Thursday, December 3, 2020

ZUENA BINTI MSASAMBUKO (26)

Must Read

HUJUMA NZITO YANGA

NA WINFRIDA MTOI UONGOZI wa Yanga upo katika harakati za kuhamishia mechi zao zilizobaki...

BEN POL AJA NA HIYO NDIO MBAYA

Na Mwandishi Wetu MSANII nguli wa muziki wa R&B na Bongo Fleva Benham Paul...

ZILE NI SALAM TU

NA MWANDISHI WETU KIPIGO cha mabao 7-0 walichokitoa Simba juzi kwa Coastal Union katika...

ILIPOISHIA jana … “Shabani umemwambia?” nikamuuliza mama ambaye sasa alitoka pale kizingitini na kuja kuketi pamoja nami pale kitandani. Akatikisa kichwa polepole kuashiria hapana. Roho ikaniuma sana. Mama alikuwa na shida ndogo ndogo nyingi mno na hakuwa na msaada wowote toka kwa wanawe tisa! Kweli si kila mtoto na riziki yake…..SASA ENDELEA…

“Na bado shangazi yako Mama Havijawa yule mwanawe wa mwisho Mkegani….anatoka wiki ijayo tunaanza na ndoweka Alhamisi, gombesugu Ijumaa, Jumamosi mkole, Jumapili mkesha, kuna sare mbili, kuna zawadi, kuna nauli, kuna mchango wa kifamilia kwa ajili ya upishi na mambo chungu nzima….hapa nimedunduliza toka kwenye ususi nina elfu kumi na moja tu….kama unayo kidogo nisaidie nipunguze aibu mwanangu,” Mama akanisomea mahitaji yake, nikachoka mara mbili! Alihitaji kama elfu 50 za kumfanya aheshimike shughulini, bado kulikuwa na mahitaji ya mle ndani. Nikacheka kwanza maana niliona kitanzi shingoni!

Nikawaza na kuwazua, nikakata shauri namfuata Salehe anisaidie kwa chochote. Na nilikuwa na uhakika wa kusaidiwa. Ewe mwanamke mwenzangu kama uliwahi kuwa na mwanamume au uko na mwanamume siku nenda siku rudi hata kitambaa cha mkononi hajawahi kukununulia seuze kukukamatisha pesa ya matumizi yako na bado unamuita mpenzi wako. Zinduka! Hakupendi huyo na kama ni enzi hakukupenda, usimkumbuke kwa lolote!

Wenyewe tunaita kumzika akiwa hai na eda unamkalia. Msinikabe koo! Ameshindwa kukutunza ukiwa peke yako ataweza kukutunza ukiwa na mwanao? Yaleyale ya kulea watoto kama mzazi pekee huku una mwenzio mliyeapishana katika shida na raha! Mambo mengine tuwe tunasoma alama za nyakati jamani!

*********

Saa moja na nusu usiku huu, nikatoka nyumbani, taratibu nikapandisha njia kuelekea kwa Salehe, mawazo ya pesa na mahitaji yote yaliyokuwa yakipishana kichwani mwangu yakatoweka ghafla nilipoingia ndani ya geti la akina Salehe. Kulikuwa na viatu vya kike mlangoni pale. Nikashusha pumzi na kupiga hatua nikiuelekea ule mlango. Nikakinyonga kitasa na kuusukumia mbele ule mlango, ukafunguka kirahisi kabisa.

Nikajitoma sebuleni pale. Taa ilikuwa inawaka na meza ndogo iliyokuwa sebuleni hapa ilikuwa na vinywaji na glasi mbili zilizoashiria uwepo wa watu wawili humo ndani. Salehe na nani? Kianga hakuwepo wiki hiyo hivyo nikamtoa akilini.

Niliingia kwa mwendo wa kunyata moyo nao ukiongeza kasi ya mwendo. Nikasogea mpaka ilipo kordo ya kuelekea vyumbani. Nikautazama mlango wa chumba cha Salehe kwa hofu isiyoeleweka! Nikaupeleka mkono wangu wa kuume kifuani nikikishika kifua na kumeza mate kwa tabu kidogo.

