NA MWANDISHI WETU,
WATU watano wakiwemo wasanii wanne walioongozwa na staa wa filamu za Tanzania, Wema Sepetu, jana walihojiwa katika Kituo cha Polisi cha Kati, Dar es Salaam kwa tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya.
Mbali na Wema, wasanii wengine waliofika kuhojiwa ni pamoja na Khalid Mohamed ‘TID’, Hamidu Chambuso ‘Dogo Hamidu’, Babuu wa Kitaa na mtu mmoja asiyefahamika.
Hatua hiyo imekuja kufuatia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, juzi kutaja majina ya wasanii saba akiwataka kufika katika kituo hicho kutoa maelezo.
Muda mfupi baada ya kufika kituoni hapo, Wema aliwapa taarifa mashabiki wake kupitia huduma yake ya habari inayoitwa ‘Wema Sepetu Mobile Application’ na kusema:
“Hey Guys, nimeshafika eneo la tukio sema waandishi wa habari ni wengi mno… And Guess wat, wooote wananisubiria mimi…. Haiyaaa Dah kwakweli hii ni kudhalilishana…. Will keep you posted. Nitaendelea kuwafahamisha,” aliandika Wema.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa mkoa amemtaka msanii wa Bongo Fleva, Vanessa Mdee, video vixen maarufu Bongo, Tunda na watu wengine wanne kufika kituoni hapo Jumatatu ya wiki ijayo kutoa maelezo baada ya kutuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya.
“Jumatatu wanaopaswa kuwepo ni Omari Sanga, Kashozi, Amani, Halidali Katwila, Tunda hawa wote nawahitaji Jumatatu hapa Central (Kituo cha Kati) akiweno dada yangu kipenzi, Vanessa sisi tunaanza na hawa wanaotumia itatusaidia,” alisema Makonda.
Wasanii ambao hawakufika kituoni hapo ni Rashid Makwilo ‘Chid Benz’, Mr Blue, Rachel, Tito na Sniper ambapo mkuu wa mkoa ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwaweka ndani mpaka siku ya Jumatatu.