Friday, December 4, 2020

ZUENA BINT MSASAMBUKO (14)

Must Read

HUJUMA NZITO YANGA

NA WINFRIDA MTOI UONGOZI wa Yanga upo katika harakati za kuhamishia mechi zao zilizobaki...

BEN POL AJA NA HIYO NDIO MBAYA

Na Mwandishi Wetu MSANII nguli wa muziki wa R&B na Bongo Fleva Benham Paul...

ZILE NI SALAM TU

NA MWANDISHI WETU KIPIGO cha mabao 7-0 walichokitoa Simba juzi kwa Coastal Union katika...

ILIPOISHIA JUMAMOSI… “Wasije niswekea mume wangu ndani bure,” mama akachoropoka na kuelekea kule barazani, mimi na wengineo tukifuata nyuma. Tukafika barazani na kuwakuta baba na Mzee Masoud wakiongea, alikuwepo Salehe na Mzee Mazrui, sikujua hata ni nani yao….SASA ENDELEA

Salehe akanitazama kwa huzuni akilitamka neno pole bila kutoa sauti, sikumjibu nikamtazama tu na kugeuza kurudi ndani. Moyo ukitulia angalau.

Nikaelekea chumbani nilikomkuta Mwanahija anambadilishia nguo mtoto wa mdogo wa Farida. Nikakaa kitandani. Dakika nzima nilitulia nikiwaza na kuwazua hicho kilichowaleta. Nimeshapigwa, nimeshaibika sasa nini? Nikajiuliza nisipate jibu Mwanahija alipomaliza shughuli yake akanitazama

“Usiwaze vya polisi wala sijui Salehe sijui vitu gani….uguza madonda hayo kisha  ujue utamuombaje msamaha Madobe.”

“Unadhani atanisamehe?” nikamuuliza Mwanahija kwa huruma utadhani alikuwa ameishikilia akili ya  Madobe mikononi mwake.

“Kama anakupenda atakusamehe tu, ila kama ndio ushamtibua mara nyingi, ndio ulinywe ulilolikoroga,” akanibwagia jibu akinyanyuka na kutoka na mtoto. Niliwaza kumpigia simu Madobe ili nizungumze naye, lakini nikaona ingempa hasira zaidi. Nilipaswa kumfuata na kumuomba masamaha ana kwa ana. Nioge nimfuate. Wazo likapita!

Nusu saa baadaye wote tulikuwa sebuleni tukijadiliana alichosema Mzee Salehe. Alikuwa amemlipa Mzee Khalfani pesa aliyokuwa anadai kama matibabu ya kumtibia bintiye na faini ya kupigwa kwa mwanawe, hivyo kesi ilikuwa imefutwa baada ya kuzungumza naye. Nikapumua nikijiapiza kutorudia ujinga wowote utakaoniweka matatani! Nilimaanisha Salehe ndio basi tena. Hivi tu hatujawa wapenzi nimeshakula ngumi za uhakika, tukiwa wapenzi si nitauawa!

Saa saba mchana nikatoka Kibaha na kuelekea Ubungo anakofanyia kazi Madobe. Kiwanda cha vyombo vya plastiki. Habari za mimi kupigana na Raya sababu ya Salehe zilishaenea. Nilikuwa gumzo mtaani, wengine wakidai nilikuwa ndani polisi, wengine wakisema nimejeruhiwa mahututi siwezi hata kugeuka, wengine wakimjadili Mwanahija na ubabe wake, mradi majina ya watoto wa Msasambuko hayakukauka midomoni wa watu! Tulishazoea, haikuwa mara ya kwanza kwa sisi kuleta habari mtaani!

Wakati nalifikia geti la ofisi ya akina Madobe nilimuona Steve Sikanda, rafiki kipenzi wa Madobe, nikamkimbilia kabla hajalifikia lile geti na kumsabahi.

“Zuena jamani ndio umemfanya nini Madobe sasa,” akanishutuma asiitikie hata ile salamu yangu, nikajua kuna makubwa kuliko nilivyotarajia.

“Angenisikiliza kwanza shemeji nina mengi ya kumwambia,” nikajitetea.

