NA SALMA MPELI
SHUTI la winga wa Yanga, Emmanuel Martin, almanusura limvunje mgongo kipa wa timu hiyo, Youthe Rostand, katika mazoezi yaliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Wachezaji wa timu hiyo walianza mazoezi ya viungo kabla ya kocha mkuu George Lwandamina kugawa vikosi viwili kwa ajili ya kucheza mechi.
Wakati mazoezi hayo yakiendelea, Martin aliambaa na mpira hadi karibu na eneo la hatari na kumchungulia vizuri Rostand, huku akimdanganya kama anatoa pasi lakini aliamua kupiga shuti kali, kipa huyo bila kutegemea alijirusha kwa lengo la kuokoa na kuangukia mgongo.
Hata hivyo, Rostand alishindwa kuamka kwa takribani dakika tatu akipatiwa matibabu kutokana na kupata maumivu makali.
Vikosi vilipangwa hivi; Rostand, Juma Abdul, Gadiel Michael, Andrew Vicent ‘Dante’, Kelvin Yondani, Thaban Kamusoko, Rafael Daud, Papy Tshishimbi, Donald Ngoma, Ibrahim Ajib na Obrey Chirwa.
Ramadhan Kabwili; Hassan Ramadhan, Fiston Kayembe, Mwinyi Haji, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Pius Buswita, Maka Edward, Said Juma Makapu, Geofrey Mwashiuya, Juma Mahadhi na Matheo Antony.
Yanga inatarajiwa kushuka dimbani kesho kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kucheza na Ndanda katika mechi ya Ligi Kuu Bara.