Canberra, Australia
HII itakuwa ni mara ya nane kwa wacheza tenisi ndugu, Venus na Serena Williams, kukutana kwenye michuano mikubwa ya mchezo huo.
Jana asubuhi, Serena alimshinda Mirjana Lucic-Baroni na kutinga fainali ya Australian Open, ambayo atakutana na Venus aliyemtoa Coco Vandeweghe.
Serena mwenye umri wa miaka 35, ambaye ni bingwa wa michuano hiyo ya Australian Open mara sita, alimshinda mpinzani wake, Mirjana kwa seti mbili (6-2 6-1).
Sasa atakutana na dada yake, Venus, mwenye umri wa miaka 36, ambaye alimshinda Vandeweghe kwa seti 3-1.
Itakuwa ni michuano yao ya kwanza mikubwa kukutana kati yao, tangu Serena amfunge Venus kwenye michuano ya Wimbledon mwaka 2009.
Hivyo hii itakuwa ni mara yao ya nane kukutana, huku Serena akiwa ameshinda mara sita kati ya hizo.
Serena, ambaye kwasasa ni mcheza tenisi namba mbili duniani ataingia kwenye michuano hiyo kuvaana na dada yake ambaye anashika nafasi ya 13.
Pia atakuwa akisaka taji lake kubwa la 23, ambapo itakuwa ni rekodi kwenye mtandao wa Open Era.