“Yapi?….ya kukutwa na mwanamume uchochoroni ukifanya matusi shemeji, hata mimi sikuelewi,” Steve akaniporomoshea tu asijali walinzi waliovalia sare waliokuwa wanatutazama tu bila kugeuza hata shingo. Umbeya mzigo!

Matusi! Watu wabaya sana, waliniona? Nikajua yameshazushwa marefu kuliko urefu wenyewe. Nikashusha pumzi kwanza na kutikisa kichwa, nguvu zilishaanza kuniishia na maneno yote niliyopanga kujitetea yalinipotea. Wabaya walishajaza sumu, atanielewa?

“Shemeji ukweli naujua mimi, sijali walimwengu wamemjaza maneno gani, naomba nimuone Madobe niongee naye,” nikabembeleza.

“Hapana, rudi tu nyumbani akijisikia kukutafuta atakutafuta kwa sasa utamvuruga zaidi,” Steve akanikata maini. Nikahisi kama ulimwengu mzima aulikuwa ukinizomea. Mshipa wa majuto ukataka kusimama, nikauzuia nikiona hauna maana kwa muda ule.

“Shemeji, maneno yamekuwa mengi mtaani, lakini mwenye ukweli ni mimi, sasa mnapokataa kunisikiliza mimi na kuwasikiliza walimwengu mna maana gani?” nikamuuliza moyo ukiumia kweli kweli.

Akabetua mabega yake kwa kuyapandisha na kuyashusha akibetua na midomo yake kumaanisha hajui. Akageuka na kutaka kuondoka, nikamshika mkono!

“Steve, nakuomba jamani, nisaidie shemeji yangu, nisaidie nimuone Madobe, au hata mwambie niko hapa nje,” nikabembeleza. Steve akanitazama tu kisha akaniambia

“subiri nikamweleze, mngojee hapa nje.”

Nikaketi kwenye jiwe kubwa lililokuwa pembezoni mwa geti la kuingilia kiwandani mle. Walinzi wakinikodolea macho, wengine wakinisemesha hili na lile. Akili yangu haikuwa pale. Nilikuwa nikiwaza namna nilivyovuruga bahati zangu kijinga. Hati ya kiwanja kule Boko ndio nilikuwa naipoteza hivi hivi, bahati ya kuwa na mwanamume nimpendaye nilikuwa naipoteza hivi hivi. Nimeng’ang’ana na mtu ambaye kuwa naye ni kukaribisha vita katika maisha yangu. Ujinga mtupu!

Nikamaliza nusu saa nzima, nikiwaza na kuwazua hakutokea Steve wala Madobe. Hatimaye saa nzima ilipogonga! Steve akatoka na kunifuata pale nje.

“Zuena nenda tu nyumbani,” akanikata maini.

“Amekataa?” nikamuuliza kwa sauti ya kukata tama

“Kapumzike kwanza, nitazungumza naye tukitoka kazini,” akanisihi.

“Yaani amekataa kutoka hata hapa nje wakati nimefunga safari toka Kibaha?” nikalalamika sasa nikihisi kudharaulika mno. Nikasimama!

“Shemeji please! We nenda kapumzike kwanza mpe muda atulize akili sasa hivi utamvuruga zaidi” Steve akajaribu kunielewesha lakini ikawa sawa na kunibembeleza kwa lugha isiyoeleweka. Sikumuelewa!

Tukabishana kwa takribani dakika kumi, nikimuomba anisaidie nimuone Madobe jioni ile naye akikazania kunisihi niondoke. Sikukubali kuondoka, nilijua ningelala na maumivu makali sana. Nikashika simu na kumpigia Madobe, ilikuwa inaita tu bila kupokelewa. Makubwa!

Steve akaniambia alikuwa anarejea ndani, kama nataka kumuona nimngoje Madobe mpaka saa moja kasoro jioni ndio walikuwa wanafunga kiwanda. Nikakubali. Nilikaa kuanzia muda ule wa saa 8 na nusu mpaka saa 12 wafanyakazi walipoanza kutoka mmoja mmoja. Nikangoja tena nusu saa bila kumuona Madobe.