Nikatulia hapo kwa sekunde kadhaa kabla ya kupiga hatua zaidi na kuukaribia mlango. Nikatega sikio, kulikuwa na ukimya wa hali ya juu. Taratibu hali mkono ukitetemeka nikakinyonga kitasa cha mlango na kukisukumia mbele. Mlango ukatii na kufunguka bila kelele. Nikasimama hapo mlangoni miguu ikifa ganzi, akili ikikataa taarifa toka machoni na mikono ikitetemeka. Machozi ambayo sikuyatarajia usiku huo yalinitoka bila kujitambua. Salehe!

Pamoja na yote, pamoja na mapenzi yote Salehe! Pamoja na kujitoa kote huku kwa Salehe bado hakuridhika na mimi. Nilizifunga kope za macho yangu na kuruhusu machozi yabubujike kwa hasira. Mkono uliokuwa umekishikilia kitasa uliteleza polepole na kukiachia kitasa kilichopiga ukelele hafifu wa kufyatuliwa na mkono. Salehe akazinduka toka pale kitandani alipokuwa amelala na Raya. Yule ambaye alimkana siku zote na kujiapiza hakuwa na mahusiano naye leo alikuwa naye kitandani.

“Zuena!” akaita kwa mshangao akiliacha shuka na kuteremka mtupu toka pale kitandani. Sikumsubiri, nikatoka mbio nikirudi pale sebuleni na kuzunguka kama mwehu kwa sekunde kadhaa. Nikauona mlango wa kutokea, nikauwahi na kutoka mbio nikikimbia mpaka nje ya geti na kuanza kukatiza njia kama mwehu, nikilia na nisijitambue ninakoelekea.

Ni nini mwanamume anahitaji ili akupende umpendavyo? Ni nini mwanamume anapewa ili atambue unampenda? Ni kujali gani anakohitaji mwanamume ajue umehiyari mauti kwa ajili yake? Ni nini mwanamume anapewa ili asikupe maumivu kama haya aliyonipa Salehe jamani?…. Nikayakumbuka maneno ya shangazi, mwanamume ni kama mzigo wa haja kubwa, usipomtua kwa uzito wake utamtua kwa harufu yake!…..

********

Ingawa alinijia na kila neno la kuombea msamaha nilishindwa kumsamehe, akajieleza yote kuwa anahisi Raya alimtilia dawa katika kinywaji na akajikuta akifanya yale bila kujielewa. Sikumuamini wala sikutaka kumpa nafasi ya kuniaminisha hayo yote.

Salehe akanitumia ujumbe kuwa kuyaepuka maumivu ya kuachana kwetu asingependa tuonane tena maishani mwetu. Na kama ni kuagana nimuone siku hiyo anieleze ukweli wa moyo wake! Sikwenda wala sikumtafuta, alishaniliza na kuniumiza sana na safari hii niligoma kumsamehe!

Mwezi umepita tangu yote yale yatokee, nikajitafutia na kibarua cha kutembeza vitu kilichonishinda wiki mbili tu, na ndipo simulizi yangu ilipoanzia, na ndio leo hii naletewa na hizi taarifa kuwa Salehe anaoa tena anamuoa Raya!

Nina mambo mawili ya kukiri, la kwanza likiwa ni kumpenda Salehe mno, namaanisha kupitiliza, na kule kugoma kumsamehe nilitaka aonje maumivu yangu na nilitaka nijue angenililia kiasi gani kumbe ndio nilikuwa nachanganya mahesabu! La pili, ni siri niliyoiweka moyoni kwa takribani wiki tatu sasa. Siri ambayo sikujua hata nianzie wapi kuisema. Nilikuwa na ujauzito wa Salehe, safari hii nikiwa na uhakika kuliko uhakika wenyewe, hapa napo nilichanganya mahesabu!

Sasa umejua nilikotoka na huyu Salehe, umenijua ndani nje, umejua kwanini nilipopewa zile taarifa niliwehuka ghafla na kuhamanika na kwanini niliita hali ile MTIHANI!….. sasa umejua hali ya hatihati niliyonayo… wiki tatu zijazo Salehe anaoa na anamuoa Raya!

Hivi kweli Salehe hakunipenda kabisa hadi kufikia hatua ya kumuoa mbaya wangu Raya?

********

JAKAMOYO! Usiku ulikuwa mrefu kupitiliza. Unaposikia mtu analalamika siku yake ilikuwa ndefu usidhani siku yake ilikuwa na masaa 28! La hasha! Mzunguko wa kichwa chako ndio unaweza kukufanya uione siku ina masaa ya mwaka mzima. Kwa wakati huu usiku kwangu ulikuwa sawa na kuimaliza nusu karne. Niligeukia kushoto nikageukia kulia, nikaketi kitandani nikatoka na kwenda msalani kule uwani nisiogope hata ule usiku mnene. Moyo ulitembelewa na hamaniko lililosindikizwa na Jakamoyo!

