NA MWANDISHI WETU
KIPIGO cha mabao 7-0 walichokitoa Simba juzi kwa Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, kimeelezwa kuwa ni salamu tu kuelekea mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Plateau United ya Nigeria.
Mbali ya mechi hiyo dhidi ya Wanigeria hao, Simba wametamba kuwa 7-0 za juzi ni ujumbe tosha kwa wapinzani wao wajao Ligi Kuu Bara, huku wakisisitiza kwa mara nyingine azma yao ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo ya Tanzania kwa msimu wa nne mfululizo ipo pale pale.
Wakitoka kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga, Novemba 7, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Simba juzi walionekana kuwa na hasira ya aina yake iliyowapa ushindi huo mnono jijini Arusha.
Safu ya ushambuliaji ya Simba iliyoongozwa na nahodha John Bocco, Bernard Morrison na Clatous Chama, ilikuwa ni moto wa kuotea mbali kiasi cha kuwatesa vilivyo mabeki wa Wagosi wa Kaya hao.
Hadi kipindi cha Kwanza kinamalizika, Simba walikuwa mbele kwa mabao 5-0.
Akizungumzia ushindi wao huo wa juzi, Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Simba, Barbara Gonzalez, alisema: “Ushindi ule mnono ni salamu kwa Plateau United tutakaokutana nao Ligi ya Mabingwa Afrika na wapinzani wetu wajao Ligi Kuu.
“Kwa sasa timu yetu ipo sawa sawa, kila mchezaji anafahamu nini anatakiwa kufanya kwa maslahi yake binafsi na ya klabu ya Simba. Lengo letu ni lile lile, kutetea ubingwa wetu wa ligi na kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Tunaamini kwa kikosi tulichonacho pamoja na ubora wa benchi la ufundi, lazima tutafanikiwa kwa haya tuliyojipangia.
“Tunachohitaji kutoka kwa mashabiki, wanachama na wapenzi wote wa Simba, ni sapoti yao kwa wachezaji, viongozi na timu kwa ujumla, maana nafahamu sote lengo letu ni moja, kuona kila Mwanasimba anapata furaha kutokana na mafanikio ya timu yetu, kitaifa na kimataifa,” alisema Barbara.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 23 baada ya kucheza mechi 11, huku Wekundu wa Msimbazi hao wakijivunia kuwa na idadi kubwa ya mabao kuliko timu yoyote ndani ya ligi hiyo, ikicheka na nyavu mara 26, wakati Azam wanaofuatia, wana 18.