Niseme tu ukweli nilikuwa nimechoka na hasira zilikuwa zinanishika sasa. Wanaume wenye visirani vya kununa wasikie tu, wanaudhi kuliko tumbo la kuhara!

Saa moja kasoro ndio Steve akatoka, akinitazama na kunionyesha kwa kichwa kuwa alikuwa anakuja. Nikasimama na kujiweka sawa. Madobe akatoka na kusimama pale getini akinitazama tu. Madobe wangu! Nikamfuata na kumsabahi wala hakujibu alikuwa akinitazama tu. Nikajua kazi leo ipo!

“Nakusalimia jamani” nikajikomba, yeye wala hakushughulika na mimi, safari hii akimtazama Steve na kumuuliza “hujamwambia nilichokwambia umwambie?”

“Aaah, Mado mambo mengine mnahitaji kuzungumza wenyewe jama!” Steve akajitetea, mimi sasa nikivurugikiwa kabisa. Kuniambia nini?

Madobe akarudisha kichwa kwangu na kunitazama tena kwa mtindo ule ule wa tafakuru! Ghafla tu akasonya na kutikisa kichwa.

“Wanawake sijui mna nini, Zuena mama naomba uende nyumbani, sitaki kukuona na sijisikii kukuona kabisa,” akaongea kwa hasira akinivuruga zaidi, safari hii machozi yalikuwa njiani. Sikutegemea! Madobe? Huyu huyu ananiambia hivi!

 

“Madobe baba sikiliza please…sio vile unavyosikia mtaani, naomba tuongee unisikilize na mimi,” nikajitetea nikimshika mikono. Akaipangua na kuanza kutembea kuelekea kituo cha mabasi. Nikamkimbilia na kumpita. Nikimzuia kwa kusimama mbele yake.

“Madobe mpenzi wangu nakuomba jamani, nisikilize basi.”

“Nikusikilize nini?….hivi aibu uliyonipa jana unategemea nitaamka leo moyo ukiwa mweupe kabisa?…kumpigania mwanamume? Kwamba mimi ni mwanamke mwenzio ama? Lipi ulitaka sikukupa mpaka ukamgombee mwanamume mwenzangu mtaani?….tena nikiwa kwenu?….umefumaniwa na mwenye mali huko ukivuliwa nguo Zuena na ndio chanzo cha kupigwa…..leo unakuja mbele yangu eti nisamehe….mpumbavu wewe sijapata ona….wenzio hata kama wanazunguka huko nje wanawapa waume zao na wake zao heshima sio vile…sio vile Zuena…sio vile mama…nipishe!” akagomba mfululizo akiongea kwa hasira, akanisukumia pembeni. Lilinishuka mara mia! Na kulia nikashindwa.

Moyo ulikuwa unanienda mbio, akili ikikosa cha maana cha kusema. Nikajisimamisha pale kama nguzo, huku nikimtazama namna Madobe alivyokuwa akiishia na rafiki yake. Sikutaka makuu, nilishalikoroga mpaka hapo, nikakitafuta kituo cha daladala, safari ya nyumbani ikaanza.

Saa tatu kasoro niliingia  nyumbani nikiwa nimechoka kupita maelezo. Uchovu ukanipotea baada ya kuliona gari la Salehe likiwa limepaki pale barazani. Nikasimama chini ya mkorosho uliokuwa mbele ya nyumba yetu. Nikiguna na kuguna! Nikachanganya miguu na kuharakia ndani na sikufika….

Salehe alikuwa ameliegemea gari upande ule uliokuwa unatazamana na mlango wa kuingilia kordoni. Nikasimama hapo nikimtazama, akatabasamu na kunisogelea

“Nimekusubiri sana babe na simu umezima Zuena,” akaniduwaza.

“Nini?!” nikamtupia swali lililovaa mshangao nikilishangaa lile jina sambamba na ile kauli kuwa nimezima simu. Nikaitazama simu iliyokuwa mkononi mwangu na kugundua imeisha chaji.