Sala ya alfajiri ilinikuta macho, nikiwa nimelala chali, nikiukunja mkono wangu wa kushoto na kuufanya egemeo la kisogo changu. Niliitazama dari bila kuitambua akilini, nikashusha pumzi ndefu hali nikiziachia kwa sauti mdomoni mithili ya mtu anayepiga mluzi. Nikajigeuza na kulala kiubavu nikikitazama chumba hiki kana kwamba nilikuwa mgeni kwa usiku huu. Akili yangu ilikuwa mbali, maili nyingi toka pale nilipokuwa.

Mimba! Nilikuwa na mtihani mkubwa wa namna ya kuanza kuwaeleza kuwa nilikuwa na mimba nyingine. Ningeonekana mwehu, hapana, ni hayawani ama pengine punguani, nilishaumwa na nyoka ilinishinda nini kuuogopa hata unyasi na kuniepusha na balaa kama hili? Kufanya kosa si kosa, kosa ni kurudia kosa na mimi ndio nilishalirudia kosa. Nilijuta! Lakini majuto kama shibe huja baada ya kushiba!

Salehe Masoud! Mtihani wa pili, nilikuwa bado nampenda mno, yumkini moyo wangu ulikuwa bado ukisusuika juu yake na sasa alikuwa ameamua kunimaliza na taarifa za ndoa yake. Muda huu mfupi tuliotengana ndio afikie hatua ya kuoa kabisa?…mbona muda aliokaa nami hakuwahi hata kuzungumzia ndoa? Sikumfaa? Sikumpendeza? Ama sikuwa moyoni mwake kabisa? Maswali yalikosa majibu, nikaumia moyo mno, nikitamani kuche upesi nimtafute nimuulize, na nimwambie alikuwa ameniachia kiumbe chake tumboni. Angeniamini? Potelea mbali. Nikahitimisha!

Madobe Fungamlango! Jitimai ilinivaa, mtihani wa tatu mgumu. Ningeanzia wapi kumueleza kuwa nilikuwa nina ujauzito wa mtu mwingine. Ningeanzia wapi kumueleza moyo wangu ulikuwa kwa mtu mwingine baada ya miaka yote tuliyokuwa pamoja na mapenzi yote aliyonionyesha na yote mema aliyonitendea, hivi kweli Madobe alistahili malipo kama haya.

Ningeanzia wapi kumueleza sikuwahi kumpenda kwa dhati muda wote huu ila mazoea ndiyo yaliyotuweka pamoja. Niliumia, niliumia sana na safari hii sikuweza kuyazuia machozi yasinitoke. Nimefanya nini hiki? Mtego gani huu? Dhambi gani hii ninayotaka kuichuma mbele ya Muumba kwa kumtendea hivi Madobe. Nikalia kwa kwi kwi nisijali hata watoto walioanza kuamka na kunisogelea pale kitandani.

 

Itaendelea kesho

 

- Advertisement -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisement -

Latest News

HUJUMA NZITO YANGA

NA WINFRIDA MTOI UONGOZI wa Yanga upo katika harakati za kuhamishia mechi zao zilizobaki...

BEN POL AJA NA HIYO NDIO MBAYA

Na Mwandishi Wetu MSANII nguli wa muziki wa R&B na Bongo Fleva Benham Paul 'Ben Pol' ameshukuru mashabiki kwa...

ZILE NI SALAM TU

NA MWANDISHI WETU KIPIGO cha mabao 7-0 walichokitoa Simba juzi kwa Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania...

DEWJI: CHAMA NI SIMBA HADI 2022

Kiungo huyo raia wa Zambia, aliyetoa mchangomkubwakwaSimbakufikisharobo fainaliyaLigiyaMabingwaAfrikamsimuwa 2018/19, ikiwamo kutwaa ubingwa wa LigiKuuTanzaniaBarakwa misimumitatu mfululizo, awali ilidaiwa alikuwa yupo katika hatuayamwishoyakujiunganaYanga.

Sven aruka kihunzi

NA ASHA KIGUNDULA KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, ameruka kihunzi na kuwaachia msala nyota wake, Clatous Chama na...
- Advertisement -

More Articles Like This

- Advertisement -