NA KYALAA SEHEYE
WAZAZI wa Shule ya Sekondari ya Kibaha Boys wamempongeza mwanamuziki, Bernad Paul ‘Ben Paul’ kwa nidhamu aliyonayo na kila mmoja kutaka mwanawe kufuata nyayo za staa huyo wa RnB nchini.
Wakizungumza Papaso la Burudani kwa nyakati tofauti wakati wa sherehe za mahafali ya kidato cha nne ya shule hiyo ambayo inasifika kutoa viongozi wengi sana nchini, walimwagia sifa kibao staa huyo kutoka Dodoma.
“Sasa hivi zama za utandawazi unamruhusu mtoto kufanya kitu anachopenda, ila tunatakiwa kusimamia nidhamu za watoto wetu hata kama wanataka kufanya muziki basi wawe na nidhamu, Ben Paul ni mfano mzuri wa wanamuziki wenye nidhamu ya hali ya juu,” alisema mzazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Kikoti.
Jina la Ben Paul lilibuka kwenye mahafali hayo kufuatia nyimbo zake kupigwa wakati wa sherehe hiyo kitu ambacho kiliwakuna wazazi hao na kummwagia sifa kibao staa huyo asiye na makuu.