“Zuena!” akaniita akikishika kiganja na mkono wangu wa kuume na kukiweka kifuani pake. Nikagutuka na kuangaza huku na kule hakukuwa na mtu, wauza samaki walishaingia ndani lakini bado mawenge ya kipigo nilichopata yalikuwa hayajanitoka.

“Zuena siogopi macho ya watu sasa…..najua nakupenda….please babe tulia nikupende,” mashairi haya yakazikusanya seli za mfumo wa ashiki na kuziweka sawa. Niliyapenda!  Nikatazama kando nikiimung’unya midomo yangu mithili ya mtu amung’unyae pipi. Nikazinduka!

“Na yule aliyetaka niungane na babu zangu akhera ni nani kwako?” nikamuuliza.

“Zuena baby….nakuapia kwa jina la Mtume sijawahi kuwa na Raya kimapenzi….sijui nisemeje…I mean (namaanisha)…ok she is just a friend (sawa ni rafiki tu)” akajitetea mie nikifaidi zile “dimpoz”, nikifaidi vile alivyokuwa akibembeleza na lugha ile ya Kiingereza na sauti ile….hata ungekuwa wewe raha ungeisikia. Kuna wanaume wamejaaliwa kubembeleza! Sio mtu anakubembeleza utadhani anakusomea matangazo ya vifo!

“So? (kwahiyo?)….why did she beat me? (Kwanini alinipiga)” na mimi nikajitutumua na lugha hii iliyokuja na merikebu mwenzangu ili angalau asijeona anaongea na maimuna.

“Babe sijui….labda ana yake moyoni, …ingia basi kwenye gari tukakae mahali tuongee.” Akaniomba, nami nikiitazama saa na kuona muda hakuniruhusu. Nikakataa. Akaomba tuzungumzie kwenye gari.

Nikadengua dakika kadhaa kisha nikaingia garini. Mwanamke mwenzangu hebu kwanza! Hata kama unampenda mtu kufa kudengua ni haki yako, sio unaambiwa panda kabla hata hajamalizia upande wapi wewe umeshapanda. Ndugu yangu utachokwa….na ukiona mwanamume anataka utii tu kila asemalo na asikubembeleze hata chembe hapana angalia vizuri umeingia wapi pengine umeingia jeshini! Na usisubiri amri ya pili, toka!

 

“Zuena sikiliza mama….unajua nilikupenda tangu nilipokuona first time ulikuwa  unavuka barabara kuelekea kule kituoni….data zako zote nimepewa na Kianga, tatizo maneno ya washikaji mtaani….kuna maneno fulani  kuhusu nyie  yana…”

“Ishia hapo hapo….” Nikamkatiza nikimnyooshea mkono kama trafiki anayesimamisha gari, nikataka kufungua kitasa cha mlango.

“Zuena ngoja kwanza basi….nisikilize bwana,” akabembeleza akinizuia kuufungua ule mlango na hivyo kunishika mwili. Nikasikia raha! Raha mno! Nikageuka tena na kumtazama.

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

HUJUMA NZITO YANGA

NA WINFRIDA MTOI UONGOZI wa Yanga upo katika harakati za kuhamishia mechi zao zilizobaki...

BEN POL AJA NA HIYO NDIO MBAYA

Na Mwandishi Wetu MSANII nguli wa muziki wa R&B na Bongo Fleva Benham Paul 'Ben Pol' ameshukuru mashabiki kwa...

ZILE NI SALAM TU

NA MWANDISHI WETU KIPIGO cha mabao 7-0 walichokitoa Simba juzi kwa Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania...

DEWJI: CHAMA NI SIMBA HADI 2022

Kiungo huyo raia wa Zambia, aliyetoa mchangomkubwakwaSimbakufikisharobo fainaliyaLigiyaMabingwaAfrikamsimuwa 2018/19, ikiwamo kutwaa ubingwa wa LigiKuuTanzaniaBarakwa misimumitatu mfululizo, awali ilidaiwa alikuwa yupo katika hatuayamwishoyakujiunganaYanga.

Sven aruka kihunzi

NA ASHA KIGUNDULA KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, ameruka kihunzi na kuwaachia msala nyota wake, Clatous Chama na...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -