Saturday, October 31, 2020

Yanga 1-1 Simba, Kelele nyingi, ufundi ‘zero’

Must Read

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya...

NA ERNEST CHENGELELA (OUT)

KAMA kawaida pambano la Yanga na Simba lilikuwa lenye tambo nyingi nje ya uwanja, lakini ndani likashindwa kuthibitisha ubora wake kiufundi, mipango na mbinu.

Ndani ya dakika 26 za pambano hilo tayari maamuzi na nidhamu mbovu zilishaharibu mchezo huo, ambao uliisimamisha Tanzania kwa dakika 90 kutokana na kelele zake, lakini si ubora wake uwanjani.

BINGWA lilikuwepo Taifa kushuhudia pambano hilo na hayo ndiyo mambo ambayo lilijifunza kutoka katika mchezo huo.

Nidhamu bado tatizo

Kadi nyekundu ya Jonas Mkude ni mwendelezo wa nidhamu mbovu uwanjani kwa wachezaji wa soka wa Tanzania ambao wakati mwingine hujisahau na kuziponza timu zao kwenye mechi muhimu.

Licha ya kosa la mwamuzi Martin Saanya kuruhusu bao la Tambwe, Mkude hakuwa sahihi kufanya alichokifanya yeye akiwa kama nahodha wa timu ambayo ilitakiwa kutoka nyuma na kurudi mchezoni, kwa sababu bao lile lilikuwa la mapema sana.

Lakini, mbali na Mkude, wachezaji wengine wa Yanga na Simba waliendelea kucheza soka kama wanazitafuta kadi, mtu kama Novaty Lufunga, Kelvin Yondan au hata Ally Mustapha ‘Barthez’ walipata kadi za njano kizembe sana.

Hivyo, inawezekana mechi imekwisha kwa sare, lakini kama si kadi nyekundu ya Mkude, si ajabu Simba wangeweza kuibuka na ushindi kutokana na kiwango ambacho timu yao inacho kwa sasa kulinganisha na Yanga.

Hakuna shabiki kuna wahuni

Hakuna asiyejua kuwa soka ni mchezo wa kiungwana, lakini huwezi kubisha kuwa juzi Taifa kulikuwa na wahuni na si waungwana, ndiyo maana kikatokea kile kilichotokea.

Baadhi ya mashabiki wanaodaiwa kuwa wa Simba baada ya bao la Amis Tambwe na kadi nyekundu ya Mkude walionyesha vitendo vya kihuni kwa kung’oa viti vya uwanja ambao umejengwa kwa kodi za wananchi, kitu ambacho ni kinyume kabisa na uungwana wa mchezo wa soka.

Kwa matukio yale, itashangaza kuona kama hawatachukuliwa hatua kali kutokana na tabia zao ambazo ipo siku kama hazitafumbiwa macho, zitazua maafa kwenye viwanja vya soka kama ilivyowahi kutokea nchini Misri.

Kichuya anatisha

Shujaa wa Simba kwenye pambano hilo, Shiza Kichuya, aliendelea kuthibitisha kuwa yeye ni moto wa kuotea mbali kwa kuonyesha soka la hali ya juu ambalo liliashiria kuwa miamba hiyo ya Msimbazi haikukosea kumsajili kutoka Mtibwa Sugar.

Ukiacha bao lake alilofunga, Kichuya alikuwa mwiba mkali kwa beki ya Yanga katika sehemu kubwa ya pambano hilo, ambalo lilishindwa kuendana na amshaamsha iliyokuwepo kabla ya pambano.

Jinamizi la Tambwe

Amis Tambwe, licha ya kufunga bao la utata, lakini ameendelea kuthibitisha kuwa moja kati ya makosa makubwa zaidi ambayo klabu ya Simba imewahi kuyafanya baada ya kumtupia virago msimu mmoja baada ya kuwa mfungaji bora.

Jinamizi la kumuacha Tambwe kiutata linaendelea kuitesa Simba, ambayo ameifunga mabao matatu kwenye mechi tatu alizokutana nao tangu atemwe na timu yake hiyo ya zamani.

Jjuuko ana namba yake

Inawezekana Kocha wa Simba, Joseph Omog, akawa anaamini kuwa mabeki wake wa kati, Lufunga na Method Mwanjali ndio bora kwenye kikosi chake, lakini baada ya mechi ya jana anahitaji kukaa chini na benchi lake la ufundi kufikiria upya.

Kwa sababu katika mechi hiyo Lufunga alionyesha udhaifu wa hali ya juu kiasi cha kuthibitisha kuwa Mganda Juuko Murshid anastahili kuanza kwenye kikosi cha kwanza kutokana na kuibadilisha timu wakati alipoingia kipindi cha pili.

Yanga imechoka

Kitendo cha kukosa muda wa kupumzika wakati Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ilipokwisha msimu uliopita, kutokana na kushiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, kumeiathiri Yanga.

Ukiiangalia Yanga kwenye mechi kadhaa ilizocheza msimu huu wachezaji wake wanaonekana kuchoka na kushindwa hata kupambana na Simba, licha ya kuwa pungufu na ndiyo maana juzi ni wachezaji wachache tu wa vijana hao wa Jangwani walitakata.

Na uchovu huu utaendelea kuitesa timu hiyo hadi pale ligi itakaposimama Desemba, mwaka huu, kupisha michuano ya Kombe la Kagame.

Waamuzi jipu

Maamuzi yaliendelea kuwa tatizo kwenye soka la Tanzania na katika mchezo wa juzi mwamuzi Martin Saanya alionekana kushindwa kuumudu mchezo huo, kutokana na kufanya maamuzi kadhaa ya kuzibana timu zote mbili.

Kwanza alishindwa kumuona Tambwe aliposhika mpira na kufunga bao la Yanga, lakini analalamikiwa kwa kukataa bao halali la Simba, na pia alishindwa kumuadhibu Lufunga kwa kadi ya pili ya njano, licha ya faulo nyingi alizomchezea Tambwe.

Maamuzi hayo na mengine mengi ya utata ndiyo yalichangia kuharibu pambano la juzi, ambalo lilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

Hamilton avunja rekodi Ureno

LISBON, Ureno STAA wa mbio za magari Lewis Hamilton, amevunja rekodi ya Valtteri...

Ronaldinho naye ana Corona

RIO, Brazil MKONGWE wa Brazil, Ronaldinho, amethibitishwa ana virusi vya corona. Ronaldinho aliandika ujumbe kupitia ukurasa wake wa...

Sterling amlilia kinda wao Man City

MANCHESTER, England WINGA wa Manchester City, Raheem Sterling, ameandika ujumbe wa majonzi baada ya kinda wa zamani wa timu...

Afua Suleiman afunguka ‘Utalijua Jiji’ ilivyompa ustaa mjini

NA JEREMIA ERNEST JINA alilopewa na wazazi wake ni Afua Suleiman na hata alipojitupa kwenye ulimwengu wa muziki wa...

Keche: Kundi maarufu Ghana linalowatamani Diamond, Kiba, Harmonize

JIACHIE na Staa Wako, wiki hii tumetua mpaka Accra, Ghana kwa kundi maarufu la muziki nchini humo, Keche linofanya vizuri na ngoma...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -