straika wa mbele unamuhitaji Tambwe. Kwanini Tambwe ni muhimu? Labda huenda ukawa unajiuliza hili kwa sasa. Sote tunafahamu ubora na udhaifu wa Tambwe.

Si mzuri pindi timu inapokosa mpira lakini ni hatari zaidi timu inaposhambulia. Mifumo yote miwili niliyoianisha hapo juu, inamhitaji mtu mwenye jukumu la kufunga tu, si kukaba.

Tambwe kama akiwa fiti asilimia 100, ni mtu sahihi mahali hapa. Ni hasara kubwa kuwa na Donald Ngoma kama straika wa mwisho. Ngoma ni mzururaji uwanjani, anapenda kuwepo ulipo mpira, si mzuri kwenye kujitenga na kusubiri nafasi.

Mfumo wa 3-5-2

Huu ni mfumo wa mwisho ninaoutazama kama mwarobaini wa kuitibu safu ya ushambiliaji ya Yanga, msimu huu. Kivipi? Tulia nikueleze hapa.

Mfumo huu unafaida mbili kwa wakati mmoja. Timu inakuwa na nafasi ya kumiliki mpira kwa asilimia kubwa lakini pia wanakuwa imara mno, pindi wakikaba na kushambulia.

Lwandamina anaweza kuwapanga Yondani, Dante na Gadiel Michael kama mabeki watatu wa nyuma. Mabadiliko kidogo yanahitaji kwenye watu watano.

Kimsingi mfumo unahitaji viungo watatu na watu wawili wa pembeni wenye uwezo wa kushambulia. Hapa ningemrudisha Said Makapu kikosini. Kwanini?

Kama tumeifatilia michezo miwili ya Yanga, tunakubaliana kuwa Tshishimbi anaweza kuwa na faida kubwa kama akisogezwa mbele na kupunguziwa jukumu la kukaba. Nieleweke, namaanisha kupunguziwa na kuondolewa kabisa.

Ni vipi kama Lwandamina akiwaacha Tshishimbi na Kamusoko wawe na jukumu la kukontroo mchezo kwa kutengeneza nafasi, huku nyuma akiwawekea Said Makapu kwa ajili ya kuwakabia tu?

Huoni faida ya Makapu kwenye jukumu hilo? Kazi yake ni kuilinda safu ya ulinzi na kuwalinda mafundi wawili mbele yake? Nani haujui ubora wa Makapu kwenye kuchafua?

Wale watu wawili wenye uwezo wa kupandisha timu, ningemuweka Hassan kessy na kushoto ningempanga Emmanuel Martin.

Pale mbele kwenye watu wawili, ningewaanzisha Ngoma na Chirwa. Unajua kwanini Tambwe hafai kwenye mfumo huu? Hapa tunahitaji mastraika wasumbufu, wahangaikaji wenye uwezo wa kutengeneza njia za kufunga kwa viungo wawili wa nyuma yao. Namaanisha Tshishimbi na Kamusoko.

Mifumo hiyo ndiyo inayoweza kuileta Yanga mpya uwanjani na mashabiki wao wakaacha sifa za kipuuzi kwa kuipamba Yanga mpya ya magazetini, isiyoleta matokeo. Naweka kalamu yangu chini.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Usiyoyajua sare ya Leicester, United

NI katika mechi ya Ligi Kuu ya England iliyomalizika kwa sare ya mabaon 2-2.-Man United wamemiliki mpira...

Eti Zidane anapangiwa kikosi!

IMEFICHUKA kuwa wachezaji waandamizi wa Real Madrid walikaa kikao na Zinedine Zidane kumwambia wachezaji anaopaswa kuwapanga na ndiyo maana timu hiyo imeshinda...

DIDA ASAINI IHEFU FC

Golikipa wa zamani wa Yanga na Simba, Deogratius Munishi ‘Dida’ amejiunga na Timu ya Ihefu inayoshiliki Ligi Kuu Tanzania Bara katika kipindi...

JDart Nation wapanga kutawala Africa

CHRISTOPHER MSEKENA MWANAMUZIKI na bosi wa JDart Nation, JDart, amesema miongoni mwa mipango yake kwa mwaka 2021 ni kuhakikisha...

HUJUMA NZITO YANGA

NA WINFRIDA MTOI UONGOZI wa Yanga upo katika harakati za kuhamishia mechi zao zilizobaki za Ligi Kuu Tanzania Bara...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -