NA SAADA SALIM
BENCHI la ufundi la Yanga limesema timu hiyo inasafiri kwenda Comoro ikiwa na tahadhari kubwa ya kutowadharau wapinzani wao Ngaya FC.
Yanga inasafiri leo kuelekea Comoro kwa ajili ya mchezo wao huo utakaochezwa kesho (Jumapili) Uwanja wa Moroni nchini humo.
Akizungumza na BINGWA jijini jana, Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, alisema wamejizatiti kuhakikisha wanapambana kwa nguvu ili kuibuka na ushindi na kamwe hawawezi kuwadharau wapinzani wao hao.
Alisema rekodi walizonazo zinaonyesha wapinzani wao hao wamefanikiwa kutwaa vikombe vitatu katika kipindi kifupi kilichopita ambazo ni Kombe la Ngazija, Super Cup na Champion Ship.
“Hatujawahi kupata mikanda yao ya video (CD) kwa ajili ya kuwaangalia, kwa hiyo hatujajua mifumo wanayotumia lakini tunaenda na historia yao kwamba wamefanya vizuri kwa msimu uliopita na kushinda vikombe vinne huko kwao,” alisema.
Mwambusi alisema kulingana na historia hiyo waliyopewa juu ya wapinzani wao, wameshtuka na kuhakikisha wako kamili na kuhitaji ushindi mkubwa katika mchezo huo.